Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tetemeko la ardhi latikisa Nepal, UN waanza usaidizi

Wafanyakazi wa UNICEF wakipakia vifaa vya msaada kwenye lori linaloelekea Wilaya ya Jajarkot.
© UNICEF
Wafanyakazi wa UNICEF wakipakia vifaa vya msaada kwenye lori linaloelekea Wilaya ya Jajarkot.

Tetemeko la ardhi latikisa Nepal, UN waanza usaidizi

Msaada wa Kibinadamu

Kufuatia tetemeko kubwa la ardhi lililokumba jimbo la Karnali nchini Nepal, jana Ijumaa jioni kwa saa za huko, mashirika ya Umoja wa Mataifa yameongeza juhudi za kutoa misaada ya kibinadamu kwa jamii zilizoathirika. Kufikia sasa, zaidi ya watu 130 wamethibitishwa kufariki na mamia ya wengine wamejeruhiwa kutokana na tetemeko hili la ardhi la ukubwa wa 6.4 kwenye vipimo vya Richter. 

Kwa mujibu wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Masuala ya Kibinadamu (UN OCHA), jimbo la Karnali la magharibi mwa Nepal lilitikiswa na tetemeko la ardhi saa 11.47 jioni kwa saa za huko jana Ijumaa. 

Kitovu cha tetemeko la ardhi kinasemekana kuwa Ramidanda katika wilaya ya Jajarkot, ambayo iko takriban kilomita 65 kutoka Surkhet, mji mkuu wa mkoa wa Karnali. 

Mitetemo ya tetemeko la ardhi ilisikika katika majimbo ya mbali ya magharibi na Lumbini huko Nepal pamoja na mji mkuu wa India, New Delhi. 

Kwa mujibu wa taarifa za awali, watu 133 wamethibitishwa kufariki katika jimbo la Karnali. Mamia ya wengine wamejeruhiwa. Idadi halisi ya majeruhi huenda ikawa kubwa zaidi, kwa kuwa watu wengi walikuwepo majumbani mwao wakati tetemeko hilo la ardhi likitokea. 

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataiafa la Afya Duniani (WHO) Tedros Adhanom Ghebreyesus ametoa salamu za rambirambi kwa waathirika wa tetemeko la ardhi katika jimbo la Karnali. 

Ghebreyesus ameihakikishia Serikali ya Nepal kwamba shirika la Umoja wa Mataifa liko tayari kukidhi mahitaji ya haraka ya afya na kurejesha mahitaji hayo. 

Nyumba zilizoharibiwa na tetemeko la ardhi la kipimo cha 6.4 lililopiga magharibi mwa Nepal tarehe 3 Novemba. Picha kwa hisani, Prakash Kumar Shahi, Afisa wa Sheria, Manispaa ya Bheri, Jajarkot
Kwa hisani: Pak Shahi, Afisa wa Sheria, Manispaa ya Bheri, Jajarkot

Juhudi za uokoaji na misaada 

Kwa mujibu wa taarifa zilizopatikana, kazi ya utafutaji na uokoaji inaendelea na kuna hofu kuwa watu wamefukiwa chini ya vifusi vya majengo yaliyoporomoka imeelezwa. 

Katika baadhi ya maeneo, barabara zimefungwa kutokana na maporomoko ya ardhi baada ya kutokea kwa tetemeko hilo la ardhi, jitihada za kuzifungua zinafanyika. 

Jajarkot na Rukum ni miongoni mwa wilaya zilizoathirika zaidi, na zikiwa katika maeneo ya mbali, mifumo ya mawasiliano ni dhaifu, na kuleta changamoto katika shughuli za uokoaji na misaada. 

Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF) limesema nyenzo za msaada zilizotayarishwa kabla zimetumwa Jajarkot na Rukum, na msaada wowote unaowezekana utatolewa kwa watoto hao na familia zao katika siku zijazo. 

UNICEF: Watoto hatarini zaidi

Alice Akunga, Mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF) nchini Nepal, amesema kuwa watoto na familia zao wako hatarini zaidi, kutokana na kupoteza makazi yao, shule na vituo vya afya.

Makadirio yanaonesha kuwa maelfu ya watoto wenye umri wa kwenda shule wanaishi katika maeneo yaliyoathiriwa na wataathirika.

"Kiwango kamili cha uharibifu kitafahamika zaidi katika siku zijazo na cha kusikitisha ni kwamba idadi ya walioathirika huenda ikaongezeka," amesema katika taarifa yake, akiongeza kuwa timu za UNICEF ziko kwenye eneo husika, kutathmini athari na kutoa msaada wa haraka, ikiwa ni pamoja na blanketi na turubai.

"Tunapima usaidizi wanaohitaji katika wakati huu muhimu katika maeneo ya afya, lishe, elimu, maji, usafi wa mazingira na usafi, ulinzi wa watoto na ulinzi wa kijamii," Bi Akunga amesema.