Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Licha ya changamoto, Afrika ‘ipo tayari kwa maendeleo’ – Guterres

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres akihutubia wakati wa Ufunguzi wa Kikao cha 36 cha kawaida cha AU mjini Addis Ababa, Ethiopia.
UNECA/Daniel Getachew
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres akihutubia wakati wa Ufunguzi wa Kikao cha 36 cha kawaida cha AU mjini Addis Ababa, Ethiopia.

Licha ya changamoto, Afrika ‘ipo tayari kwa maendeleo’ – Guterres

Ukuaji wa Kiuchumi

Ajenda 2063, Muongo wa kuhakikisha wanawake wanashirikishwa kifedha na kiuchumi, utajiri na wingi wa maliasili katika bara la afrika na faida kubwa zaidi ya kuwa na watu, ambao wanawakilisha utajiri wa utofauti mkubwa wa utamaduni na lugha. Yote haya yanaonesha namna ambavyo Afrika ipo tayari kwa ajili ya maendeleo na ina kila sababu ya kuyafikia lakini changamoto iliyopo ni kukosa uungwaji mkono kimataifa kwenye masuala mbalimbali na hivyo kujikuta ikikwama kufikia maendeo kamili.

Hayo yamesemwa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres hii leo wakati akizunguma katika ufunguzi wa kikao cha 36 cha kawaida cha mkutano wa ngazi ya juu ya viongozi wa Muungano wa Afrika, AU jijini Addis Ababa, nchini Ethiopia.

Guterres akitumia dakika 11 kuwasilisha hotuba yake kwa lugha mbili kiingereza na kifaransa mbele ya wakuu wa nchi na serikali wanachana wa Muungano wa Afrika alianza hotuba yake kwa kuupongeza uongozi wa AU na wanachama wote kwa kuungana pamoja katika mkutano huo na kuzungumza kuhusu mada “Afrika iliyoungana, yenye mafanikio na amani.”

Amesema Umoja wa Mataifa inafurahi kuwa mshirika kwa AU na kufanya kazi pamoja na uhusiano wa mashirika hayo mawili upo imara zaidi na kupongeza juhudi zinazofanywa katika kuhakikisha maendeleo kwa bara hilo yanapatikana.

“AU imechukua hatua za kutia moyo ili kusaidia kuonesha uwezo wa bara hili kubwa. Afrika ipo tayari kwa maendeleo. Nimefurahia kuona mkazo uliowekwa kwenye kutengeneza ajira kwenye eneo la biashara huria kwa bara la Afrika, jambo hili litawasilisha mabadiliko ya kweli ikiwa njia ya kwenda kuunda ajira nyingi na vyanzo vingine vingi vya ustawi kwa afrika hususan kwa vijana.”

Hata hivyo pamoja na juhudi zote hizo bado Guterres ameeleza kutambua namna Afrika inavyopitia kwenye changamoto nyingi. Pamoja na kuwa changamoto hizo pia zinakumba kila kona ya dunia lakini Afrika ndio imekuwa ikipata machungu zaidi.

Makao Makuu ya Muungano wa Afrika, mjini Addis Ababa, Ethiopia
UNECA/Daniel Getachew
Makao Makuu ya Muungano wa Afrika, mjini Addis Ababa, Ethiopia

Miongoni mwa changamoto zinazolitesa zaidi bara la Afrika ni

  1. Mfumo wa kifedha wa kimataifa - usiofanya kazi vizuri na usio na usawa ambao umezifanya nchi zinazoendelea kushindwa ufikiaji wa fedha hata pale wanapokuwa na uhitaji zaidi
  2. Kukosekana kwa usawa kwenye upatikanaji wa rasilimali za kuweza kukabiliana na hali baada ya janga la COVID-19.
  3. Mgogoro wa kupanda kwa gharama ya maisha - uliozidishwa na matokeo ya Urusi kuivamia Ukraine.
  4. Athari za Mabadiliko ya Tabianchi- ambayo watu wengi wa wamesababisha uharibifu kwa kiasi kidogo sana lakini wao ndio wanaathirika zaidi ya Mafuriko, ukame mkali kuwahi kushuhudiwa, hali inayoziweka jamii nyingi matatani na mamilioni ya watu kuwa wakimbizi.
  5. Changamoto nyingine nyingi za amani na usalama ambazo zinahusisha maslahi ya watu walio nje ya mipaka ya bara la Afrika.

Na katika changamoto zote hizi Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa amesema ujumbe upo wazi kabisa kuwa Afrika inahitaji kuchukua hatua, na akazitaja hatua tatu ambazo zinapaswa kuchukuliwa.

Ripoti ya UNCTAD kuhusu maendeleo ya uchumi Afrika inataka udhiibiti wa utoroshaji wa fedha barani humo ambao hupora mitaji yenye thamani ya takribani dola bilioni 89 kila mwaka. ( Maktaba)
Unsplash/Jason Leung
Ripoti ya UNCTAD kuhusu maendeleo ya uchumi Afrika inataka udhiibiti wa utoroshaji wa fedha barani humo ambao hupora mitaji yenye thamani ya takribani dola bilioni 89 kila mwaka. ( Maktaba)

Mosi- Hatua za kiuchumi

“Afrika ina utajiri wa Uwezo lakini haina utajiri wa uungwaji mkono Mikataifa” amesema Guterres na kutaka mindombinu ya upatikanaji wa fedha iweze kurekebishwa ili nchi za afrika ziweze kufanya uwekezaji zaidi kitu ambacho kwa sasa hakifanyiki kutokana na mifumo ya utapikanaji wa fedha mbali na kutoza riba kubwa kwenye fedha zinazokopwa lakini pia zina masharti magumu kuweza kutimizwa.

Mazingira hayo magumu ya upatikanaji wa fedha yanaathiri jamii za afrika kwneye maeneo kama elimu, afya, matumizi ya nishati jadidifu na ulinzi wa kijamii na kubwa zaidi kushindwa kutengeneza ajira ambazo zingeweza kuinua uchumi wa jamii nyingi.

“Nchi za Kiafrika haziwezi kuwekeza katika maeneo haya muhimu, na kupanda ngazi ya maendeleo kwa mkono mmoja huku mkono mwingine ukiwa umefungwa mgongoni. Nimetoa wito kwenye mkutano wa Bretton Woods nimetaka kuwepo na mabadiliko makubwa kwenye usanifu wa kifedha wa kimataifa. Nimepata jambo la msingi kuzingatiwe mahitaji ya nchi zinazoendelea.”

Guterres pamoja na kuzungumzia ahueni ya madeni kwa nchi za kipato cha chini na cha kati anezitaka pia benki ya maendeleo kubadili miundo yao ya biashara na kuchukua mwenendo mpya ni kwa njia hiyo wataweza kuvutia nchi kutafuta mitaji.

“Pia nitaendelea kuzisukuma nchi tajiri Zaidi duniani G20 kuendelea kuchochea utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu SDGs ili kuzisaidia nchi za kusini. Mkutano wa SDG unafanyika mwezi Septemba mwaka huu, lazima uwe wakati wa mafanikio katika kutoa usaidizi kwa nchi zinazoendelea na kurekebisha mfumo wa kifedha wa kimataifa uliovunjika.” Alitoa ahadi Guterres huku akisema ataendelea kusimama na Afrika katika kupigania hilo.  

Wanaharakati vijana wakitoa ujumbe wao kwa washiriki wa COP27 wakidai fidia kwa hasara na uharibifu kwa nchi maskini kutokana na jinsi zinaathiriwa na mabadiliko ya tabianchi.
Kiara Worth
Wanaharakati vijana wakitoa ujumbe wao kwa washiriki wa COP27 wakidai fidia kwa hasara na uharibifu kwa nchi maskini kutokana na jinsi zinaathiriwa na mabadiliko ya tabianchi.

Mbili – Mabadiliko ya tabianchi

Athari za mabadiliko ya tabianchi ni thabiti kwa kuangalia mafuriko ukame, njaa na joto Kali bara la Afrika linalokabiliana nalo. Nchi hizo ambazo zimesababisha uharibifu kidogo ndio zinaathirika zaidi.

Guterres amesema hatua madhubuti za kukabiliana na changamoto hizo zinahitajika nakupongeza hatua kadhaa zilizochukuliwa n anchi kama Kenya na Jamhurii ya Kidemokrasia Kongo DRC.

“Nchi kadhaa za Kiafrika zinaonesha uongozi thabiti juu ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi. Mkakati wa uchumi wa kijani wa Kenya, juhudi za kulinda misitu ya kitropiki ya Kongo, Ushirikiano wa Nishati wa Mpito wa Afrika Kusini na Mpango kabambe wa AU wa kuchochea matumizi ya nishati safi.” Alitaja baadhi ya miradhi hiyo na kuongeza kuwa “ Nimetiwa moyo na jukumu kuu la Nchi za Visiwa Vidogo vya Afrika, jukumu wanalotekeleza katika kutetea Mpango Mkuu wa Ukuta wa Bluu.”

Hata hivyo pamoja na juhudi zote hizo amesema lazima dunia ipunguze matumizi ya nishati inayoharibu tabaka la ozoni na kuhamia katika nishati jadidifu. Pia amepongeza miradi yote inayozingatia utunzaji wa amzingira na ahadi zilizotolewa katika Mkutano COP27 lazima yatekelezwe wakati dunia ikijiandaa kwa mkutano mwa mwaka huu COP28.

Wakimbizi kutoka Somalia wakiwasili katika kambi ya wakimbizi ya Burumino nchini Ethiopia. Kutokana na mvua duni, na kuendelea kwa ukosefu wa usalama nchini Somalia, idadi ya wakimbizi katika kambi hiyo iliongezeka. (Maktaba)
UNICEF/Jiro Ose
Wakimbizi kutoka Somalia wakiwasili katika kambi ya wakimbizi ya Burumino nchini Ethiopia. Kutokana na mvua duni, na kuendelea kwa ukosefu wa usalama nchini Somalia, idadi ya wakimbizi katika kambi hiyo iliongezeka. (Maktaba)

Tatu – Afrika inahitaji Amani

 Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa amesema anafurahi vile shirika hili ni washirika wa kuhakikisha Afrika ina amani na wanafanya kazi kwa kila nji katika kuhakikisha hilo linatimia iwe kwa mikutano ya ana kwa ana Ama kwa njia ya mtandao.

Hata hivyo kuna changamoto kadhaa ikiwemo ugaidi na kuzidi kuibuka kwa mizozo akitolea mfano nchini DRC ambapo hivi karibuni kumezidi kuibuka kwa makundi yenye silaha huko mashariki wa DRX pamoja na makundi ya kigaidi huko ukanda wa Sahel pamoja na maeneo mengine.

“Sote tunajua kuwa amani inaweza kupatikana. Makubaliano ya kusitisha mapigano yaliyofikiwa hapa nchini Ethiopia chini ya uangalizi wa AU - na ninampongeza Waziri Mkuu Abiy Ahmed kwa kufanikisha mchakato huo - usitishaji vita ulioanzishwa nchini Libya na amani ya Sudan Kusini na Jamhuri ya Afrika ya Kati, pamoja na maendeleo yanayoonekana nchini Somalia, zote ni habari za matumaini. Lazima tuendelee kupigania amani.”

Hata hivyo Guterres alisema pamoja na juhudi hizo lakini ni wazi kabisa kuwa bado kuna kuyumba kwenye taratibu za kusaka amani.

“Ajenda Mpya ya Amani tunayopendekeza ndani ya Umoja wa Mataifa inalenga kuleta uhai mpya katika mfumo wa kimataifa na kuimarisha shughuli zetu za amani duniani kote. Angenda hii inajengwa kwa kufikiriwa kutoka kwenye mtazamo wa jumla - kutambua sababu kuu za migogoro na kuzuia mbegu za vita kuota.”

Pamoja na kuzungumzia kwa upana zaidi eneo hili la amani na usalama barani Afrika Guterres alieleza pia wanaunga mkono kikamilifu kuundwa kwa kizazi kipya cha utekelezaji wa amani kinacho ongozwa na Umoja wa Ulaya na operesheni za kukabiliana na ugaidi Afrika na kwa mamlaka ya Baraza la Usalama chini ya Sura ya VII - pamoja na ufadhili wa uhakika ikijumuisha kupitia michango iliyotathminiwa kwanza kabla ya kukubaliwa.

“Na lazima tuendelee kuimarisha ushirikiano wetu katika mipango mikuu ya amani, kama tulivyofanya na Jopo Huru la Ngazi ya Juu kuhusu Usalama na Maendeleo katika Sahel. Ninatazamia kufanya kazi nanyi (AU) kunyamazisha bunduki na kuunda mazingira ya amani - amani inayohitajika sana kwa watu bilioni 1.4 wanaoishi Afrika.”

Guterres alihitimisha hotuba yake kwa kusema “Karne ya 21 ina kila kitu cha kuifanya kuwa karne ya Afrika na Umoja wa Mataifa umejitolea kufanya kazi na kila mmoja wenu ili kufungua uwezo huu mkubwa na kushinda vikwazo vinavyotuzuia.Tuchukue hatua kwa ajili ya Afrika.