Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Je wafahamu ugonjwa wa chikungunya?

Mbu aina ya Aeded aegypti ambaye anaweza kusambaza zika, dengue au chikungunya
IAEA/Dean Calma
Mbu aina ya Aeded aegypti ambaye anaweza kusambaza zika, dengue au chikungunya

Je wafahamu ugonjwa wa chikungunya?

Afya

Ugonjwa wa chikungunya kwa mujibu wa shirika la Umoja wa Mataifa la afya ulimwenguni, WHO ni ugonjwa unaonezwa na mbu jike aina ya Aedes aliyebeba virusi vya chikungunya. WHO kupitia ukurasa wake wa kuchambua magonjwa inasema kuna spishi mbili za Aedes zinasambaza ugonjwa huo ambazo ni Aedes aegypti na Aedes albopictus. Spishi hizi mbili zinaweza pia kusambaza magonjwa mengine yanayoenezwa na kama vile dengue. Mbu hawa hung’ata nyakati za mchana, ingawa wanaweza pia kung’ata asubuhi na alasiri.

Mlipuko wa kwanza Tanzania: Asili ya Chikungunya ni kimakonde

Kwa mara ya kwanza duniani ugonjwa huu ulibainika wakati wa mlipuko kusini mwa Tanzania na ndio chanzo cha jina hilo Chikungunya kwani kwa kimakonde humaanisha kujikunja na kuelezea kuelezea hali ya mgonjwa kujiinamia na kujikunja kutokana na maumivu ya viungo.

Ugonjwa huu umejikita zaidi barani Afrika na Asia, ingawa wagonjwa wengine wameripotiwa Ulaya na Amerika kutokana na mienendo ya watu kusafiri kutoka maeneo yenye ugonjwa kwenye maeneo hayo ambako ugonjwa huo haukuweko. Zaidi ya wagonjwa  zilizoagizwa kutoka nje zimerekodiwa katika Kanda ya Ulaya ya WHO na Kanda ya Amerika.

Zaidi ya wagonjwa milioni 2 wameripotiwa duniani kote tangu 2005 kwani WHO inasema ugonjwa huo umethibitka katika zaidi ya nchi 110 barani Asia, Afrika, Ulaya na Amerika.

Dalili za Ugonjwa wa Chikungunya

Dalili kuu za chikungunya ni homa ya ghafla ikiambatana na maumivu ya viungo. Dalili nyingine za kawaida ni maumivu ya misuli, kichwa, kichefuchefu, uchovu na kutoka vipele. Maumivu ya viungo yanachosha kwani hudumu kwa siku hadi wiki chache.

Dalili huonekana kati ya siku 4 na 7 baada ya mgonjwa kung’atwa na mbu aliyebeba vimelea vya chikungunya. Kwa ujumla dalili nyingi hudumu kwa siku 2 hadi 3 na ni nadra sana mtu kufa kwa chikungunya.

Mama na binti yake huko Barranquilla, Colombia. Mamlaka za kitaifa zinapita nyumba kwa nyumba ili kudhibiti mbu wanaoweza kubeba Zika, Dengue na Chikungunya.
PAHO/WHO Joshua E. Cogan
Mama na binti yake huko Barranquilla, Colombia. Mamlaka za kitaifa zinapita nyumba kwa nyumba ili kudhibiti mbu wanaoweza kubeba Zika, Dengue na Chikungunya.

Mgonjwa anaweza kupona lakini kwa wazee huweza kusababisha kifo

Wagonjwa wengi hupona kikamilifu, lakini wakati mwingine maumivu ya viungo yanaweza kudumu kwa miezi kadhaa au hata miaka. Matukio ya mara kwa mara ya matatizo ya jicho, mfumo wa mishipa ya fahamu na moyo yameripotiwa, pamoja na malalamiko ya utumbo.

Matatizo makubwa si ya kawaida, lakini ugonjwa huo unaweza kuchangia sababu ya kifo kwa wazee. Mara nyingi dalili za watu walioambukizwa huwa hafifu na huenda maambukizi yasitambuliwe au kutambuliwa kimakosa katika maeneo ambayo homa ya dengue pia hutokea.

Hakuna tiba wala chanjo: Ni kukabili dalili

Hakuna tiba mahususi dhidi ya virusi vya chikungunya na hakuna chanjo iliyoko sokoni dhidi ya chikungunya. Hata hivyo chanjo kadhaa zinatengenezwa kwa sasa.

Kinachofanyika iwapo mtu anapata chikungunya ni matibabu ya kupunguza dalili, pamoja na kupunguza maumivu.

Hii inafanikiwa kwa kiasi kikubwa kwa kutumia dawa za kushusha homa na kupunguza maumivu na zile za kupunguza maji mwilini.

antipyretic ili kupunguza homa, kwa kuboresha matumizi ya dawa za maumivu na mgonjwa kuwekewa maji.

Aspirini na dawa zingine za kupunguza maumivu na uvimbe hazipaswi kutumiwa hadi pale itakapothibitishwa kuwa mgonjwa hana dengue, kwani akipatiwa bila taarifa mahsusi mgonjwa anaweza kupata tatizo la kutokwa na damu.

Kinga thabiti: Kuondokana na mazalia ya mbu

Kinga na udhibiti hutegemea sana kuondoa mazali ya mbu. Na wakati wa milipuko ya ugonjwa dawa za kuua wadudu zinaweza kunyunyiziwa kuua mbu wanaoruka, halikadhalika kuwekwa kwenye maeneo ya mazalia ya mbu kwenye makazi ya watu ili pia kuua viluilui vya mbu.

Mavazi nayo ya kufunika mwili yatumike kupunguza uwezo wa mbu kung’ata, halikadhalika dawa za kupaka kwenye ngozi.

Kwa wale wanaolala wakati wa mchana, hasa watoto wadogo, wagonjwa au wazee, vyandarua vyenye viuatilifu vina uwezo wa kuwalinda. Dawa za mbu za kuchoma na mashine za kutoa unyevunyevu wenye dawa nazo zinaweza kutumiwa ndani ili kuu mbu.