Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNMISS wakarabati mahakama na kujenga jela mpya jimboni Equatorial magharibi

Umoja wa Mataifa unaunga mkono juhudi za kujenga amani kwa jamii katika jamii za Sudan Kusini.
UN Photo/Isaac Billy
Umoja wa Mataifa unaunga mkono juhudi za kujenga amani kwa jamii katika jamii za Sudan Kusini.

UNMISS wakarabati mahakama na kujenga jela mpya jimboni Equatorial magharibi

Wahamiaji na Wakimbizi

Katika kuhakikisha wanawavutia wakimbizi wa ndani kurejea makwao, ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini UNMISS, umekarabati na kukabidhi jengo la mahakama pamoja na kujenga jengo jipya la jela huko jimboni Equatorial Magharibi katika kaunti ya Maridi.

Nchini Sudan Kusini wananchi waliokuwa wakimbizi wa ndani na sasa wameanza kurejea katika vijiji vyao wanataka kurejea katika mazingira ambayo kuna utawala wa sheria.

Sarah Barnet ni kiongozi wa wanawake wa kaunti ya Maridi iliyoko jimboni Equatorial Magharibi, 

“Tunahitaji kuona haki ikitendeka, hasa kwa wanawake. Kuna kesi nyingi za unyanyasaji wa kijinsia katika jamii yetu, na zinapaswa kushughulikiwa na mahakama. Haki zetu kama wanawake lazima ziheshimiwe.”

Kwakutambua hili na kutekeleza jukumu lake la kuhakikisha wanalinda amani na kuimarisha mifumo ya haki nchini Sudan Kusini UNMISS wametekeleza mradi uliogharimu takriban dola 100,000 kwa kukarabati jengo la mahakama ya kaunti ya Maridi na kujenga jengo jipya la jela ili yaweze kutoa huduma ya kuhakikisha sheria zinafuatwa na wale wasiofuata sheria jela mpya iliyojengwa lipo kwa ajili yao.

Ibrahim Tahiru ni afisa wa Ulinzi, Mpito na Uunganishaji wa UNMISS na anasema wanachukulia utekelezaji wa miradi hii ya kuleta mabadiliko haraka kuwa ni kichocheo muhimu cha kuwavutia watu wengi zaidi kuweza kurejea makwao kutoka ukimbizini,

"Tunaamini kuwa tutaweza kukuza hali ya kudumu ya watu kurejea makwao na kuwaunganisha wakimbizi hawa wa ndani pamoja na waliokimbilia nje ya mipaka ya nchi. Tunataka waweze kujisikia kulindwa na kujua kwamba hawata pokonywa mali zao kiholela. Pia tunataka wajue watalipwa ikiwa, walipokuwa wakikimbia mzozo baadhi ya mali zao zilichukuliwa na watu wengine. Kwa hivyo, taratibu zote hizi kama ujenzi wa mahakama na jela zinategemeana. Tunaamini kuwa mfumo madhubuti wa haki utawasaidia sana watu wanaotafuta haki.”

Ujumbe wa Umoja wa Mataifa ya kulinda amani nchini humo, UNMISS haujajitolea tu kuboresha uwezo wa mfumo wa haki nchini Sudan Kusini, bali pia kukuza heshima na kufuata matakwa ya haki za binadamu.

Jamii ikiwa imewekewa mazingira bora ya kuwawajibisha wahalifu, ukiukaji wa haki za binadamu unatarajiwa kupungua.