Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Nalaani vikali mashambulizi yanayoendelea dhidi ya raia na wahudumu wa misaada: Nyanti

Wakimbizi wa ndani wakikimbia machafuko huko Abyei, Sudani Kusini
© UNOCHA/Dan De Lorenzo
Wakimbizi wa ndani wakikimbia machafuko huko Abyei, Sudani Kusini

Nalaani vikali mashambulizi yanayoendelea dhidi ya raia na wahudumu wa misaada: Nyanti

Amani na Usalama

Mratibu wa masuala ya kibinadamu wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini Sara Beysolow Nyanti,amelaani vikali machafuko yanayoendelea kote nchini ambayo yanaathiri usalama wa raia na wahudumu wa misaada ya kibinadamu , yanatatiza fursa za kufikisha misaada na kuingilia usambazaji wa misaada na huduma kwa watu walio hatarini zaidi.

Akitoa mfano Bi Nyanti amesema tarehe 10 Februari muuguzi ambaye alikuwa akifanyakazi na shirika la misaada la kimataifa aliuawa pamoja na raia wengine wakiwemo wahudumu wa misaada ya kibinadamu walijeruhiwa huko Agok kutokana na machafuko ambayo yamekuwa yakiendelea  kaunti ya Twic, jimbo la Warap na Abyei.

Tweet URL

Kwa mujibu wa mratibu huyo wa Umoja wa Mataifa “watu takribani 70,000 wametawanywa na mapigano na operesheni za kibinadmu ikiwemo huduma za afya zimesitishwa kwa muda.”

Muhudumu mwingine wa misaada aliuawa kwa risasi wakati wa mapigano yalitokea katika eneo la MirMir jimbo la Unity.

Bi. Nyanti amesema zaidi ya hayo kituo cha msaada kwa wanawake na wasichana kimeripotiwa kuporwa , huku kituo cha afya na lishe kikifungwa kwa muda jimbopni Unity ambako pia fursa za watu 500,000 wanaohitaji msaada kufikishiwa msaada huo zikitoweka.

Amesisitiza kuwa “Vitendo hivyo vya ukatili dhidi ya raia na wahudumu wa misaada lazima vikome mara moja. Kila siku watu wa Sudan Kusini wanahaha kuweza kuishi na machafuko hayana nafasi katika nchi hiyo ambayo imedhamiria kusonga mbele kuelekea kwenye mustakbali wa amani.”

Ameongeza kuwa “Mashambulizi dhidi ya raia na wahudumu wa kibinadamu na mali zao, sanjari na uharibifu na uporaji wa misaada iliyokusudiwa kwa watu walio hatarini zaidi ni suala lisilokubalika. Kwani pia inathiri kwa kiasi kikubwa uwezo wetu wa kufikisha na kusambaza misaada.”

Machafuko na mvitisho vya mara kwa mara dhidi ya wahudumu wa misaada ya kibinadamu na mali zao vimesababisha wahudumu kuhamishwahamishwa na kusitisha usambazaji wa misaada muhimu ya kuokoa maisha nchini Sudan Kusini.