Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Maelfu ya wakimbizi wa ndani wa Tambura warejea makwao

Watu walioyakimbia makazi yao katika eneo la Equatoria Magharibi Sudan Kusini wakikutana na viongozi wa vijiji.
UNMISS
Watu walioyakimbia makazi yao katika eneo la Equatoria Magharibi Sudan Kusini wakikutana na viongozi wa vijiji.

Maelfu ya wakimbizi wa ndani wa Tambura warejea makwao

Amani na Usalama

Sudan Kusini ni moja ya nchi iliyoathirika kwa muda mrefu na vita vya wenyewe kwa wenyewe ambapo mara kwa mara makundi ya wapiganaji wenye silaha yalikuwa yakivamia katika vijiji na kuwaua raia na kupora mali zao. Kutokana na sababu hiyo wananchi wengi wamekuwa wakikimbilia katika kambi za kijeshi zilizoko karibu na maeneo yao ili kusaka hifadhi.

Lakini mazungumzo na mipango ya amani inayotelekezwa nchini humo kwa ushirikiano wa serikali, Umoja wa Mataifa na wadau wengine umeleta matunda na sasa maeneo mengi amani na utulivu umerejea. Moja ya maeneo hayo ni katika jimbo la Equotoria Magharibi ambapo maelfu ya wakimbizi waliokuwa katika kambi za wakimbizi wa ndani za eneo la Tambura kuanzia mwishoni mwa mwaka jana 2022 wameanza kurejea makwao ili kuendelea na maisha ikiwemo watoto kurejea shuleni na kuendelea na shughuli za kilimo.

Mary Sebit ni mmoja kati ya maelfu ya watu walioamua kurejea makwao, yeye alirejea mwezi Novemba mwaka 2022. Hapo awali walikimbilia katika kambi za wakimbizi zilizoko eneo la Tambura kutokana na vijiji vyao kuvamiwa na watu wenye silaha.

Akisimulia hali ilivyokuwa anasema "nilikimbilia katika kambi za jeshi zilizo karibu na kijiji chetu. Maisha huko yalikuwa magumu sana. Hakukuwa na kitu cha kula. Niligundua kwamba nikiendelea kukaa huko, maisha yangu na watoto wangu hayatakuwa sawa, kwa hiyo niliamua kurudi nyumbani na watoto wangu wote.”

Waswahili husema nyumbani ni nyumbani na Mary anasema licha ya changamoto wanazokabiliana nazo kwa sasa lakini anafurahia kurejea nyumbani na anasubiri msimu wa mvua uanze na ombi lake ni “Hatuombi chakula, bali watuletee angalau mbegu na zana tutakazo tumia kupanda mbegu hizo. Hilo tu litatusaidia.”

Lakini si wote waliokimbilia katika kambi za wakimbizi wamefanya maamuzi ya kurejea katika vijiji vyao, Angelina Lazaro yeye bado yupo kambini na anasema “Sina nyumba. Sina hata karatasi ya plastiki ninayoweza kutumia kuezeka nyumba nikirejea katika makazi yangu ya zamani. Nilimpoteza mume wangu wakati wa mzozo. Niko peke yangu, basi ni nani awezaye kunijengea nyumba?”.

Katika kuhakikisha changamoto za wanaorejea makao zinatatuliwa, timu ya tathmini ya UNMISS inatembelea maeneo ya wananchi wanaorejea na kushuhudia changamoto ambazo wahamiaji hao wanakabiliana nazo.

Thomas Bazawi, ni afisa Ulinzi, Mpito na Uunganishaji wa UNMISS, ambaye anasema watu wengi wameamua kurejea nyumbani ili kuungana na vyanzo vyao vya kujikimu na ili pia waweze kuwapeleka watoto wao shule na kuendelea na shughuli zao za kilimo.

“Kama unavyoona nyuma yangu, mahema haya ya muda yanakaribia kuwa tupu. Mengi yapo matupu hakuna watu. UNMISS kama mshirika wa amani, itafanya kazi ya kuunga mkono serikali. Lakini zaidi, tunaiomba serikali ifanye utambuzi wa maeneo yenye msongamano mkubwa wa watu wanaorejea, na sisi tutaona jinsi gani tunaweza kuwasaidia kwa fedha kidogo tulizonazo za miradi ya kuleta mabadiliko kwa haraka kwa ajili ya kuziba baadhi ya mapengo ya huduma ambazo wananchi wanaorejea wanakumbana nazo”