Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kutoka kutumikishwa kitumwa hadi mfanyabiashara ajitegemea: Asante ILO

Mafunzo ya kilimo cha mbogamboga huko Surkhet katika Mkoa wa Karnali, Nepal. Shughuli zinasaidiwa na Mradi wa BRIDGE 2021.
©ILO/ILO BRIDGE.
Mafunzo ya kilimo cha mbogamboga huko Surkhet katika Mkoa wa Karnali, Nepal. Shughuli zinasaidiwa na Mradi wa BRIDGE 2021.

Kutoka kutumikishwa kitumwa hadi mfanyabiashara ajitegemea: Asante ILO

Ukuaji wa Kiuchumi

Nchini Nepal mradi wa BRIDGE unaotekelezwa na shirika la  Umoja wa Mataifa la kazi duniani, ILO umewezesha familia moja ya kimaskini kuondokana na sio tu kutumikishwa kwenye ajira za kitumwa bali pia kuepusha baba wa familia kuondokana na kwenda nchi za nje kusaka vibarua.

Shanti Devi Lohar, mama wa familia mwenye  umri wa miaka 50. Akifungua redio kujiburudisha akiwa anauza mboga mboga huko Bajura nchini Nepal.
ILO Video
Shanti Devi Lohar, mama wa familia mwenye umri wa miaka 50. Akifungua redio kujiburudisha akiwa anauza mboga mboga huko Bajura nchini Nepal.

Tuko wilaya ya Bajura magharibi mwa Nepal barani Asia, tunakutana na Shanti Devi Lohar, mama wa familia mwenye  umri wa miaka 50. Akifungua redio kujiburudisha akiwa anauza mboga mboga na maboga huku akikumbuka maisha yalivyokuwa awali. 

Shanti anasema mume wangu amekwenda India kusaka kibarua kutokana na hali mbaya ya kifedha ya familia yetu. Peke yangu nyumbani ilikuwa vigumu kupata kazi. Fedha ilikuwa changamoto kwani hatukuwa na ardhi. 

Punde anapata mteja na anauza boga moja kwa dola tatu. Msingi wa biashara hii ni nini? 

Shanti anasema “nilibaini kuwa kituo cha rasilimali watu kilikuwa kinaanzisha mafunzo ya kilimo cha mboga mboga nje ya msimu husika wa mazao hayo kwa wafanyakazi waliokuwa wanatumikishwa. Nilijiunga ili nipate mafunzo ya kilimo na niwe mfanyabiashara ninayejitegemea.” 

Mafunzo yalifanyika na kisha Shanti alimweleza mumewe ambaye alimtumia mtaji wa dola 343 wa kuanzisha kilimo biashara cha mboga mboga. ILO na mdau wake waliwapatia makaratasi ya nailoni ya kuezekea bustani hizo, madumu ya kumwagilia pamoja na mbegu. 

Faida ni dhahiri na anasema kwa kuuza viazi faida ni kati ya dola 86 hadi 129 kwa mwaka. Mapato kutokana na kuuza nyanya ni kati ya dola 258 hadi 300.” 

Ingawa watoto wake wa kiume wanasoma bweni na gharama ni dola 429 kwa mwaka, Shanti hana tena hofu kwani anapata fedha hizo kupitia kilimo biashara na binti zake wawili wanasoma shahada ya kwanza. Na zaidi ya yote anachofurahia Shanti ni kwamba mumewe hatokwenda tena nje ya Nepal kusaka kibarua.