Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Saratani ikigundulika mapema inatibika na kupona hivyo upimaji ni muhimu sana: WHO

Wadau wa afya serikalini na wafadhili kwenye kongamano la kwanza la taifa la saratani nchini Kenya.
UN News Nairobi/Thelma Mwadzaya
Wadau wa afya serikalini na wafadhili kwenye kongamano la kwanza la taifa la saratani nchini Kenya.

Saratani ikigundulika mapema inatibika na kupona hivyo upimaji ni muhimu sana: WHO

Afya

Saratani ni muiongoni mwa magonjwa yasiyo ya kuambyukiza ambayo tyanakatili Maisha ya mamilioni ya watu kila mwaka, ndio maana shirika la afya la Umoja wa Mataifa WHO na wadau wengine wa kupambana na saratani wanapigia upatu upimaji wakiamini kwamba siku zote kinga ni bora kuliko kuponya, kwani saratani ikigundulika mapema inatibika na mgonjwa kupona.

Kenya kama yalivyo mataifa mengine duniani ugonjwa wa saratani ni chanzo cha vifo vingi na kwa kutambua hilo hivi karibuni kumefanyika kongamano la kwanza la kitaifa la saratani jijini Nairobi ili kuwaleta pamoja wadau wakiwemo serikali, watalaam. Mashirika mbalimbali na manusura wa ugonjwa huo.

Shirika la Umoja wa mataifa la idadi ya watu duniani na afya ya uzazi , UNFPA, limeiunga mkono serikali ya Kenya kwa kuchangia kwenye uzinduzi wa chanjo ya virusi vya human papilloma, HPV, kununua na kusambaza mashine za vipimo vya saratani pamoja na elimu kwa wahudumu wa afya ya uzazi.

Changamoto ya saratani Kenya

Saratani za masuala ya afya ya uzazi ni pamoja na ile ya mfuko wa uzazi, shingo ya kizazi, na matiti ambazo huwaathiri wanawake wengi Kenya.

Lucy Njeri Kariuki ni mama wa watoto watatu na aliugua saratani ya matiti na kupona.

Safari ya kutibu saratani ilikuwa ngumu na ndefu kwa Lucy Njeri Kariuki. Matibabu yake na vipimo vikuwa ghali sana.Kwa mara ya kwanza nchini Kenya, watalaam na mashujaa waliogua saratani walikutana mwanzoni mwa Februari mwaka 2023 kwenye kongamano lililofanyika jijini Nairobi kubadilishana mawazo.

Lucy anamshukuru Mola kwa kumvusha salama kwenye safari ya kutibu saratani na anasema,’’Nilijifunza kuwa na shukrani maishani.Na kila siku ina baraka zake.Kuwa na siku njema sio kitu cha kawaida, ni baraka. Tulikuwa wengi lakini wengine wanashindwa na safari ila Mungu ni mwema na niko hapa. Nimetibiwa hapa hapa Kenyatta na kunywa dawa. Hatufanani kwahiyo dawa huwa na matokeo tofauti kwa kila mtu. Kuna wale ambao zinawakubali na wengine mambo hayaendi vizuri wanaaga. Mambo ya kuishi na kufa ni ya Mungu.”

Maonyesho ya bidhaa za kupambana na saratani kwenye kongamano la kwanza la taifa la saratani nchini Kenya.
UN News Nairobi/Thelma Mwadzaya
Maonyesho ya bidhaa za kupambana na saratani kwenye kongamano la kwanza la taifa la saratani nchini Kenya.

Saratani inagunduliwa kuchelewa

Mada kuu ya kongamano hilo la kwanza la kitaifa la saratani ilikuwa ni kusema kwa kauli moja na kuchukua hatua.

Takwimu za wizara ya afya ya Kenya zinaashiria kuwa kiasi cha nusu ya wagonjwa wa saratani wanagunduliwa katika hatua za mwisho za kuugua. Kimsingi ni muhimu kupimwa mara kwa mara ili kuijua hali halisi.

Thomas Lindi ni mwanachama wa bodi ya taifa ya mashirika ya kupambana na saratani, KENCO na anausisitizia umuhimu wa kupimwa kila wakati na ujumbe wao ni,”Tunasisitiza watu waweze kupata matibabu mapema,yaani kinga ni bora kuliko tiba. Matumizi ya bidhaa kama tumbaku ambayo imebainika kuwa inauongeza uwezekano wa kupata saratani ni vitu ambavyo wananchi wanapaswa kujitenga navyo.”

Taasisi ya kitaifa ya saratani nchini Kenya, NCI, kwa ushirikiano na wadau muhimu ndio wenyeji wa kongamano hilo la kwanza la saratani.

Dhamira ni kuwaleta pamoja watalaam kujadili mbinu mujarab za kupambana na saratani.

Wadau katika vita dhidi ya saratani Kenya

Shirika la Umoja wa mataifa la idadi ya watu duniani,UNFPA, ni moja ya washirika wa karibu wa serikali ya Kenya katika vita dhidi ya saratani.UNFPA inayohusika na masuala ya afya ya uzazi imekuwa mstari wa mbele katika mapambano dhidi ya saratani za masuala ya uzazi ambazo zinaipa sekta ya afya ya Kenya mzigo mkubwa.

UNFPA ilizipiga jeki juhudi za wizara ya afya ya Kenya mwaka 2013-2015 kwa kuzindua katika kaunti ya Kitui majaribio ya mpango wa chanjo dhidi ya virusi vya Human Papilloma HPV, vinavyoaminika kusababisha saratani ya shingo ya kizazi.

Mwakilishi wa UNFPA nchini Kenya Anders Thomsen anaelezea kuwa hatua zimepigwa japo kazi bado ipo hasa ikizingatiwa kuwa,”Idadi ya wanaochanjwa bado ni ndogo.Ningependa kuona ikiongezeka.kwa sasa ni 10%. Sababu ni kuwa ni mchanganyiko wa watu kutotaka kuchanjwa kama ilivyojitokeza wakati wa janga la COVID kwani walipata maelezo ya kupotosha. Hata hivyo hii ni hatua nzuri.Tuna imani kuwa tukiwa na serikali hii mpya ambayo imeahidi kuajiri wahudumu wa afya wa ziada katika kaunti zote, tunaamini tutaweza kutumia nguvu hizo kusambaza ujumbe kuwa chanjo ni bora na inaokoa maisha.”

Bango la taasisi ya saratani. nchini Kenya.
UN News Nairobi/Thelma Mwadzaya
Bango la taasisi ya saratani. nchini Kenya.

Saratani ni ya tatu kwenye orodha ya vyanzo vya kifo

Kadhalika, UNFPA, imeunga mkono juhudi za kuwapa mafunzo wahudumu wa afya mintarafu vipimo na tiba ya mapema na pia kuchangia katika ununuzi na usambazaji wa mashine muhimu kwenye vituo vya msingi vya afya kote nchini.

Saratani inaripotiwa kuwa ya tatu kwenye orodha ya vyanzo vya vifo nchini Kenya.

Kulingana na ripoti ya saratani nchini Kenya ya mwaka 2022/23 aina tano za saratani ambazo ni za matiti,shingo ya kizazi, korodani, umio na non-Hodgkins lymphoma husababisha kiasi cha nusu ya wagonjwa wote wa saratani nchini. Wizara ya afya ya Kenya inasema,saratani za shingo ya kizazi na matiti ambazo ndizo zinazoathiri afya ya uzazi, zinachangia 23% ya vifo vinavyosababishwa na saratani nchini Kenya.

Lucy Njeri Kariuki aliugua saratani ya matiti na akapona na anayasifia matibabu aliyoyapokea humu nchini. Kwa mtazamo wake,”Saa hii pale Kenyatta(hospitali ya rufaa ) wamejaribu kuna madaktari wengi na kliniki tofauti. NHIF (Bima ya taifa ya afya) ilinilipia vizuri. Serikali pia imejaribu, hapa kwenye chuo kikuu cha Kenyatta wamefungua kituo cha saratani .Pale kuna vyombo vya kisasa vinavyosaidia katika matibabu ya saratani.Kwahiyo naona kwa miaka kadhaa inayokuja tutaleta India hapa Kenya kwa maana huduma hizo zilikuwa zinapatikana pekeyake India.”

Elimu kuhusu saratani ukizingatia vichocheo vya uwezekano wa kuipata,athari za uvutaji wa sigara, umuhimu wa lishe kamili yote ni mambo ya kupewa uzito.John Sitienei ni mzee wa asili wa jamii ya Talai ya Wakalenjin na anaamini kuwa mabadiliko ya mfumo wa maisha yamechangia katika ongezeko la wagonjwa wa saratani na suluhu iko kwenye elimu na,”Tunataka wizara ya afya iwafundishe wazee kwa kila wadi au kata wazee wawili na mama mmoja.Hawa watu ni wa kujitolea ila wafunzwe na wawezeshwe ili waweze kuielimisha jamii.”

Teknolojia ni muhimu katika kubaini saratani

Teknolojia ina mchango muhimu katika vita dhidi ya saratani hasa ukizingatia vipimo vya mapema ili kuanza tiba mujarabu.

Mary Karanja ni muuguzi ambaye sasa anauza mashine za vipimo vya afya na anasisitiza kuwa ni muhimu kujua mapema ikiwa uwezekano wa kupata saratani upo kupitia vipimo maalum kwani,”Mashine ambazo tunauza zinatusaidia katika kutambua kama mtu ana uwezekano wa kupata saratani.Hii mashini ya inbody S10 inaweza kukuonyesha jinsi misuli ilivyo hasa ya mgonjwa na kuashiria awamu ya ugonjwa.Kama afya yake imedhoofika,misuli inaendelea kuathirika na inaweza kuwa na maana kuwa anaugua saratani au ugonjwa mwengine."

Kwa mujibu wa shirika la afya la Umoja wa Mataifa WHO saratani ikigunduliwa mapema inatibika na mhusika kupona na kuendelea kuishi maisha ya kawaida.