Miradi ya UN yagusa maisha ya wakulima Tanzania

24 Oktoba 2018

Leo ni siku ya Umoja wa Mataifa ambapo pamoja na mambo mengine tunaangazia kile ambacho chombo hicho chenye wanachama 193 kinatekeleza kule mashinani ili kuboresha maisha ya wananchi.

Miradi inayotokelezwa na shirika la chakula na kilimo duniani FAO nchini Tanzania kwa lengo la kuongeza tija kwenye kilimo, imesaidia wakulima siyo tu kuondokana na njaa bali pia kuboresha lishe na kuinua kipato.

Akihojiwa na Stella Vuzo wa kituo cha habari cha Umoja wa Mataifa nchini Tanzania, Mwakilishi mkazi wa FAO nchini humo Fred Kafeero ametolea mfano wa mradi wa kilimo kinachohimili tabianchi ambao unatekelezwa mkoani Kagera.

Amesema “ni kwa kutambua kuwa tabianchi inabadilika kwa hivyo kubadili pia mbinu za kilimo ili wakulima nao waendeleze uzalishaji wao na wapate kipato. Kwa hivyo tuna mradi huo ambao unaendana na ainisho la kilimo ukijumuisha mazao, mifugo na uvuvi ambapo tunafanya kazi na wakulima wa vijijini, wanawake na vijana  na kuwawezesha kufanya maamuzi ya kile wanachotaka kupanda na wanataka kupanda vipi. Lakini pia kuleta mfumo wa mashamba darasa ambako wanaweza kujifunza na kubadilisha ujuzi miongoni mwao.”

Manufaa ya miradi ya FAO yamefikia pia wakazi wa wilaya ya Kibondo, mkoa wa Kigoma nchini Tanzania ambako wimbi la wakimbizi limeibua changamoto ya chakula kwa wenyeji.

FAO imetoa mafunzo ya kilimo bora kinachohimili tabianchi kwa lengo la kutokomeza njaa na kuinua kipato ambapo miongoni mwa wanufaika ni Lucy Lugano, mwakilishi wa kikundi cha wakulima walipokea mafunzo ya awali kutoka FAO.

Ameshukuru Umoja wa Mataifa akisema  "kwa kutuwezesha kupata mafunzo ya kilimo kinachohimili mabadiliko ya tabianchi, lakini pia matumizi ya vipimo kwenye kupanda mbegu. Hata hivyo tuna changamoto, kwani hatuna mbolea kwa hiyo tunaomba mtujengee uwezo kwa kutukopesha hasa vikundi vya wanawake."

 

 

 

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter