Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

WHO na Kenya zahaha kudhibiti Chikungunya huko Mombasa

Mbu aenezae malaria na magonjwa mengine kama chikungynya. Picha:WHO

WHO na Kenya zahaha kudhibiti Chikungunya huko Mombasa

Nchini Kenya, harakati bado zinaendelea kudhibiti mlipuko wa homa ya Chikungunya huko Mombasa ambako hadi sasa watu 27 kati ya 154 wamethibitishwa kuambukizwa ugonjwa huo.

Shirika la afya duniani, WHO nchini humo linashirikiana na serikali kudhibiti mlipuko huo wa ugonjwa huo unaoenezwa na mbu ambao umekumba vitongoji vyote sita vya Mombasa ambavyo ni Mvita, Kisauni, Nyali, Changamwe, Jomvu na Likoni.

Dalili za ugonjwa huo ni pamoja na homa kali na maumivu ya viungo, misuli, kichefuchefu na uchovu.

Nimezungumza na Nollascus Ganda afisa wa WHO masuala ya dharura nchini Kenya na kumuuliza ni kitu gani sasa shirika hilo linafanya..

(Mahojiano kati ya Flora Nducha na Nollascus Ganda wa WHO- Kenya)

Dalili za ugonjwa huo ni pamoja na homa kali na maumivu ya viungo, misuli, kichefuchefu na uchovu.

Mwakilishi wa WHO nchini Kenya Dkt. Rudi Eggers amesema wanachofanya hivi sasa ni kuipatia serikali msaada wa kiufundi na usaidizi wa kufuatilia hali ilivyo ili kudhibiti mlipuko.

Mathalani kuna afisa wa dharura aliyeko Mombasa akisaidia jopo la serikali kufuatilia hali ilivyo.

Ripoti za awali kabisa za kuwepo ugonjwa huo wa Chikungunya zilipatikana katikati ya mwezi uliopita ambapo kilichofuatia kilikuwa ni kukusanya sampuli za damu na kuziwasilisha maabara kwa ajili ya uchunguzi.

Ugonjwa wa Chikungunya unaweza kwa kuchukua hatua kadhaa ikiwemo kuhakikisha mazingira ni masafi ili kuepusha mazalia ya mbu.