Ajenda ya wanawake, amani na usalama ndio kipaumbele chetu:Guterres

9 Oktoba 2020

Vita vya silaha vimewaathiri kwa kiasi kikubwa wanawake na wasichana na ndio sababu ushiriki wa kikamilifu, wenye usawa na maana wa wanawake kwenye ulinzi wa amani wa Umoja wa Mataifa ni kipaumbele chetu amesema Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres. 

Akizungumza Alhamis kwenye majadiliano kuhusu wanawake , amani na usalama (WPS) katika operesheni za ulinzi wa amani yaliyofanyika kwa njia ya mtandao Guterres amekumbusha azimio la kihistoria la Baraza la Usalama namba 1325 ambalo ameliita msingi wa amani ya kimataifa. 

Amesema mwezi huu wa Oktoba ni maadhimisho ya miaka 20 ya azimio hilo muhimu akieleza kwamba linathibitisha uhusiano baina ya pengo la usawa wa kijinsia na hali tete, na pia baina ya ulinzi wa wanawake na ulinzi wa kimataifa.” 

Amesisitiza kwamba, “tangu wakati huo Umoja wa Mataifa umefanya kazi bila kuchoka kusongesha mbele ajenda ya wanawake, amani na usalama.” 

Wanawake wamezingirwa 

Ingawa wanawake wameendesha ujumbe mkubwa wa afya ya umma wakati wote wa janga la corona au COVID-19, Bwana. Guterres amesema, “wanawake hao wamezingirwa wakibeba mzigo mkubwa wa kutoa huduma na kiuchumi katika jamii nyingi huku pia wakikabiliwa na wimbi la machafuko majumbani.” 

Na katika hali za migogoro amesema ingawa wanawake mara nyingi ndio waleta amani katika jamii zao wanaendelea kutengwa katika ngazi ya kitaifa na kimataifa. 

Guterres amesema mwaka mzima wa 2018 wanawake walikuwa asilimia 13 pekee ya washawishi na asilimia 3 pekee walihusika katika upatanishi na asilimia nne pekee ndio walioweka saini.  

Wakati wanawake wakiendelea kupigania sauti zao kusikika , licha ya kuwepo kwa mlima wa Ushahidi kuhusu uhusiano uliopo baina ya ushiriki wa wanawake na amani endelevu.” 

Walinda amani wanawake kutoka Tanzania wakiwa na wanawake na watoto wakazi wa Beni, nchini DRC.
TANZBATT 7/Ibrahim Mayambua
Walinda amani wanawake kutoka Tanzania wakiwa na wanawake na watoto wakazi wa Beni, nchini DRC.

 

Ujumbe binafsi 

Akizungumza mbele ya wanawake viongozi kutoka Jamhuri ya Afrika ya Kati CAR, Cyprus, Sudan na Mali waliohudhuria mkutano huo  , Bwana Guterres amewaeleza uzoefu wake katika kila nchi hizo ambako alishuhudia, “jukumu muhimu la wanawake katika kupunguza madhila na kusaka amani. Wanawake wa Darfur bila kuchoka wamekuwa wakipigia upatu na kuifanyia kazi amani na usalama katika serikali ya mpito inayoendelea”.  

Ameendelea na kuwaita wanawake walioshiriki utiaji saini wa mazungumzo ya amani ya Juba hivi karibuni kuwa ni mafanikio makubwa. 

Na kwa mara ya kwanza katika historia ya Jamhuri ya Afrika ya Kati CAR, Guterres amesema wanawake walishiriki katika mazungumzo ya Khartoum na mmoja wa wanawake hao alitia saini makubaliano ya amani mwaka jana. 

Nchini Mali amesema wanawake wanabeba jukumu kubwa la kisiasa katika hali ya sasa ya mpito, na wanawake walikuwa katika pande zote za meza ya mazungumzo ya amani nchini Cyprus kuanzia 2015 hadi 2017. 

Hata hivyo amesema bado mikwamo ya kisiasa, uwekezaji mdogo katika mashirika ya wanawake, fikra finyu na mizizi ya mfumo dume , vinapunguza kasi ya maendeleo ya wanawake  amesema Katibu Mkuu akisisitiza kwamba hili lazima libadilike. 

“Usawa wa kijinsia ni suala la madaraka. Tunahitaji mabadiliko thabiti ili kubadili na kugawanya jinsi madaraka yanavyoshikiliwa na kutumika.” 

Wito wa kuchukua hatua 

Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa ametoa wito kwa serikali, mfumo wa Umoja wa Mataifa, mashirika ya kikanda na ya asasi za kiraia  miongoni mwa mengine kuchukua hatua madhubuti kutekeleza kikamilifu ajenda ya wanawake amani na usalama. 

“Sote lazima tuchukue mtazamo wa kupigania wanawake ili kusongesha kikamilifu ushiriki sawa na wenye maana wa wanawake , na ili kujenga mustakabali wenye usawa na amani , uongozi wa wanawake ni lazima ubadilishwe kutoka kwenye sababu na kuwa kawaida.” 

 

 

 

♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter