Skip to main content

UNESCO: Watoto milioni 6 hawaendi shuleni

Mtoto mvulana mwenye umri wa kuenda shule anafanya kazi katika mradi wa uchimbaji wa granite katika kitongoji cha Ouagadougou, Burkina Faso.
© UNICEF/Frank Dejongh
Mtoto mvulana mwenye umri wa kuenda shule anafanya kazi katika mradi wa uchimbaji wa granite katika kitongoji cha Ouagadougou, Burkina Faso.

UNESCO: Watoto milioni 6 hawaendi shuleni

Utamaduni na Elimu

Ripoti ya mwaka 2023 ya Ufuatiliaji wa Elimu Duniani iliyotolewa leo na Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu Sayansi na Utamaduni UNESCO inaonesha kuwa kumekuwa na ongezeko wa watoto na vijana milioni sita wasioenda shule tangu mwaka 2021 na kufanya idadi ya wanafunzi ambao hawapo shuleni kufikia milioni 250. 

Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari hii leo Mkurugenzi Mkuu wa UNESCO Aidrey Azoulay amesema ongezeko hilo kwa kiasi limechangiwa na wanafunzi wa kike na wanawake kutengwa katika kupata elimu nchini Afghanistan lakini pia sababu nyingine ni kuendelea kudumaa katika maendeleo ya elimu duniani kote.

“Elimu iko katika hali ya dharura.” Amesema Azoulay na kueleza kuwa ingawa juhudi kubwa zilifanywa katika miongo kadhaa iliyopita ili kuhakikisha elimu bora kwa wote, lakini takwimu za UNESCO zinaonesha kuwa idadi ya watoto wasioenda shule sasa inaongezeka. 

“Mataifa lazima yajipange upya kama hawataki kuuza mustakabali wa mamilioni ya watoto.” 

Matokeo haya yanarudisha nyuma utekelezaji wa lengo namba 4 la Malengo ya maendeleo endelevu SDG ambayo yamepangwa kufikiwa ifikapo mwaka 2030.

Mkuu huyo wa UNESCO amebainisha kuwa kulingana na uchambuzi uliofanywa na ofisi yake “Iwapo nchi zingekuwa kwenye mstari na malengo yao ya kitaifa ya SDG 4, watoto milioni 6 zaidi walio katika umri wa kujiunga na shule ya msingi wangekuwa katika shule ya awali, watoto milioni 58 zaidi barubaru na vijana wangekuwa shuleni, na angalau milioni 1.7 zaidi shule za msingi, walimu nao wangepewa mafunzo.”

Ahadi za 2022 zitekelezwe

Hapo mwaka jana katika mkutano wa Umoja wa Mataifa wa Kubadilisha Elimu nchi 141 ziliazimia katika Kubadilisha mifumo yao ya elimu ili kuharakisha maendeleo kuelekea SDG 4. Miongoni mwao, nchi 4 kati ya 5 zililenga kuendeleza mafunzo ya walimu na maendeleo ya kitaaluma, 7 kati ya 10 zilijitolea kuongeza au kuboresha uwekezaji katika elimu na 1 kati ya 4 alijitolea kuongeza msaada wa kifedha na chakula cha shule.

Bi. Azoulay amesema wakati umefika sasa kwa ahadi hizo kutimizwa “Ahadi hizi lazima sasa zionekane katika vitendo. Hakuna wakati zaidi wa kupoteza. Ili kufikia SDG 4, mtoto mpya anahitaji kuandikishwa shuleni kila baada ya sekunde 2 kati ya sasa na 2030.”

Ili nchi kufikia malengo yao, wanafunzi milioni 1.4 wanahitaji kuandikishwa katika elimu ya awali kila mwaka hadi 2030, na maendeleo katika viwango vya kuhitimu elimu ya msingi yanahitaji kuongezwa kwa karibu mara tatu.