Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Uzalishaji wa nafaka unaboreka Sudan wakati uhaba wa chakula ukiendelea: FAO

Kituo cha Ufadhili wa Uagizaji wa Chakula Ulimwenguni (FIFF)
FAO
Kituo cha Ufadhili wa Uagizaji wa Chakula Ulimwenguni (FIFF)

Uzalishaji wa nafaka unaboreka Sudan wakati uhaba wa chakula ukiendelea: FAO

Ukuaji wa Kiuchumi

Wakati uhaba wa chakula ukiendelea nchini Sudan, uzalishaji wa nafaka umeimarika kwa kiasi kikubwa Kaskazini Mashariki mwa Afrika, limesema shirika la Umoja wa Mataifa la chakula na kilimo FAO.

Katika ripoti iliyotolewa leo na shirika hilo lenye makao yake makuu mjini Roma Italia inayohusu mchakato wa tathmini ya ugavi wa mazao na usambazaji wa chakula inaonyesha kwamba uzalishaji wa nafaka wa kitaifa mwaka 2022, unaojumuisha mazao ya mtama, ulezi na ngano yaliyovunwa mwezi huu wa Machi 2023, yanakadiriwa kuwa ni takriban tani milioni 7.4 hii ikiwa ni asilimia 45zaidi ya mwaka 2021.

FAO inasema uzalishaji wa mtama pekee ni karibu tani milioni 5.2, ongezeko la asilimia 50 kuliko mwaka uliopita.

Uzalishaji wa mtama unakadiriwa kuwa tani milioni 1.7, likiwa ni ongezeko la asilimia 86 ikilinganishwa na mwaka 2021.

Ziada ya tani 484,000 za mtama na tani 679,000 za uzeli pia zinatarajiwa.

Hameed Nuru wa WFP akiwa na wanafunzi darfur, Sudan, walipokuwa wakifurahia chakula kilichopikwa kwa viungo kutoka bustani yao ya shule. Ziara hiyo ilifanyika wakati Nuru alikuwa Mkurugenzi wa Nchi wa WFP Sudan.
© WFP/Sudan
Hameed Nuru wa WFP akiwa na wanafunzi darfur, Sudan, walipokuwa wakifurahia chakula kilichopikwa kwa viungo kutoka bustani yao ya shule. Ziara hiyo ilifanyika wakati Nuru alikuwa Mkurugenzi wa Nchi wa WFP Sudan.

Sudan inahitaji kuagiza tani milioni 3.5 za chakula

Ripoti hiyo inasema ongezeko hili kubwa la jumla la uzalishaji wa nafaka linaweza kuhusishwa na hali nzuri ya hewa, hasa ufanisi mzuri wa msimu wa mvua, uliopigwa jeki na zaidi ya tani 5,000 za mbegu bora za aina zilizoboreshwa zinazotolewa na FAO ili kuimarisha uzalishaji wa chakula katika kaya zilizo katika mazingira magumu.

Kwa mujibu wa ripoti asilimia 95 ya ardhi inayolimwa iko chini ya kilimo cha kutegemea mvua na mvua ni kichocheo muhimu cha uzalishaji wa kilimo nchini Sudan.

“Zaidi ya hayo, pembejeo nyingi za kilimo, zikiwemo mbegu, mbolea, dawa za kuulia magugu, mafuta na nguvu kazi, vilipatikana mwaka 2022, lakini kwa gharama kubwa sana ikilinganishwa na msimu uliopita. Matokeo yake, wakulima wengi walilazimika kutumia mbegu walizohifadhi kutokana na mavuno ya mwaka uliopita kwa sababu ya bei ya juu ya soko,” ripoti hiyo ya FAO inaeleza.

Imeendelea kueleza kwamba licha ya kuimarika kwa uzalishaji wa kilimo kwa ujumla, ngano itakayovunwa Machi mwaka huu wa 2023 inatarajiwa kufikia takriban tani 476,000, kiwango ambachi kimeshuka kwa 30% kutoka mwaka 2021, kutokana na kupungua kwa eneo lililopandwa nafaka na kutoa fursa ya kilimo cha faida cha kunde na viungo.

Kulingana na makadirio ya ongezeko la idadi ya watu zaidi ya milioni 47 kufikia katikati ya mwaka huu 2023, mahitaji ya kuagiza nafaka kwa mwaka huu wa uuzaji yanakadiriwa kuwa tani milioni 3.6 zote ni za ngano.

Hii itahitaji kuagiza tani milioni 3.5 kutoka nje ili kufidia matumizi ya ndani.

Kuendelea kuongeza uzalishaji wa nafaka kitaifa

Kwa mujibu wa FAO, hali hii itakuwa na athari nzuri kubwa kwa uhakika wa chakula kwa mamilioni ya Wasudan, wakati bei ya ngano ya kimataifa ikiendelea kupanda na sarafu ya taifa ya nchi hiyo kudhoofika.

"Kuendelea kuongeza uzalishaji wa kitaifa wa nafaka ni muhimu ili kuimarisha uhakika wa chakula na mnepo wa watu walio hatarini zaidi nchini Sudan," amesema Adam Yao, kaimu mwakilishi wa FAO nchini Sudan.

Ameongeza kuwa "Ingawa uzalishaji wa nafaka kwa ujumla katika ngazi ya kitaifa ni wa juu zaidi kuliko msimu uliopita, uhaba wa chakula katika ngazi ya kaya bado ni changamoto kubwa. Ni muhimu kukumbuka kuwa jamii zinakabiliwa na udhaifu wa aina tofauti, kutokana na kupanda kwa bei ya mazao makuu na athari za pamoja za mdororo wa kiuchumi, mfumuko wa bei, hatari za mabadiliko ya tabianchi na migogoro".

Mchakato huu wa kutafuta ukweli ulifanyika kwa ombi la wizara ya kilimo ya Sudan kwa ushirikiano wa karibu na washirika wakuu, ikiwa ni pamoja na shirika la Umoja wa Mataifa la mpango wa chakula duniani (WFP), Mtandao wa mifumo ya tahadhari ya mapema ya njaa na shirika la maendeleo ya kimataifa la Marekani.