Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Miaka 20 ya azimio namba 1325: Mafanikio na Changamoto

Ushirikiano baina ya wanawake ni muarobaini wa maendeleo hata kule mashinani kama inavyoonekana pichani walinda amani wanawake huko Darfur, Sudan wakielekeza wanawake mapishi ya maandazi.
UN /Muntasir Sharafdin
Ushirikiano baina ya wanawake ni muarobaini wa maendeleo hata kule mashinani kama inavyoonekana pichani walinda amani wanawake huko Darfur, Sudan wakielekeza wanawake mapishi ya maandazi.

Miaka 20 ya azimio namba 1325: Mafanikio na Changamoto

Wanawake

Mwaka huu azimio namba 1325 la Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kuhusu wanawake na ulinzi na usalama duniani, limetimiza miaka 20 tangu kupitishwa kwake.
 

Azimio hilo lilipitishwa tarehe 31 mwezi Oktoba mwaka 2000, likisititiza umuhimu wa nafasi ya wanawake katika kuzuia na kutatua mizozo, mashauriano ya amani, ujenzi wa amani, ulinzi wa amani, hatua za usaidizi wa kibinadamu na ujenzi baada ya mizozo na kusisitiza umuhimu wa ushiriki sawa katika uendelezaji wa amnai na usalama duniani.

Hii leo Baraza hilo katika maadhimisho hayo limekuwa na kikao kwa njia ya mtandao kuangazia mafanikio na changamoto ambapo Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres amesema suala la wanawake kushika nafasi za uongozi na kupitisha uamuzi si suala la kuwapendelea bali ni muhimu kwa ajili ya amani na maendeleo kwa watu wote duniani.

Unaisi Bolatolu-Vuniwaqa (katikati) Kamishina wa polisi wa mpango wa Umoja wa Mataifa Sudan Kusini UNMISS na maafisa wengine wanawake wa UNPOL wakizuru hospital ya watoto Juba na chuo cha uganda Juba ambako wametoa msaada wa vitu visivyo chakula . Kamishi
Picha na UN Photo/Nektarios Markogiannis
Unaisi Bolatolu-Vuniwaqa (katikati) Kamishina wa polisi wa mpango wa Umoja wa Mataifa Sudan Kusini UNMISS na maafisa wengine wanawake wa UNPOL wakizuru hospital ya watoto Juba na chuo cha uganda Juba ambako wametoa msaada wa vitu visivyo chakula . Kamishi

Bwana Guterres amesema “janga la COVID-19 limekuwa na madhara makubwa kwa wanawake na wasichana na bado wanawake wanaendelea kuwa na dhima kuu katika hatua za kukabili janga hilo” ambalo hadi sasa limesababisha vifo vya watu zaidi ya milioni 1 duniani kote.

Amesema mafanikio makubwa ambayo wanawake viongozi wamepata katika kudhibiti janga hilo huku wakisaidia watu kuendeleza mbinu zao za kujipatia kipato ni dhahiri.

Hivyo amesema, “hatua hii inathibitisha kuwa taasisi, mashirika, kampuni na serikali zinaweza kufanya kazi kwa ubora zaidi iwapo watajumuisha nusu ya idadi ya watu duniani badala ya kuwapuuza.”

Guterres amesisitiza, hatuwezi kuwa na matumaini ya kubadili mwenendo wa janga la mabadiliko ya tabianchi, kupunguza mgawanyiko kwenye jamii, au kuwa na amani endelevu bila mchango kamilifu wa jamii nzima. Uongozi wa wanawake katika nyanja zote utakuwa muhimu katika kusaka hatua haraka na salama kutoka katika janga hili na kujenga mustakabali bora zaidi na wenye amani na endelevu kwa wote.”

Sajini Bari Mwita, mwanamke pekee dereva na fundi makenika katika kikosi cha 7 cha Tanzania, TANZBATT 7, huko Beni, DRC akijiandaa kurekebisha gari lililoharibika.
TANZBATT 7 Video
Sajini Bari Mwita, mwanamke pekee dereva na fundi makenika katika kikosi cha 7 cha Tanzania, TANZBATT 7, huko Beni, DRC akijiandaa kurekebisha gari lililoharibika.

Usawa wa Jinsia ni hoja ya mamlaka

Amerejelea kauli yake kuwa suala la usawa wa jinsia ni hoja ya madaraka kwa kuwa mfumo wa madaraka na mamlaka bado unaendelea kudhibitiwa na wanaume. “Mchango wa maana na fanisi wa wanawake kwenye masuala ya usuluhishi, hupanua wigo wa amani, utulivu, utangamano wa kijamii na maendeleo ya kiuchumi.”

Ni kwa mantiki hiyo amesema kuwa wakati huu ambapo dunia inhaha kujinasua kutoka katika janga la COVID-19, chaguo ni moja; Kuendelea na mwenendo wa mapigano, mizozo na kupoteza vizazi au kusaka mbinu za ujumuishi zaidi, usawa, kuzuia mizozo na majanga ya aina yote.

Amesisitiza kuwa usawa wa jinsia ni moja ya mbinu ya uhakika zaidi ya kujenga jamii yenye utangamano, kuaminiana na kuvutia watu kuwa raia wawajibikaji na wenye kushiriki masuala yanayowahusu.

Guterres ametamatisha akisema, “kwa wanawake wasuluhishi, wajenga amani, watetezi wa haki za binadamu na wafanyakazi muhimu wa mstari wa mbele; kwa mamilioni ya wanawake na wasichana, wanaume, wavulana, watoto wa kike ambao matumaini yao ya amani na usalama yako katika jamii zenye usawa zaidi na haki; Hatuwezi kusubiri miaka mingine 20 kutekeleza ajenda ya wanawake, amani na usalama. Hebu na tuanze pamoja kazi hiyo leo hii.”

UN Women nayo yapaza sauti

Mkurugenzi Mtendaji wa shirika la Umoja wa Mataifa la kushughulikia masuala ya wanawake, UN Women Phumzile Mlambo-Ngcuka amesema Umoja wa Mataifa umeunga mkono wanawake kama wajenzi wa amani na imeongeza umakini wake na rasilimali kuchagiza uongozi wa wanawake ambao wameathiriwa na mizozo sambamba na kusaidia ili kushughulikia machungu waliyopitia.

Hata hivyo amesisitiza umuhimu wa ujumuishaji wa wanawake zaidi wa wanawake askari na wanajeshi kwenye ulinzi wa amani.

Akimulika mfumo wa mashauriano ya amani, Bi. Mlambo-Ngcuka amesema, “mashauriano hayo hivi sasa mfumo wake bado uko katika kumulika pande zinazochochea mzozo badala ya kuwajengea uwezo wajenzi wa amani, na hivyo kufanya uenguaji baadhi ya makundi na ukwepaji sheria kama jambo la kawaida. Wanawake bado wamenasa kwenye vita vya wanaume na ziada ya maneno ya kuwaunga mkono lakini hakuna fedha. Bado wanasalia kujilisha wenyewe kwa maneno matupu!”

Amesema miaka 20 iliyopita, Baraza la Usalama lilipitisha lengo la muda mrefu la wanawake na uongozi katika utatuzi wa mizozo na hivyo wakati umefika hivi sasa kuondoa nakisi katika utekelezaji wa ajenda hiyo.

“Duniani kote, kwenye uwanja vita, na kila pahali duniani, wanawake na watu wengine wanataka ujumuishwaji na uwakilishi, na ndio maana watu wengi wa kawaida wanaingia mitaani, wanaandaa maandamano na kupaza sauti zao. Vijana wa kike na vijana wajenga amani wako tayari kufanya kazi. Wanataka mabadiliko na wanataka kujumuishwa,” amesema Mkurugenzi Mtendaji huyo wa UN Women.
 

Aibu vyumba vya uamuzi kujaa wanaume peke yao- Danai

Mkutano huo pia ulihutubiwa na Balozi mwema wa UN Women, Danai Gurira ambaye amesema wasanii na waandishi mara kwa mara wanatumia  mashujaa kuhamasisha hadhira yao, lakini Baraza la Usalama limepata fursa ya kusikiliza moja kwa moja kutoka kwa mashujaa halisi wa maisha.

Wanawake wabunge Afghanistan wakiingia Bungeni (Wolesi Jirga )
UN Photo/Eric Kanalstein
Wanawake wabunge Afghanistan wakiingia Bungeni (Wolesi Jirga )

“Jambo moja ambalo hawa mashujaa halisi wa maisha wanalo wote ni ule ushawishi wa kweli wanaotupatia ya kwamba ujumuishaji ndio njia pekee ya kuondokana na zama hizi za giza na usawa kati ya wanawake na wanaume katika kupitisha uamuzi ni njia pekee kabisa  ya kujenga amani,” amesema Danai ambaye ni mmoja wa waigizaji katika filamu iliyojizolea umaarufu ya Black Panther.

Pamoja na kupongeza hatua zote zilizofikiwa katika baadhi ya maeneo ya azimio hilo namba 1325, Danai amesema bado haitoshi, “na katika karne hii ya 21 vyumba vya kupitisha uamuzi ambamo wanaume ni wengi vinapaswa kuwa ni aibu kwa wote kama si kwa wanaume pekee.”

Shujaa halisi: Mwanamke Afghanistan akiondoka nyumbani hana uhakika wa kurejea

Kutoka Afghanistan, Zarqa Yaftali, mkuu wa shirika la kiraia la utafiti wa kisheria kwa wanawake na watoto amesema “kila uchao wanawake nchini Afghanistan wanaondoka nyumbani bila kuwa na uhakika iwapo watarejea. Zaidi ya raia 100,00 wameuawa katika muongo uliopita pekee. Mapigano yanaua zaidi wanawake na watoto wa kike. Asilimia 70 ya wanawake wa Afghanistan hawajui kusoma na kuandika, asilimia 35 ya watoto wa kike wameozeshwa kabla ya kutimiza umri wa miaka 18, na asilimia 87 ya wanawake wanakabiliwa na ukatili wa kijinsia.”
Hata hivyo amesema licha ya changamoto, wanawake wa Afghanistan, wameendelea kufanya kazi bila kuchoka katika mazingira magumu na kwamba wanawake hao leo hii chini ya uongozi wa sasa wanachanua na kustawi baada ya kunyimwa haki zao za msingi wakati wa utawala wa watalibani.