Mbu dume anayeeneza Zika, Dengue na Chikungunya kupigwa mionzi ili wasizaliane

14 Novemba 2019

Kufuatia kitendo cha mataifa mengi zaidi kutaka kutumia mbinu ya kutumia mionzi ili kuondoa uwezo wa mbu kuzaliana na hivyo kudhibiti magonjwa kama vile dengue, chikungunya na zika, imesababisha mashirika ya Umoja wa Mataifa na wadau kuandaa mwongozo mpya kuhakikisha kuwa mbinu hiyo inakuwa salama na fanisi.

Taarifa ya WHO iliyotolewa hii leo huko Geneva, Uswisi inasema kuwa mbinu hiyo ijulikanayo kwa kiingereza Sterile Insect Technique, kwa kifupi, SIT, ni aina ya njia ya uzazi wa mpango kwa wadudu  ambapo mchakato wake unahusisha kuwafuga katika eneo maalum mbu dume kisha kuwapiga mionzi ya kuondoa uwezo wa kuzalisha mayai na halafu wanaaachiliwa porini ili wakutane na mbu jike. Na kwa kuwa hawana uwezo wa kuza, idadi ya wadudu hao baada ya muda inapungua.

Mradi malum wa utafiti na mafunzo kwa magonjwa ya kitropiki, TDR na shirika la nishati ya atomiki duniani, IAEA kwa ubia na shirika la chakula na kilimo duniani, FAO na lile la afya WHO wameandaa mwongozo huo kwa mataifa ambayo sasa wanataka kutumia mbinu ya kufanya tasa madume ya mbu aina ya Aedes wanaosababisha ugonjwa wa Zika, Chikungunya na Dengue.

Nusu ya wakazi wa dunia wako hatarini kupata dengue.

Wakati mwongozo huu unaandaliwa, Dkt. Soumya Swaminathan ambaye ni mwanasayansi mkuu wa WHO amesma kuwa, “nusu ya wakazi wa dunia wako hatarini kuambukizwa ugonjwa wa dengue na licha ya harakati zote bora zilizofanyika, na juhudi za sasa za kudhibiti bado hazijawa na mafanikio. Tunahitaji sana mbinu mpya na mpango huu unatia matumaini na unahamasisha.”

WHO inasema kuwa katika miongo ya hivi karibu ni, visa vya homa ya dengue vimeongezeka kwa kiasi kikubwa kutokana na mabadiliko ya kimazingira, ukosefu wa usimamizi bora wa miji, usafirishaji na ukosefu wa mbinu toshelezi na endelevu za usimamizi wa kuenea kwa wadudu.

UNICEF/Ueslei Marcelino
Huko Recife nchini Brazil, mama akiwa na mwanae mwenye umri wa miezi 4 ambaye alizaliwa na kichwa kidogo,ugonjwa usababishwao na kirusi cha Zika kinachoenezwa na mbua aina ya aedes aegypti.

Hivi sasa milipuko ya dengue inatokea katika maeneo mengi, hususan bara la Asia ambako Bangladesh ndio inaoongoza zaidi kwa kuwa mlipuko mbaya zaidi wa dengue tangu iripoti ugonjwa huo mwaka 2000. Tangu mwezi Januari mwaka huu Bangladesh imekuwa na wagonjwa zaidi ya 92,000 ambapo kila siku wagonjwa ni 1,500 na hii ni moja ya nchi ambayo imeonesha nia ya kutumia mbinu hiyo ya kuwaondoa mbu dume uwezo wa kutaga mayai yanayoweza kuzalisha mbu wengine.

Magonjwa kama vile malaria, dengue, zika na chikungunya ambayo huenezwa na mbu, huchangia asilimia 17 ya magonjwa yote ya kuambukiza kote duniani na kusababisha vifo vya watu zaidi ya 700,000 kila mwaka.

Mlipuko wa zika huko Brazil mwaka 2015 ulihusishwa na ongezeko la idadi ya watoto wanaozaliwa na vichwa vidogo.

Mbinu mpya imekuwa na mafanikio dhidi ya mazao na mifugo

Teknolojia ya SIT ilibuniwa kwa mara ya kwanza na Wizara ya Kilimo ya Marekani na imekuwa na mafanikio makubwa katika kulenga wadudu waharibifu wa mazao na mifugo. Hivi sasa inatumika katika sekta ya kilimo kwenye mabara 6.

Kwa mantiki hiyo mwongozo wa matumizi ya mbinu hiyo dhidi ya wadudu wanaosababisha magonjwa kwa binadamu, unapendekeza kupitishwa kwa mfumo ambao unaruhusu kwanza majaribio ya ufanisi wake na ufuatiliaji wa ufanisi katika kudhibiti kuenea kwa magonjwa. Halikadhalika inatoa mapendekezo ya uzalishaji wa kiasi kikubwa cha mbu dume tasa, ushiriki wa serikali, jamii na kupima athari za muda mrefu za mbinu hizo.

 

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud