Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

OHCHR yakaribisha majuto ya ukiukwaji wa haki wa kihistoria Indonesia

Geti la kuingia kwenye makao makuu ya ofisi ya haki za binadamu OHCHR mjini Geneva Uswis
UN Photo/Jean-Marc Ferré
Geti la kuingia kwenye makao makuu ya ofisi ya haki za binadamu OHCHR mjini Geneva Uswis

OHCHR yakaribisha majuto ya ukiukwaji wa haki wa kihistoria Indonesia

Haki za binadamu

Ofisi ya kamishina mkuu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa OHCHR leo imesema"Tunakaribisha kukiri kwa Rais Joko Widodo wa Indonesia na kujieleza kwa majuto kuhusu matukio 12 ya kihistoria ya ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu, ikiwa ni pamoja na ukandamizaji wa kupinga Ukomunisti wa mwaka 1965-1966, mauaji ya waandamanaji mwaka 1982-1985, kutekelezwa kwa hatua za watu kutoweka mwaka 1997 na 1998, na tukio la Wamena Papua mwaka wa 2003. Ishara hii ya Rais ni hatua katika njia ndefu ya kuelekea upatikanaji wa haki kwa waathiriwa na wapendwa wao.” 

Ofisi hiyo imesema hatua hii inafuatia ripoti ya timu ya azimio lisilo la kimahakama la ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu wa zamani, ambayo iliteuliwa na Rais huyo.  

“Tunatumahi ripoti hiyo itawekwa hadharani ili kuuchagiza umma kujadili na kuichambua.”  Imeongeza kusema ofisi hiyo ya kamishina mkuu wa haki za binadamu. 

Hata hivyo taarifa hiyo imesema” Tunatambua kwamba kauli ya Rais, iliyotolewa Jumatano, haizuii hatua zaidi za mahakama kuchukuliwa na inajitolea kufanya mageuzi ambayo yanapaswa ili kuhakikisha kutojirudia tena kwa ukiukwaji huo.” 

Kwa mantinki hiyo ofisi ya UHCHR  imesema “Tunaiomba serikali ya Indonesia kuendeleza kasi hii kwa hatua zinazoonekana ili kuendeleza mchakato wa haki wa mpito wenye maana, ulio jumuishi na shirikishi, unaohakikisha ukweli, haki, fidia na kutojirudia kwa ukiukwaji huo kwa ajili ya waathiriwa na jamii zilizoathiriwa, ikiwa ni pamoja na waathirika wa ukatili wa kingono unayohusiana na migogoro na vurugu.” 

Taarifa ya ofisi hiyo imesisitiza kuwa mchakato wa kina wa mpito wa haki utasaidia kuvunja mzunguko wa miongo mingi wa kutokujali, kuendeleza uponyaji wa kitaifa na kuimarisha demokrasia ya Indonesia. 

Takriban watu nusu milioni waliuawa katika ukandamizaji dhidi ya Ukomunisti wa miaka ya 1960 na waandamanaji wengi wanaounga mkono mageuzi walipoteza maisha yao katika mauaji katika miaka ya 1980.