IAEA imeazimia kusaidia Afrika kutibu vyema saratani

4 Januari 2019

Shirika la Umoja wa Mataifa la nishati ya atomiki, IAEA limechukua hatua kusaidia mataifa 28 ya Afrika ambayo hayana hata mashine moja ya kutibu saratani. Lengo la IAEA ni kuhakikisha kuwa inabadili mwelekeo wa ugonjwa huo ambao mwaka 2012 kulikuwa na wagonjwa wapya 847,000 barani  humo na idadi inatarajiwa kufikia milioni 1.4 mwaka 2030. Taarifa zaidi na John Kibego.

Saratani ni tatizo linalokua kila  uchao barani Afrika, wakati huu ambapo licha ya idadi ya wagonjwa kuongezeka nchi 28 hazina hata mashine za kutibu ugonjwa huo, jambo ambalo shirika la nishati ya atomiki, duniani, IAEA, linataka kubadili. Shaukat Abdulrazak ni mkuu wa Idara ya Afrika, IAEA.

“Tunasaidia nchi wanachama kwa kuzipatia fursa za mafunzo na pia kupitia mpango kushirikiana na serikali kununua pamoja vifaa vya kudhibiti saratani. Na pia tunaweza kushughulikia suala la usalama na miundombinu. “

IAEA  inasema huduma ya mionzi ni mojawapo ya mbinu muhimu za kudhibiti saratani ikitolea mfano Zambia ambayo mwaka 2007 ilianzisha kitengo chake cha kwanza cha kutibu ugonjwa huo na sasa ina mpango wa kuwana kitengo cha pili.

Serikali ya Zambia inakiri kuwa bila IAEA, isingaliweza kuwa na kituo hicho chenye vifaa vya hali ya juu.

Msaada wa IAEA umesaidia pia  mafunzo kwa wahudumu wa afya nchini Zimbabwe kwa lengo la kuboresha usalama na tija kwenye huduma dhidi ya saratani. Hali hii imeongeza idadi ya wagonjwa wanaopata huduma za msingi dhidi ya saratani.

Dkt. Ntokozo Ndlovu ni Mhadhiri katika Idara ya sayansi za afya ya Chuo Kikuu cha Zimbabwe.

“Tulipokuwa hatuna huduma za kutosha za mionzi, wagonjwa wengi hawakuwa na mbadala. Na si kwamba huduma za mionzi zimeimarika, bali pia kiwango cha ubora wa mionzi ambayo tunapatia wagonjwa kimeongezeka.”

 

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter