Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kampeni ya chanjo ya kipundupindu Msumbiji yalenga watu 720,000: WHO

Kampeni ya chanjo ya kipindupindu imezinduliwa katika wilaya ya Caia jimboni Sofala nchini Msumbiji
© Sofala District Health Directorate/Zainabo
Kampeni ya chanjo ya kipindupindu imezinduliwa katika wilaya ya Caia jimboni Sofala nchini Msumbiji

Kampeni ya chanjo ya kipundupindu Msumbiji yalenga watu 720,000: WHO

Afya

Shirika la afya la Umoja wa Mataifa duniani WHO limesema Msumbiji leo imeanza kampeni ya chanjo ya kipindupindu inayolenga takriban watu 720,000 katika wilaya nane huku nchi hiyo ikichukua hatua za kudhibiti kusambaa kwa mlipuko huo ambapo hadi sasa wagonjwa 5260 na vifo 37 vimerekodiwa tangu kuzuka Septemba 2022. 

 

Shirika hilo linasema watu wenye umri wa mwaka mmoja na zaidi watapata chanjo katika kampeni ya siku tano, ambayo imeanza siku 10 tu baada ya nchi hiyo kupokea chanjo.  

Mbali ya kampeni ya chanjo, mamlaka za afya nchini humo pia zinaimarisha ufuatiliaji wa magonjwa, hatua za kuzuia na kudhibiti, matibabu pamoja na kuongeza uelewa wa umma ili kuzuia kuenea kwa ugonjwa huo na kukomesha mlipuko huo. 

Wagonjwa wa kipindupindu wameongezeka kwa kasi Afrika mwanzoni mwa mwaka 2023
© WHO
Wagonjwa wa kipindupindu wameongezeka kwa kasi Afrika mwanzoni mwa mwaka 2023

Umuhimu wa kampeni hii ya chanjo 

"Kampeni hii ya chanjo itakuwa muhimu katika kukomesha kusambaa kwa kipindupindu na kusaidia kuokoa maisha ya watu. Pia tunafanya kazi na mamlaka za afya ili kuimarisha hatua muhimu za kukabiliana na milipuko na tumepeleka wafanyakazi katika mikoa mitatu iliyoathiriwa zaidi ili kusaidia mamlaka za afya za mikoa kugundua, kuzuia na kukomesha ugonjwa wa kipindupindu."amesema Dkt. Severin von Xylander, mwakilishi wa WHO nchini Msumbiji. 

 WHO pia imetoa dola 856,000 kusaidia kukabiliana na kipindupindu Msumbiji na kutoa vifaa vya matibabu na madawa.  

Msumbiji imerekodi ongezeko kubwa la wagonjwa tangu katikati ya mwezi Desemba 2022.  

Kipindupindu hadi sasa kimeripotiwa katika majimbo matano kati ya 11 ya nchi hiyo. Mikoa ya kaskazini ya Niassa, Sofala na Tete ndiyo iliyoathiriwa zaidi. 

Wakati huu wa kampeni ya chanjo watoa chanjo wanatumia mbinu mseto ya kutoa chanjo kwa wagonjwa katika vituo vya afya, kupitia timu zinazotembea na kwa kuwatembelea watu nyumba kwa nyumba.  

Chanjo za kipindupindu kwa njia ya matone zitatumika pamoja na uboreshaji wa maji na usafi wa mazingira ili kudhibiti milipuko ya kipindupindu na kuzuia kusambaa zaidi katika maeneo yanayojulikana kuwa hatarishi kwa ugonjwa huo. 

Kampeni inaendeshwa kwa ushirikiano na wadau 

"Tunasherehekea uzinduzi wa kampeni hii muhimu ya chanjo pamoja na Serikali ya Msumbiji na muungano wa washirika wetu”. Amesema Thabani Maphosa, ,mkurugenzi mkuu, wa program za nchi za utoaji chanjo wa GAVI, ambayo ni muungano wa chanjo duniani.  

Ameongeza kuwa "Ongezeko la hivi karibuni la milipuko ya magonjwa na hatari zinazojitokeza linaonyesha umuhimu wa kazi yetu katika kufadhili hifadhi ya kimataifa ya chanjo ya kipindupindu, kampeni za kukabiliana na kipindupindu na upatikanaji wa chanjo za kukabiliana na milipuko ya magonjwa kama vile kipindupindu, surua, homa ya manjano na polio." 

 Licha ya uhaba wa chanjo ya kipindupindu duniani na kuongezeka kwa mahitaji kutokana na kuongezeka kwa milipuko duniani, WHO na washirika wake, ikiwa ni pamoja na GAVI, na vituo vya Afrika vya kudhibiti magonjwa wameweza kusambaza chanjo kwa nchi zilizoathirika zaidi na kipindupindu kusini mwa Afrika ambapo Msumbiji imepokea takriban dozi 720,000 za chanjo ya kipindupindu.

UNICEF inashiriki katika ufuatiliaji wa kukutana na familia zilizoathirika na na mvua kubwa zilizosababisha mafuriko Kusini mwa Msumbiji
© UNICEF/Cremildo Assane
UNICEF inashiriki katika ufuatiliaji wa kukutana na familia zilizoathirika na na mvua kubwa zilizosababisha mafuriko Kusini mwa Msumbiji

 

Hatari ya ugonjwa wa kipindupindu 

Kipindupindu ni maambukizi makali na hatari sana ambayo yanaweza kuenea kwa haraka na kusababisha upungufu wa maji mwilini , maradhi mengine na vifo vingi. Hata hivyo, ugonjwa huo unatibika kwa urahisi limesema shirika la WHO likiongeza kuwa watu wengi wanaweza kutibiwa kwa ufanisi kwa kutumia mara moja dawa ya kurudisha maji mwilini oral dehaydration solution au kuongezwa maji mwilini kupitia kwenye mishipa. 

Ugonjwa wa kipindupindi ni wa kawaida nchini Msumbiji pamoja na magonjwa mengine ya kuhara, ni sababu kubwa ya vifo vya watoto wachanga.  

Kumekuwa na milipuko ya kila mwaka katika majimbo ya kaskazini mwa nchi hiyo.  

Maambukizi ya kipindupindu yanahusiana kwa karibu na hali duni ya vyoo na upatikanaji duni wa maji safi ya kunywa. Matukio makubwa ya hali ya hewa kama vile ukame na mafuriko yanazidisha hatari za kipindupindu.  

Nchini Msumbiji, mafuriko yaliyotokana na msimu huu wa mvua yameathiri zaidi ya watu 39,000, na kusababisha vifo vya watu tisa na k uharibifu mkubwa wa miundombinu, ikiwa ni pamoja na barabara, madaraja, vituo vya afya na nyumba 76,000.