Msumbiji yahitimisha kampeni ya dharura ya chanjo dhidi ya Kipindupindu

9 Aprili 2019

Nchini Msumbiji, Wizara ya afya inakamilisha kampeni ya dharura ya chanjo dhidi ya ugonjwa wa kipindupindu ambapo hadi sasa wameshafikia watu 745 609 katika wilaya nne zilizokumbwa na kimbunga Idai.

Msemaji wa shirika la afya ulimwenguni, WHO mjini Geneva, Uswisi, Tarik Jašarević amewaambia waandishi wa habari kuwa chanjo hizo zilizotolewa na fuko la chanjo duniani, GAVI zilianza kupatiwa wahusika tarehe 2 mwezi huu na ndani ya saa 24 wahitaji walishafikiwa.

Bwana Jašarević amesema chanjo zilizosalia zinatumika kuhakikisha kuwa hakuna pengo lolote la wahitaji wanaotakiwa kupatiwa kwenye jamii na pia kwenye maeneo ambayo bado hayajafikiwa.

Kampeni hiyo inayoongozwa na Wizara ya afya ya Msumbiji, na msaada kutoka WHO, shirika la Umoaj wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF na shirika la madaktari wasio na mipaka, MSF, shirikisho la  msalaba mwekundu, IFRC na Save the Children, inahusisha wafanyakazi wa kujitolea zaidi ya 1200.

UNICEF/DE WET
Wahudumu wa afya wakiwa nje ya hema linalotumika kwa ajili ya matibabu ya kipindupindu yaliyoandaliwa na MSF, UNICEF na msaaba mwekundu katika kituo cha afya cha Macuruguo mjini Beira.

Waliopatiwa chanjo ni watu waliotambuliwa na serikali kuwa wako hatarini zaidi kupata kipindupindu ambao ni wale wasio kuwa na uwezo wa kupata maji safi na salama na wanapatikana wilaya hizo nne za Beira, Dondo, Nhamatanda na Buzi.
Msemaji huyo wa WHO amefafanua kuwa mafanikio yametokana na mwitikio chanya kutokakwa jamii ambapo dozi moja ya chanjo inampatia mtu asilimia 85 yakinga dhidi ya kipindupindu kwa kipindi cha miezi sita.

“Pindi asilimia 60 ya jamii inakuwa  imepatiwa chanjo, hii inatosha kabisa kupatia jamii nzima ulinzi dhidi ya kipindupindu,” amesema Bwana Jašarević.

Tangu kimbunga Idai kipige Msumbiji tarehe 14 mwezi Machi, mamia ya maelfu ya watu wamekuwa wanaishi kwenye makazi ya muda bila huduma ya maji safi na salama pamoja na huduma za kujisafi.

UNICEF/UN0293297/DE WET
Watoto wakionekana wakitembea kwenye matope baada ya kimbunga Idai kupiga eneo hili la Buzi nchini Msumbiji tarehe 14 mwezi Machi mwaka 2019

Wizara ya afya nchini Msumbiji ilitangaza tarehe27 mwezi uliopita wa Machin a hadi tarehe 8 mwezi huu wa Aprili zaidi ya wagonjwa 3577 wameripotiwa ambapo kati yao, 6 wamefariki dunia.

WHO inasema kuwa chanjo dhidi ya kipindupindu ni mbinu mojawapo tu ya kudhibiti mlipuko lakini hatua mahsusi kwa watu wenye dalili ni kupata matibabu na jamii kupatiwa maji safi na salama na huduma za kujisafi.

Hadi sasa nchini Msumbiji kuna vituo 12 vya kutibu kipindupindu vikiwa na vitanda 500 na vimeandaliwa na mamlaka za Msumbiji kwa ushirikiana na wadau wa kimataifa.

 

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud

Fuatilia Habari: Habari zilizopita za Mada Hii

Athari za IDAI za anika mzigo wa madeni ya siri Msumbiji-UN

Athari za kimbunga Idai kilichoikumba Msumbiji na kwingineko kimeanika hadharani mzigo wa madeni ya siri ambayo hayajalipwa nchini Msumbuji kwa mujibu wa mtalaam wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa.