Dungusi kakati ni jibu la njaa- FAO

Image

Dungusi kakati ni jibu la njaa- FAO

Shirika la chakula na kilimo duniani, FAO limesema majani na matunda ya dungusi kakati ni suluhu ya ukosefu wa chakula kwa binadamu na mifugo katika maeneo yenye  ukame.

Ni kwa mantiki hiyo FAO tayari imekutanisha wataalamu ili kubonga bongo kusaidia wakulima na watunga sera juu ya jinsi ya kutumia vema tunda hilo lenye rangi nyekundu ambalo mara nyingi hupuuzwa.

Hans Dreyer ambaye ni mkurugenzi wa FAO anayehusika na kitengo cha uzalishaji na ulinzi wa mimea ametolea mfano Madagascar ambapo wakati wa ukame mkali hivi karibuni, matunda na majani ya dungusi kakati yalikuwa chakula muhimu kwa binadamu na wanyama.

Nayo Brazil ina eka 500,000 za dungusi kakati ambapo majani yake hutumika kutengenezea chakula cha Wanyama.

Dreyer amesema kwa kuwa mabadiliko ya tabianchi nayo yanatishia uwepo wa mmea huo, hivi sasa hatua zimechukuliwa katika nchi 26 ili kuulinda kwa kuwa  ni suluhu wakati wa njaa .

Tayari FAO imechapisha kitabu chenye maelezo kuhusu matumizi ya mmea huo kwa binadamu na wanyama.