Ajenda ya wanawake, amani na usalama bado ni moja ya vipaumbele vya juu vya UN -Guterres

29 Oktoba 2019

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres hii leo akihutubia Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa linalojadili ajenda ya wanawake, amani na usalama amesema pamoja na hatua zilizopigwa lakini bado kasi ya kuwainua wanawake hairidhishi.

“Huu ni ukweli wa kusikitisha ,na tunapaswa kuwa wakweli juu suala hili, kujitolea ambako kunaonekana katika meza hii hakuonekani katika mabadiliko halisi duniani.” Amesema Bwana Guterres.

Ambaye ameongeza kuwa mabadiliko hayaji kwa kasi inayotosha au kwenda mbali kiasi cha kutosha na kwamba mabadiliko hayo yanakuja kwa mwendo wa taratibu mno kwa wanawake na wasichana ambao maisha yao yanategemea mabadiliko hayo na kwa ufanisi wa juhudi zetu za kutunza amani na usalama wa kimataifa.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amesisitiza, “takribani miongo miwili tangu azimio namba 1325 lilipoidhinishwa, wanawake bado wanakabiliwa na kutengwa katika michakato ya amani na siasa.”

Aidha ameeleza kuwa mikataba ya amani hupitishwa bila vifungu kuzingatia mahitaji na vipaumbele vya wanawake na wasichana. Kiasi kidogo, kama asilimia mbili ya misaada ya nchi na maeneo dhaifu na yaliyoathiriwa na migogoro huenda kwa mashirika ya wanawake.

Akionesha hali ilivyo mbaya, Bwana Guterres amesema idadi ya mashambulizi dhidi ya wanaharakati wa haki za wanawake, haki za binadamu na walinda amani inazidi kuongezeka.

Unyanyasaji wa kingono na wa kijinsia vinaendelea kutumika kama silaha ya vita, huku waathirika wa manyanyaso hayo mara nyingi wakiachwa bila kutendewa haki au kupata msaada wanaouhitaji.

“Kwa mwaka huu pekee, mamilioni ya wanawake na wasichana walikuwa katika mahitaji muhimu ya huduma za kiafya na afya ya uzazi, na mamilioni zaidi walihitaji usaidizi wa kuzuia manyanyaso ya kingono na kijinsia.” Ameeleza Bwana Guterres

Aidha amesema kuna ongezeko la idadi ya makundi ya wapiganaji ambayo ukosefu wa usawa wa kijinsia ni lengo lao la kimkakati na sehemu mbaya ya chimbuko la itikadi yao.

Pia amenukuliwa akisema, “na tunafamu kuwa wanawake na wasichana wanaendelea kulipia kwa gharama kubwa migogoro kwa ujumla. Kwa kutoa mfano mmoja,  huko kaskazini mashariki mwa Syria, tuliona maelfu ya wanawake na watoto wakikimbia vurugu za hivi karibuni. Lakini pamoja na hali hii mbaya, hatutakata tamaa. Hii kwangu ni kipaumbele cha muhimu.”

Hata hivyo ametaja baadhi ya mafanikio akieleza kuhusu Yemen ambako wanawake walikuwa wameachwa nje ya mzunguko rasmi na mashauriano lakini mjumbe maalumu wa Katibu Mkuu akaanzisha kundi la ushauri wa kitaalamu la wanawake wa Yemen ili kuhakikisha mtazamo wa wanawake wa Yemen unajumuishwa.

Huko nchini Guinea-Bissau, wanawake walishiriki katika jukumu la moja kwa moja la  kumaliza mgogoro wa kisiasa mwaka jana kwa kufadhiliwa na mfuko wa ujenzi wa amani.

Aidha ameeleza nchini Syria asilimia 30 ya kamati mpya ya katiba ni wanawake wakiwemo wengine kutoka kwenye bodi ya ushauri ambayo imekuwa ikifanya kazi ya amani kwa miaka hii yote.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa pia ameeleza hatua zinazopigwa katika Umoja wa Mataifa kuhusu kuwapa nafasi wanawake akisema, “nimewateua wanawake wengi kama wakuu na manaibu wa ujumbe mbalimbali wa Umoja wa Mataifa na tunatekeleza hatua za dharura kuhakikisha tunafikia usawa wa kijinsia.”

“Wanawake, amani na usalama ni moja ya nguzo nane za kipaumbele za hatua yetu ya utunzaji wa amani, iliyoidhinishwa sasa na zaidi ya nchi 150.” Amesema Guterres.

Amehitimisha akitoa wito kwa wadau wote kushiriki pamoja katika kubadili hali ilivyo ili kuwahusisha wanawake katika masuala yote.

 

 

♦ Kutembelea ukurasa maalum wa COP26 bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter