Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Heko wanawake wa Somalia kwa mchango wa kulijenga vyema taifa lenu: UNSOM

Wanawake wa Somalia wanaangazia maeneo ya msaada ili kufikia usawa wa kijinsia.
UN Photo / Mukhtar Nuur
Wanawake wa Somalia wanaangazia maeneo ya msaada ili kufikia usawa wa kijinsia.

Heko wanawake wa Somalia kwa mchango wa kulijenga vyema taifa lenu: UNSOM

Wanawake

Katika kuadhimisha siku ya kimataifa ya wanawake hii leo Mpango wa Umoja wa Mataifa nchini Somalia UNSOM, umewapongeza wanawake wa nchi hiyo ya Pembe ya Afrika kwa mchango wao mkubwa unaoendelea kwa ajili ya kusongesha maendeleo ya taifa hilo.

Akitoa pongezi hizo mjini Moghadishu naibu mwakilishi wa Katibu Mkuu nchini Anita Kiki Gbeho amesema "Kuanzia juhudi za kujenzi wa amani na upatanisho, hadi shughuli za kuleta utulivu katika maeneo yaliyopatikana hivi karibuni kutoka kwa udhibiti wa Al-Shabaab na mwitikio wa shughuli za kibinadamu kutokana na ukame uliofurutu ada wanawake wa Somalia wanaendelea kuchangia kwa kiasi kikubwa katika nyanja zote za maisha ya umma."

Michango ya wanawake wa Somalia ni pamoja na kuandaa utoaji wa misaada ya kibinadamu kama vile chakula na vifaa vingine muhimu, na malazi kwa watu walioathiriwa na migogoro na ukame wa muda mrefu.

Wanawake wa Somalia wanaangazia maeneo ya msaada ili kufikia usawa wa kijinsia.
UN Photo / Mukhtar Nuur
Wanawake wa Somalia wanaangazia maeneo ya msaada ili kufikia usawa wa kijinsia.

Toeni ushirikiano kwa wanawake

Afisa huyo ameendelea kusema kwamba Umoja wa Mataifa nchini Somalia unatambua juhudi zinazoendelea za wanawake wa Somalia kwa miaka mingi na kuwataka wadau wote wa Somalia, hasa viongozi wa nchi hiyo, kuhakikisha ushirikishwaji Zaidi wa wanawake, kuwapa sauti na fursa ya ushirikishwaji wa wanawake katika vyombo vyote vya kitaifa na serikali kama sehemu ya juhudi za kudumisha amani, ustawi na maendeleo nchini Somalia.

Kaulimbiu ya siku ya kimataifa ya wanawake mwaka huu ni “Dijitali kwa wote: Ubunifu na Teknolojia kwa Usawa wa Jinsia,” na inalenga kuangazia umuhimu wa teknolojia ya kidijitali kama fursa ya kupunguza mapengo ya kijinsia kwa kuimarisha ufikiaji wa wanawake wote.

Amesisitiza kuwa “Ikiwa wanawake hawawezi kufikia mtandao na hawajihisi salama mtandaoni, hawataweza kukuza ujuzi wa kidijitali unaohitajika ili kushiriki katika nafasi za kidijitali.”

Umoja wa Mataifa nchini Somalia unawahimiza wanawake wa Somalia kukumbatia matumizi ya teknolojia katika kazi zao ili kusaidia kujenga Somalia bora.

Kiwango cha matumizi ya intaneti nchini Somalia kimekuwa kikipanda kwa kasi katika miaka michache iliyopita mathalani kimepanda kwa asilimia  16.4 kutoka mwaka 2021 hadi 2022, kulingana na kampuni ya ufuatiliaji wa matumizi ya kidijitali ya DataReportal.

Siku ya kimataifa ya wanawake inaadhimishwa duniani kote tangu mwaka 1975 wakati Umoja wa Mataifa ulipoanza kufanya hafla ya kusherehekea mafanikio ya kijamii, kiuchumi, kiutamaduni na kisiasa ya wanawake.

Siku hii inaadhimisha wito wa kuchukua hatua ili kuharakisha usawa wa kijinsia.