Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mashine za kisasa zinazoratibiwa na IAEA nchini Tanzania zaboresha utoaji huduma kwa wagonjwa wa saratani

Mradi wa IAEA wa kusaidia tiba dhidi  ya saratani katika nchi za kipato cha chini na kati umesaidia mataifa kutekeleza mipango mahsusi ya kutibu saratani
IAEA
Mradi wa IAEA wa kusaidia tiba dhidi ya saratani katika nchi za kipato cha chini na kati umesaidia mataifa kutekeleza mipango mahsusi ya kutibu saratani

Mashine za kisasa zinazoratibiwa na IAEA nchini Tanzania zaboresha utoaji huduma kwa wagonjwa wa saratani

Afya

Mamia ya wanawake nchini Tanzania wameanza kunufaika na upatikanaji wa huduma bora zaidi za saratani ya shingo ya kizazi baada ya kufungwa kwa mashine za kuimarisha kiwango cha juu cha dozi HDR katika Taasisi ya Saratani ya Ocean Road (ORCI) jijini Dar es Salaam, mashine ambazo zinayoratibiwa na IAEA.

Taarifa iliyochapishwa katika tovuti ya IAEA imeeleza kuwa tangu kufungwa kwa mashine hiyo mwezi Oktoba mwaka jana 2022, IAEA imekuwa ikiendesha mafunzo na uundaji wa mfumo wa kupanga matibabu ili kuhakikisha matumizi ya mashine hiyo ni salama na yenye ufanisi.

Taasisi ya Saratani ya Ocean Road au ORCI, pamoja na Kituo cha Tiba cha Bugando (BMC) kilichopo mkoani Mwanza magharibi mwa Tanzania ni vituo viwili pekee vya kutolea huduma za saratani nchini Tanzania.

Kwa mujibu wa Daktari Shaid Omari Yusuph, mwanafizikia wa matibabu katika Taasisi ya Ocean Road, ambayo iko chini ya Wizara ya Afya ya Tanzania Tanzania inakabiliwa na ongezeko la wagonjwa wa saratani katika kipindi cha miaka mitano iliyopita “Lakini tangu kuzinduliwa kwa mfululizo wa miradi ya IAEA, vituo vya kutolea huduma za saratani jijini Dar Es Salaam na Bugando vimeshuhudia ongezeko kubwa la uwezo wao wa kutoa huduma kwa wananchi na idadi ya wagonjwa wanaodhibitiwa kila mwaka.”

Naye mkurugenzi wa Idara ya Afya ya Binadamu ya IAEA May Abdel-Wahab amesema huduma hii mpya ya Brachytherapy ni sehemu muhimu katika matibabu ya aina hii ya uvimbe, na shirika lao limejitolea kutoa msaada wa kiufundi kwa nchi hiyo ili kuimarisha mpango wao wa brachytherapy.

“Tunatarajia kuendelea kushirikiana na mamlaka za Tanzania na wataalamu wa afya kwa ajili ya kuboresha na kupanua huduma ya tiba ya mionzi nchini humo".

Kuhusu mashine za Brachytherapy

Katika nchi ya Tanzania saratani inashika nafasi ya tano kwa kusababisha vifo vya wanaume na ya pili kwa wanawake.

Saratani zinazosababisha vifo hivyo ni pamoja na saratani ya shingo ya kizazi, saratani ya matiti, saratani ya tezi dume na saratani nyingine za uzazi, ambazo hukabiliana vyema na dozi inayotolewa na mashine mpya iliyofungwa (HDR brachytherapy).

Mashine hiyo ya HDR Brachytherapy inahusisha matumizi kidogo cha mionzi kilichofunikwa na kuwekwa moja kwa moja ndani au karibu eneo linalotakiwa kutibiwa, hatua hiyo huruhusu kipimo cha juu cha mionzi kuingia moja kwa moja ndani ya uvimbe ambapo huangusha dozi kali nje ya uvimbe.

Matumizi ya aina hii ya matibabu kwa ujumla ni mdogo, unaolenga eneo husika kwenye viuvimbe vidogo vilivyopata mionzi vizuri na hupunguza athari za mionzi kwenye tishu zingine.

“Kwa pamoja, BMC na ORCI sasa wana uwezo wa kutibu wagonjwa wengi wa saratani ya shingo ya kizazi kwa siku kwa kutumia brachytherapy, na mafunzo yaliyotolewa na IAEA yametuwezesha kuanzisha tiba ya mionzi ya 3D, tiba ya mionzi ya intensity-modulated na njia zingine bora zaidi," alisema Dk Yusuph na kuongeza kuwa “Katika mwaka 2022, huduma za brachytherapy zimetolewa katika hospitali za BMC na ORCI kwa wagonjwa zaidi ya 340 wa saratani ya shingo wa kizazi."

Saratani ya shingo wa kizazi nchini Tanzania

Kwa mijibu wa shirika la Global Cancer Observatory, saratani ya shingo ya kizazi huathiri zaidi ya wanawake 10,000 kwa mwaka nchini Tanzania.

Hadi hivi karibuni, wagonjwa wengi wa saratani nchini Tanzania walikuwa wanapewa rufaa kwenda kliniki za kibinafsi nje ya nchi kwa ajili ya usimamizi zaidi, ikiwa ni wastani wa wagonjwa 80 wanaopewa rufaa kwa mwaka kwa gharama ya karibu Dola milioni 2 kwa Serikali ya Tanzania.

Kupitia mfululizo wa miradi na ushirikiano wa kiufundi wa IAEA katika miaka minane iliyopita, msaada umepanuliwa kwa ORCI na BMC ili kuzipa hospitali vifaa vinavyohitajika na kujenga uwezo wa kibinadamu kupitia programu mbalimbali ili kuwezesha wananchi kupata huduma za uchunguzi na kuwezesha matibabu kwa wagonjwa wa saratani.

Hivi karibuni Tanzania imeomba kujiunga na mpango wa IAEA wa Rays of Hope, ambao utaimarisha udhibiti wa saratani nchini.