Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Dengue na Chikungunya yatia hofu, Zika kuna unafuu – WHO

Wahudumu wa afya wakifanya operesheni ya kunyunyizia dawa ya kutokomeza mbu aina ya Anopheles. Mbu huyu ndiye aenezaye ugonjwa wa Malaria.
WHO
Wahudumu wa afya wakifanya operesheni ya kunyunyizia dawa ya kutokomeza mbu aina ya Anopheles. Mbu huyu ndiye aenezaye ugonjwa wa Malaria.

Dengue na Chikungunya yatia hofu, Zika kuna unafuu – WHO

Afya

Hii leo shirika la Umoja wa Mataifa la afya ulimwenguni, WHO limetoa mwelekeo wa magonjwa ya Dengue, Chikungunya na Zika duniani, ambapo kwa Dengue idadi kubwa ya wagonjwa imeripotiwa Sudan, huku hofu ikiongezeka kutokana na kuenea kwa Chikungunya katika nchi za Amerika ya Kusini ilhali kwa Zika kuna nuru kwani idadi ya wagonjwa imepungua. 

Taarifa hizo ni kwa mujibu wa ripoti iliyotolewa leo mbele ya waandishi wa habari mjini Geneva, USwisi na wataalamu wa WHO ambao ni Dkt. Raman Velayudhan na Dkt. Diana Rojaz-Alvares. Magonjwa hayo yote yanaenezwa na mbu. 

Dengue inasambaa kila mwaka 

Dkt. Velayudhan amezungumzia dengue akisema katika miongo ya karibuni umesambaa duniani na idadi ya wagonjwa ikiongezeka kutoka 505,430 mwaka 2000 hadi milioni 5.2 mwaka 2019. 

“Ukanda wa Amerika umeripoti wagonjwa milioni 2.9 na vifo 1280 mwaka 2022. Mwelekeo huu unaendelea mwaka huu wa 2023 kwani hadi mwisho wa mwezi Machi mwaka  huu, kumeripotiwa wagonjwa 441,898 na kati yao hao 119 wamefariki dunia,” amesema Dkt. Velayudhan. 

Hofu kubwa ni kusambaa kwa kasi huko Bolivia, Paraguay na Peru. 

Mabadiliko ya hali ya hewa ni moja ya sababu za hatari zinazosababisha ongezeko la maambukizi mengine.
© UNICEF/Alfredo Zuniga
Mabadiliko ya hali ya hewa ni moja ya sababu za hatari zinazosababisha ongezeko la maambukizi mengine.

Kwa upande wa Ulaya mtaalamu huyo amesema mbu wanaoeneza dengue na Chikungunya wameripotiwa katika nchi 24 na kwamba magonjwa hayo yamekuwa yakiripotiwa kwenye ukanda huo mara kwa mara tangu mwaka 2010. 

Idadi kubwa ya wagonjwa imeripotiwa pia Sudan ambako tangu mwezi Julai mwaka 2022 wagonjwa 8239 wameripotiwa na kati yo hao 45 wamekufa. 

Ingawa hivyo amesema hawajapata takwimu kutoka Asia lakini mwelekeo unatia hofu kubwa. 

Sababu za kuenea kwa magonjwa hayo ni pamoja na mienendo ya misafara ya watu na bidhaa, kukua kwa miji na changamoto zinazoibuka za ukosefu wa  maji na huduma za kujisafi na kuendelea kusambaa kwa mbu kwenye maeneo na nchi nyingine zaidi. 

Chanzo kingine kinachohusiana na tabianchi ni ongezeko la unyevunyevu kwenye mazingira, ongezeko la viwang ovya joto na uhaba wa maji nao ni mazingira bora kwa mazalia ya mbu. 

Ugonjwa wa dengue una chanjo moja na mbili ziok kwnye hatua za mwisho za majaribio na kwamba kwa sasa WHO imepeleka timu za kiufundi kwenye nchi husika ili kudhibiti milipuko na kuimarisha ubadilishanaji wa taarifa mipakani. 

Mbu aina ya anopheles waambukizao malaria wakiwa katika maabara ya taasisi ya KEMRI/CDC nje ya mji wa Kisumu nchini Kenya
Sven Torfinn/WHO 2016
Mbu aina ya anopheles waambukizao malaria wakiwa katika maabara ya taasisi ya KEMRI/CDC nje ya mji wa Kisumu nchini Kenya

Chikungunya yabisha hodi ambako haikuweko 

Kuhusu chikungunya, Dkt. Diana Rojaz-Alvares amesema hofu kubwa ni kwamba ugonjwa unazidi kusambaa bara la Amerika hasa kwenye maeneo ambayo awali haukuweko. 

“Hofu nyingine ni kwamba misafara ya watu imeanza tena na hivyo kuna hatari ya kuenea kwa maambukizi katika maeneo ambayo awali hayakuwa na ugonjwa huo.” 

Kwa sasa WHO inashirikiana na nchi husika kujenga uwezo wa maabara kwenye uchunguzi na pia utekelezaji wa miradi ya kuua mazalia ya mbu ambapo WHO inasema mtu anaweza kujikinga kwa kuepuka kung’atwa na mtu huyo aina ya aedes nyakati za mchana. 

Mbu aina ya aedes aegypti ambaye anaeneza ugonjwa wa zika, bila kusahau dengue na chikungunya
IAEA
Mbu aina ya aedes aegypti ambaye anaeneza ugonjwa wa zika, bila kusahau dengue na chikungunya

Zika idadi inapungua 

Wakizungumzia zika, wamesema kwa sasa duniani kote maambukizi yamepungua tangu mwaka 2017. 

Mwaka 2016 wagonjwa wasiozidi 600,000 waliripotiwa, mwaka 2017 50,000 na 2018 30,000, idadi ambayo inaonekana ni wastani tangu wakati huo. 

Mwaka huu pekee wagonjwa 3,000 wameripotiwa huko Amerika hususan Brazil, Bolivia, Guatemala, Belize na Colombia. 

Duniani kote nchi 89 na maeneo zina wagonjwa au ziliwahi kuwa na wagonjwa wa Zika unaoenezwa na mbu aina ya Aedes.