Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Uhalifu dhidi ya ubinadamu ulifanywa tangu mwaka 2016

Wahamiaji wakiwa ndani ya jengo moja katika kituo cha kizuizi cha wahamiaji nchini Libya. (Maktaba)
© UNICEF/Alessio Romenzi
Wahamiaji wakiwa ndani ya jengo moja katika kituo cha kizuizi cha wahamiaji nchini Libya. (Maktaba)

Uhalifu dhidi ya ubinadamu ulifanywa tangu mwaka 2016

Haki za binadamu

Wachunguzi huru wa haki za binadamu walioteuliwa na Umoja wa Mataifa hii leo wamesema kuna misingi ya kuamini kwamba mamlaka ya Libya na makundi ya wanamgambo wenye silaha wamehusika na "safu nyingi" za uhalifu wa kivita, na uhalifu dhidi ya ubinadamu katika miaka ya hivi karibuni.

Katika ripoti yao yenye kurasa 19 wachunguzi hao kutoka Misheni ya kutafuta ukweli au Fact-Finding Mission FFM wamesema kwa upande wa vikosi vya usalama vya Taifa la Libya, ukiukwaji wa haki za binadamu ulifanywa ili kukomesha upinzani na kuwanyonya wahamiaji walio katika mazingira magumu, bila haki.

Ripoti pia imesema kuna “tabia iliyoenea” ya watu kuwekwa vizuizini kiholela, mauaji, mateso, ubakaji, utumwa na kulazimisha kutoweka nchini. Aidha, Ujumbe kwa mara ya kwanza ujumbe huo umesema kwamba utumwa wa ngono ulifanywa dhidi ya wahamiaji.

“Kuna haja ya dharura ya uwajibikaji kukomesha hali hii ya kutokujali iliyoenea," alisema Mohamed Auajjar, mwenyekiti wa Misheni. "Tunatoa wito kwa mamlaka ya Libya kuandaa mpango wa utekelezaji wa haki za binadamu na wawe na muongozo utakaoonesha njia watakazotumia zinazo zingatia waathiriwa wakati huu wa mpito bila kuchelewa, na kuwawajibisha wale wote wanaohusika na ukiukaji wa haki za binadamu.”

Libya imekumbwa na msukosuko tangu kuondolewa madarakani kwa aliyekuwa kiongozi wa muda mrefu Muammar Gaddafi, huku nchi hiyo ikigawanyika kati ya tawala hasimu na wapiganaji wanamgambo, huku kukiwa na Serikali ya Makubaliano ya Kitaifa inayotambuliwa na Umoja wa Mataifa yenye makao yake makuu mjini Tripoli na vikosi vya Jenerali Khalifa Haftar -linaloitwa Jeshi la Taifa la Libya likishikilia mamlaka katika maeneo ya mashariki na kusini mwa taifa hilo lenye utajiri mkubwa wa mafuta.

Hakuna uwajibikaji

Wachunguzi huru wameripoti tangu mwaka wa 2016, ilibainika kuwa uwajibikaji kwa ukiukaji huo ulikosekana kwa kiasi kikubwa, kwani walionusurika walikuwa na hofu kubwa na kutoamini mfumo wa haki kuripoti rasmi unyanyasaji huo. Kutokana na hali hiyo, ukiukaji unaendelea "bila kupunguzwa", Ujumbe ulisema.

Wakati majukumu yake yanafikia tamati wiki ijayo, Ujumbe huo ulitoa wito wa kuundwa kwa mbinu mpya za ufuatiliaji na uchunguzi wa haki, ili “kuunga mkono juhudi za upatanisho wa Libya” na kusaidia mamlaka kufikia “katika mpito wa haki na uwajibikaji.”

Unyonyaji mkubwa kwa wahamiaji

Ripoti hiyo inabainisha kuwa zaidi ya wahamiaji 670,000 kutoka zaidi ya nchi 41 walikuwepo nchini Libya katika kipindi cha kuanzia Julai 2022, wakati mamlaka ya Ujumbe huo yalipooongezwa muda wake kwa mara ya mwisho, hadi Machi mwaka huu 2023.

Ujumbe huo uliwahoji zaidi ya wahamiaji 100 wakati wa uchunguzi wake na ripoti yake inaangazia “ushahidi mwingi” wa mateso ya kimfumo na utumwa wa kingono, miongoni mwa ukiukwaji mwingine.

Vituo vya kizuizini ambako wahamiaji walifanywa watumwa vilikuwa "chini ya udhibiti halisi au wa kawaida" wa mamlaka, ikiwa ni pamoja na Kurugenzi ya Kupambana na Uhamiaji Haramu na Walinzi wa Pwani ya Libya.

Unyonyaji wa wahamiaji ni suala pana na ni biashara yenye faida kubwa, Ujumbe huo ulisema, ukibainisha kuwa "usafirishaji haramu wa binadamu, utumwa, kazi ya kulazimishwa, kufungwa, unyang'anyi na magendo yalileta mapato makubwa kwa watu binafsi, vikundi na taasisi za Serikali."

Dhuluma kizuizini

Ukiukaji unaohusiana na kizuizini pia ulipatikana kuwaathiri Walibya kwa kiwango kikubwa, na Misheni inaelekeza wajibu wa mamlaka za Serikali na uongozi wao.

Ripoti hiyo inabainisha kuwa waathisiriwa "walitoka katika kila sehemu ya jamii ya Libya na walijumuisha watoto, wanaume na wanawake watu wazima, watetezi wa haki za binadamu, washiriki wa kisiasa, wawakilishi wa mashirika ya kiraia, wanajeshi au vikosi vya usalama, wataalamu wa sheria na watu wanaodhaniwa au wa aina mbalimbali za ngono kutokana na utambulisho wa kijinsia."

Wengi wa wale waliohojiwa na wachunguzi hao walishikiliwa bila kufunguliwa mashtaka katika mazingira ya kutisha, "wakiteswa mara kwa mara, kufungiwa peke yao, kuzuiliwa bila mawasiliano" na kunyimwa maji, chakula na vitu vingine muhimu.

Haki za wanawake zinarudi kinyume

Kwa mujibu wa Ujumbe huo, hali ya wanawake nchini Libya imezidi kuwa mbaya zaidi katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita, katika muktadha wa "kudhoofika kwa taasisi za Serikali" huku kukiwa na ongezeko la nguvu za makundi yenye silaha.

Ripoti hiyo inakadiria ubaguzi wa kimfumo dhidi ya wanawake, kuongezeka kwa unyanyasaji wa nyumbani, ambao hauadhibiwi na sheria yoyote ya kina, na ukosefu wa uwajibikaji kwa uhalifu dhidi ya viongozi mashuhuri wa wanawake, kama vile kutoweka kwa mbunge Sihem Sergiwa karibu miaka minne iliyopita, na kuuawa kwa Hannan Barassi mwaka 2020.

Ujumbe huo ulikariri wito wake kwa mamlaka huko Benghazi, ambako uhalifu huo wa hali ya juu ulifanyika, "kuwachunguza vya kutosha" na kuwafikisha wahusika mbele ya sheria.

Watoto wakipita karibu na majengo yaliyoharibiwa kwa makombora huko Benghazi nchini Libya
© UNOCHA/Giles Clarke
Watoto wakipita karibu na majengo yaliyoharibiwa kwa makombora huko Benghazi nchini Libya

Mifumo ya uchunguzi bado inahitajika

Ikianzishwa na Baraza la Haki za Kibinadamu la Umoja wa Mataifa mwaka 2020 ili kuchunguza ukiukwaji wa haki za binadamu na pande zote tangu mwanzo wa 2016, jukumu la Ujumbe huo linamalizika tarehe 4 Aprili, wakati ambapo "hali ya haki za binadamu nchini Libya inazidi kuzorota, mamlaka za Serikali sambamba zinaibuka na mageuzi ya sekta ya sheria, utendaji na usalama yanayohitajika ili kuzingatia utawala wa sheria na juhudi za kuunganisha nchi yao bado zipo mbali kutekelezwa,” inasema ripoti hiyo.

Katika muktadha huu, Ujumbe huo unatoa wito kwa Baraza la Haki za Kibinadamu la Umoja wa Mataifa kuanzisha "utaratibu wa kutosha wa uchunguzi wa kimataifa wenye rasilimali za kutosha," na kwa Ofisi ya Kamishna Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa Haki za Kibinadamu kuunda utaratibu mwingine "na mamlaka inayoendelea ya kufuatilia na ripoti kuhusu ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu nchini Libya.

Wakiukaji wanapaswa kutengwa

Miongoni mwa mapendekezo mengine, ripoti hiyo inaitaka jumuiya ya kimataifa "kusitisha msaada wote wa moja kwa moja na usio wa moja kwa moja kwa watendaji wa Libya wanaohusika na uhalifu dhidi ya ubinadamu na ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu dhidi ya wahamiaji, kama vile Kurugenzi ya Kupambana na Uhamiaji Haramu, kwani ni kifaa cha Msaada wa Utulivu na Walinzi wa Pwani ya Libya."

Ujumbe huo pia unasema utawasilisha matokeo yake kwa Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ICC, ikiwa ni pamoja na orodha ya "watu wanaowezekana kuwa wahalifu wa kimataifa.”

Kuhusu wachunguzi hao nchini Libya

Wataalamu wa haki za Kibinadamu walioteuliwa na Baraza la Haki za Kibinadamu la Umoja wa Mataifa kama vile wajumbe wa Misheni hufanya kazi kwa hiari na bila malipo, sio wafanyakazi wa UN, na wanafanya kazi bila kuingiliwa na serikali au shirika lolote.

Vizingiti vya kisiasa

Kufuatia usitishaji mapigano uliosimamiwa na Umoja wa Mataifa o Oktoba 2020, uchaguzi ulipaswa kufanyika Desemba 2021, lakini uliahirishwa.

Mwezi uliopita, Abdoulaye Bathily, Mwakilishi Maalum wa Libya na mkuu wa ujumbe wa kisiasa wa Umoja wa Mataifa nchini humo (UNSMIL) alitangaza kwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa mpango mpya unaolenga kuwezesha kufanyika kwa uchaguzi wa rais na wabunge kabla ya mwisho wa mwaka.

Akizungumzia hitaji la upatanisho nchini Libya, Bathily alisema wakati huo, "Maridhiano ni mchakato wa muda mrefu ambao unapaswa kuwa jumuishi, unaozingatia waathirika, unaozingatia haki na msingi wa kanuni za haki za mpito."

Kusoma zaidi kuhusu ripoti hiyo kwa lugha ya kiingereza bofya hapa.