Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wataalamu wa UN: Uchunguzi ufanyike nchini Mali dhidi ya Wagner group na vikosi vya serikali

Familia moja iliyokimbia makazi yao imeketi mbele ya hema lao katika kambi isiyo rasmi huko Bagoundié nchini Mali.
© UNOCHA/Michele Cattani
Familia moja iliyokimbia makazi yao imeketi mbele ya hema lao katika kambi isiyo rasmi huko Bagoundié nchini Mali.

Wataalamu wa UN: Uchunguzi ufanyike nchini Mali dhidi ya Wagner group na vikosi vya serikali

Haki za binadamu

Wataalamu huru wa Umoja wa Mataifa wametaka kufanyika mara moja kwa uchunguzi huru nchini Mali kwa kile walichoeleza kuwa ni kuwepo kwa ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu pamoja na uwezekano wa uhalifu wa kivita unaosadikiwa kufanywa na vikosi vya serikali kwa kushirikiana na kundi binafsi la wanajeshi la Wagner group.

Katika taarifa yao iliyotolewa leo jijini Geneva Uswisi wataalamu hao wamesema tangu mwezi machi 2021 wamekuwa wakipokea taarifa za mauaji ya kikatili, mateso, uwepo wa makaburi ya watu wengi, vitendo vya ubakaji, unyanyasaji wa kijinsia, uporaji na watu kuwekwa vizuizini kiholela huku watu wengine wakipotea na mengi wa waaathirika wakiwa ni jamii ya watu wachache ya peuhl.

wataalamu hao wa Umoja wa Mataifa wamesema “Tuna wasiwasi sana na ripoti za kuaminika kwamba katika muda wa siku kadhaa mwishoni mwa mwezi Machi 2022, wanajeshi wa Mali wakiandamana na wanajeshi wanaoaminika kuwa wa Kundi la Wagner, waliwaua mamia ya watu, ambao walikuwa wamekusanywa huko Kijiji cha Moura, kilichopo katikati mwa nchi ya Mali.”

Wataalamu hao pia wameeleza kusikitishwa na kuongezeka kwa kazi za kijeshi za jadi kwa kile kinachojulikana kama Kundi la Wagner katika operesheni mbalimbali za kijeshi, pia zinazojumuisha operesheni zinazofafanuliwa kama kupambana na ugaidi, katika maeneo ya Nia Ouro, Gouni, na Fakala.

“Mali lazima iwe na umakini mkubwa katika kuzuia ushiriki wa moja kwa moja katika uhasama wa watu wote binafsi wanaoendesha shughuli zao katika eneo lake. Matumizi ya mamluki, watendaji wanaofanana na mamluki na makampuni ya kibinafsi ya ulinzi na kijeshi yanazidisha mzunguko wa ghasia ulioenea nchini humo.” Wataalamu hao wameonya.

Kundi la Wagner

Waathiriwa wa kundi linaloitwa Wagner Group wanakabiliwa na changamoto nyingi katika kupata haki na suluhu kutokana na vitendo walivyofanyiwa vya ukiukwaji wa haki za binadamu, ikiwa ni pamoja na unyanyasaji wa kijinsia, na uhalifu unaotendwa dhidi yao, hasa kwa kuzingatia usiri na uwazi unaozunguka shughuli za Wagner nchini Mali.

Wataalamu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa wamesema “Kukosekana kwa uwazi na utata juu ya hadhi ya kisheria ya Kundi la Wagner, pamoja na kulipiza kisasi kwa wale wanaothubutu kusema, kunaleta hali ya jumla ya ugaidi na kutokujali kabisa kwa waathiriwa wa dhuluma za Kundi la Wagner.”

Tayari wataalamu hao wamewasilisha wasiwasi wao kuhusu madai hayo kwa Serikali ya Mali.

Kufahamu zaidi kuhusu wataalamu hao bofya hapa.