Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Naibu Katibu Mkuu azungumza na wanafunzi wa shule ya msingi nchini Niger

Naibu Katibu Mkuu Amina Mohammed akikutana na wanafunzi katika shule ya Pays-Bas mjini Niamey, Niger
© UNECA/Daniel Getachew
Naibu Katibu Mkuu Amina Mohammed akikutana na wanafunzi katika shule ya Pays-Bas mjini Niamey, Niger

Naibu Katibu Mkuu azungumza na wanafunzi wa shule ya msingi nchini Niger

Utamaduni na Elimu

Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Amina J Mohammed aliyeko ziarani nchini Niger siku ya Jumatano, alitembelea shule huko Niamey ambapo alizungumzia umuhimu wa kubadilisha mfumo wa elimu na kuhakikisha elimu inatolewa kwa wote bila kukatizwa.

Bi. Mohammed alianza siku yake kwa kutembelea shule ya msingi ya Ecole Pays-Bas - iliyoathiriwa vibaya na moto mwaka 2021 baada ya madarasa yao ya nyasi kushika moto na wanafunzi kuwa wanajifunzia katika majengo ya shule ambayo si salama.

Kwa msaada wa serikali, jumuiya na wadau wengine, Umoja wa Mataifa ulikarabati jengo la shule, kujenga madarasa ya ziada na kutoa samani muhimu na vifaa vya kujifunzia.

Wakiwa wameketi katika darasa lao jipya, Naibu Katibu Mkuu huyo wa UN alizungumza na kundi la wanafunzi, wasichana na wavulana, ambao walimuelezea ndoto zao na matarajio yao ya siku zijazo, huku wakielezea baadhi ya changamoto.

Naibu Katibu Mkuu alisema, "Nilichojifunza kutokana na mazungumzo yetu ya kuvutia, kutoka kwao wote wasichana na wavulana, ni umuhimu wa elimu kwao, na jinsi walivyounganisha elimu na kile wanachotaka kufanya."

Wanafunzi wa shule ya Pays-Bas mjini Niamey, Niger wakikutana na Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Amina Mohammed
© UNECA/Daniel Getachew
Wanafunzi wa shule ya Pays-Bas mjini Niamey, Niger wakikutana na Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Amina Mohammed

Kituo cha kidijitali

Naibu Katibu Mkuu, akiwa na timu ya Umoja wa Mataifa nchini Niger na wadau pia walikabidhi kituo cha kidijitali kinachotumia nishati ya jua kwa shule hiyo, pamoja na kompyuta mpakato (laptop), ambazo wanafunzi wanaweza kutumia kupata intaneti.

Kuhusu kituo hicho Bi. Mohammed alisema "hiki kituo kinaunganisha Niger na Afrika, Afrika kwa dunia, na kwa lugha nyingine ni sawa na kusema ulimwengu unafika Afrika na, na hayo ni maendeleo."

Naibu Katibu Mkuu anaamini kuwa "huo ndio mustakabali unaoweza kufikiwa" na "huo ni kufungua uwezo kwa kila mtu nchini Niger, kuwa na ujuzi na uwezo wa kujihusisha kiuchumi, kujihusisha na haki za kimsingi, na kuhakikisha kuwa jamii hii inastawi.”

Kwa upande wake mwalimu Abdoulaye Haoua Dabougui, aliyepata mafunzo ya kutumia kampyuta alishukuru kwa elimu wanayopata kituoni hapo. “Nawashukuru sana kwa msaada huu. Unasaidia sana kwa sababu mimi binafsi sikutarajia. Nimetapa mafunzo ya wiki moja.”