Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ni wakati wa kuhakikisha mwanamke anashika usukani kila nyanja Guterres akiambia kikao cha CSW65

Muuguzi akiwasalimu wageni katika kliniki iliyowekwa kwenye hospitali nchini Thailand kwa ajili ya wagonjwa wenye dalili za COVID-19
WHO/P. Phutpheng
Muuguzi akiwasalimu wageni katika kliniki iliyowekwa kwenye hospitali nchini Thailand kwa ajili ya wagonjwa wenye dalili za COVID-19

Ni wakati wa kuhakikisha mwanamke anashika usukani kila nyanja Guterres akiambia kikao cha CSW65

Wanawake

Mkutano wa kamisheni ya hali ya wanawake  duniani kikao cha 65 umefungua pazia hii leo ikiwa ni mara ya pili kufanyika katika mazingira ya janga la virusi vya corona au covid-19 ambapo Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema janga hili lina sura ya mwanamke akisema kwamba hali ya sasa imedhihirisha jinsi ukosefu wa usawa wa kijinsi ulivyo kwa kiasi kikubwa na umekita mizizi katika mifumo ya kisiasa, kijamii na kiuchumi. 

Bwana Guterres amesema wanawake ni asilimia 70 ya wahudumu wa afya kote ulimwenguni na wanafanya kazi katika sekta nyingi za kiuchumi zilizoathirika vibaya wakati wa janga hili. 

Ikilinganishwa na wanaume, wanawake asilimia 24 zaidi  wako katika hatihati ya kupoteza kazi zao, na wanaweza kutarajia mapato yao kuanguka kwa asilimia 50 kwa kasi zaidi.

Kazi ya utunzaji na huduma za bila malipo kwa wanawake na wasichana zimeongezeka sana kwa sababu ya masharti ya kusalia nyumbani, kufungwa kwa shule na vituo vyakulelea watoto, kuongezeka kwa utunzaji wa wazee na mengi mengineyo. Amesema mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa.

Ameongeza kuwa janga la COVID-19 pamoja na mambo mengine vimezidisha janga la ukatili wa kijinsi dhidi ya wanawake kote ulimwenguni kwenye mitandao na kwingineko na kwamba, ni“tatizo linaongezeka kila mwezi kuanzia ukatili wa kingono hadi ndoa za utotoni na kwamba, sasa ndio wakati wa kubadili mkondo na ushiriki wa wanawake katika mizani sawa ndio mabadiliko tunayohitaji.” 

Nchini Guinea, katika kijiji cha Katfoura, shirika la kiraia la PREM linapatia wanawake wa vijijini fursa mpya za kujipatia kipato na kuimarisha maisha yao.
UN Women/Joe Saade
Nchini Guinea, katika kijiji cha Katfoura, shirika la kiraia la PREM linapatia wanawake wa vijijini fursa mpya za kujipatia kipato na kuimarisha maisha yao.

 Ushiriki wa wanawake unalipa mara dufu

Bwana Guterres amesema miongo kadhaa ya ushahidi inaonyesha kuwa ushiriki wa wanawake huongeza tija ya matokeo ya kiuchumi, husababisha uwekezaji mkubwa katika ulinzi wa jamii, huchangia amani endelevu zaidi na maendeleo ya hatua za mabadiliko ya tabianchi.

 “Na sasa ni hatua za kukabiliana na  COVID-19 ambazo zimedhihirisha uwezo mkubwa wa uongozi wa wanawake.”

Takribani wanawake milioni 12 duniain kote wamekumbwa na kuvurugwa kwa huduma za uzazi wa mpango kutokana na janga la COVID-19
© UNFPA/Ollivier Girard
Takribani wanawake milioni 12 duniain kote wamekumbwa na kuvurugwa kwa huduma za uzazi wa mpango kutokana na janga la COVID-19

 Ameongeza kuwa katika mwaka uliopita, viongozi wanawake ni miongoni mwa wale ambao wamehakikisha viwango vya maambukizi ya COVID-19 vinasalia chini na kuziweka nchi kwenye njia ya kuelekea kujikwamua.

 Mashirika ya wanawake yameziba mapengo muhimu katika utoaji wa huduma na taarifa, haswa katika ngazi ya jamii na uwiano mkubwa wa kijinsia umesababisha matokeo bora.

“Kinyume chake, amesema katika nchi ambazo hatua zina ufanisi mdogo ni zile ambazo mtazamo wa mfumo dume unatawala na haki za wanawake zinakandamizwa.”

Umoja wa Mataifa, kwa upande wake, umeweka wanawake katikati ya jitihada zake za kujikwamua na janga la COVID-19.

Hatari ya kutawaliwa na mfumo dume

Katibu Mkuu amesisitiza hatari ya kuendelea kwa utawala wa mfumo dume katika maisha ya umma, na kwa nini ni muhimu sana kwa wanawake kushiriki katika michakato ya kufanya maamuzi.

"Wakati wanawake wanakosekana katika kufanya maamuzi, tunaona ulimwengu kupitia mtazamo mmoja tu. Tunaunda mifano ya kiuchumi ambayo inashindwa kupima kazi yenye tija inayofanyika nyumbani."

Wanafunzi nchini Uganda wakijadili katika klabu yao ya Wasichana katika Elimu, suala la ukatili dhidi ya wanawake wakiwa na muongozaji wao.
© UNICEF/Jimmy Adriko
Wanafunzi nchini Uganda wakijadili katika klabu yao ya Wasichana katika Elimu, suala la ukatili dhidi ya wanawake wakiwa na muongozaji wao.

Bwana Guterres amefafanua mabadiliko yanayofanywa katika Umoja wa Mataifa ili kuhakikisha usawa wa kijinsia katika shirika hilo. 

Hii ni pamoja na kuweka wanawake wengi katika nafasi za uongozi wa juu, kufikia usawa wa kijinsia katika viwango vya usimamizi wa juu, na kujitahidi kuhakikisha ushiriki wa wanawake katika kulinda amani, upatanishi na mchakato wa ujenzi wa amani.

Ameongeza kuwa "Tunahitaji kupiga hatua zaidi ya kurekebisha wanawaka, na badala yake turekebishe mifumo yetu. Kujikwamua na janga la COVID-19 ni fursa kwetu ya kupanga njia ya mustakabali wenye sawa. "

Mambo matano ya kuleta usawa wa kijinsia

Katibu Mkuu amependekeza hatua tano ambazo viongozi wa ulimwengu wanaweza kuzichukua ili kusongesha mbele mchakato wa usawa wa kijinsia.

1. Kutambua kikamilifu haki sawa za wanawake: pamoja na kufuta sheria za ubaguzi na kuchukua hatua nzuri.

2. Kuhakikisha uwakilishi sawa: kuanzia kwenye bodi za makampuni hadi kwenye mabunge, kutoka kwenye elimu ya juu hadi taasisi za umma kupitia hatua maalum na nafasi za upendeleo.

3. Kuendeleza ujumuishaji wa wanawake kiuchumi:  kupitia malipo sawa, mikopo inayolenga wanawake, ulinzi wa ajira zao na uwekezaji mkubwa katika uchumi wa hifadhi na ulinzi wa jamii.

4. Kuweka mpango wa dharura wa kukabiliana na majanga katika kila nchi ili kushughulikia unyanyasaji dhidi ya wanawake na wasichana, na kufuatili hilo kupitia ufadhili, sera, na utashi wa kisiasa.

5. Kutoa fursa za mpito kwa vizazi vinavyoendelea.

Phumzile Mlambo-Ngcuka, Mkurugenzi mtendaji wa UN Women
UN Women/ Tian Liming
Phumzile Mlambo-Ngcuka, Mkurugenzi mtendaji wa UN Women

Wanawake wamezingirwa na ukatili wa kijinsia

Kikao hiki cha 65 cha kamisheni ya hali ya wanawake duniani kilichoanza leo 15 Machi kinatarajiwa kufunga pazia 26 Machi, na kinahusisha vikao halisi, na sehemu kubwa kupiotia mtandaoni na UN Women, shirika la Umoja wa Mataifa linalofanya kazi kuharakisha usawa wa kijinsia ulimwenguni, kwa kushirikiana na wadau wengine, mashirika na asasi za kiraia.
Mkurugenzi Mtendaji wa UN Women, Phumzile Mlambo-Ngcuka, katika hotuba yake kwenye ufunguzi wa kikao hicho amesema kwamba wale walioathiriwa zaidi na janga la COVID-19 ni wale ambao hawawezi kuhimili.
Kwa sababu ya janga hilo , Bi Mlambo-Ngcuka, amesema “wanawake milioni 47 zaidi wamesukumwa kuishi kwa umasikini wa chini ya dola $ 1.90 kwa siku, wasichana milioni 10 zaidi wanatarajiwa kuwa katika hatari ya ndoa za utotoni katika miaka kumi ijayo, na wanawake wamezingirwa na unyanyasaji wa kijinsia , wanaoathirika na viwango vya juu zaidi vya unyanyasaji kutoka kwa wenzi wao wa karibu zaidi kuwahi kuonekana, katika miezi 12 iliyopita.”
Kwa kuongezea, amesema unyanyasaji dhidi ya wanawake katika maisha ya umma ni kikwazo kikubwa kwa ushiriki wao wa kisiasa, na huathiri wanawake katika sehemu zote za ulimwengu. "Uwakilishi duni wa wanawake ni sababu ya maendeleo ya polepole katika nyanja zote za usawa wa kijinsia".
Bi. Mlambo-Ngcuka amewahimiza wajumbe katika kikao hicho kuzingatia vipaumbele, na kuhakikisha kuwa wanawake wana nafasi yao katika meza kuu ya majadiliano, na kuongeza kuwa haiwezekani hali hiyo kuweza kushughulikiwa, bila wanawake wenyewe kushiriki katika kufanya maamuzi.

Volkan Bozkir, Rais wa mkutano wa 75 wa Baraza Kuu akifungua mjadala wa wazi wa Baraza Kuu.
UN Photo/Eskinder Debebe)
Volkan Bozkir, Rais wa mkutano wa 75 wa Baraza Kuu akifungua mjadala wa wazi wa Baraza Kuu.


Rais wa ECOSOC na Rais wa Baraza Kuu

Munir Akram, Rais wa Baraza la Uchumi na Jamii la Umoja wa Mataifa  (ECOSOC), na Volkan Bozkir, Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa pia wamezungumza katika ufunguzi wa kikao hicho.
Sauti za wanawake katika nchi zilizoendelea na zinazoendelea zinaendelea kunyamazishwa, huku kukiwa na ubaguzi na vurugu zilizoenea, mesema Bwana Akram. 
Ameongeza kuwa “wanawake na wasichana wanakabiliwa na vizuizi vingi, ikiwa ni pamoja na mizozo, ugaidi, majanga ya asili, na ukosefu wa usawa wa mafunzo na ajira.”
Mkuu wa ECOSOC ametangaza kuwa maendeleo endelevu hayawezekani ikiwa wanawake wataendelea kutengwa, na ametaka muungano mpya wa kimataifa wa kuwawezesha wanawake, na kuondoa aina zote za unyanyasaji dhidi ya wanawake na wasichana.
Bwana Bozkir Rais wa Baraza Kuu kwa upande wake ametoa wito kwa nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa kuchukua hatua kadhaa thabiti, pamoja na kuimarisha sheria dhidi ya unyanyasaji wa kijinsia; kuanzisha mifumo ya kuripoti na kurekebisha mchakato kwa ajili ya waathirika, na kujitolea kwa ufuatiliaji wa vurugu.
"Hakuna mwanamke anayepaswa kuhisi haja ya kuhalalisha uwepo wake au kuogopa kujieleza. Hakuna mwanamke anayepaswa kutishiwa, kulipwa mshahara mdogo, au kudharauliwa. “ amesisitiza Rais huyo.