Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNFPA: Tetemeko la ardhi limevunja si tu majengo ya Syria bali pia matumaini yao

Laila Baker Mkurugenzi wa UNFPA wa nchi za Kiarabu, atembelea Aleppo, Syria kufuatia tetemeko kubwa la ardhi
UNFPA
Laila Baker Mkurugenzi wa UNFPA wa nchi za Kiarabu, atembelea Aleppo, Syria kufuatia tetemeko kubwa la ardhi

UNFPA: Tetemeko la ardhi limevunja si tu majengo ya Syria bali pia matumaini yao

Msaada wa Kibinadamu

Mkuu wa kanda ya nchi za kiarabu katika shirika la Umoja wa Mataifa la Idadi ya watu duniani, na afya ya uzazi, UNFP Laila Baker amesema pamoja na shirika hilo kuhitaji fedha ili kuweza kuwahudumia wanawake na wasichana waliathiriwa na matetemeko nchini Turkiye na Syria lakini kila sehemu anapopita nchini Syria wanawake hutoa ombi moja tu nalo ni kuhitaji amani.

Soundcloud

Ni Laila Baker huyo, mkuu wa UNFPA katika kanda ya nchi za kiarabu katika mahojiano maalum na Idhaa ya Umoja wa Mataifa akieleza kwa siku nzima amekuwa katika mji wa Aleppo nchini Syria akizunguka kutembelea kliniki zilizoanzishwa na shirika hilo linalohusika na afya ya uzazi na kuzungumza na kila anayehusika katika kukabiliana na dharura iliyoletwa na matetemeko ya ardhi.

Bi. Baker anasema ni vigumu sana kwake kueleza kwa sentensi moja au kuchora taswira ya madhila waliyomo wananchi wa Syria kwani madhara si katika miundombinu pekee bali pia kimwili kwani watu hawa kwa takriban muongo mmoja wamekuwa wakihaha kutokana na nchi hiyo kuwa na mizozo na vita.

“Kuna majengo ambayo yameanguka, mtaa mzima umebomolewa, lakini kubwa zaidi ni muunganiko wa uchovu mwingi wa watu hawa ambao wamekuwa wakipigania uwepo wao, na sasa wanahisi kwamba wakati huo huo wanaanza kurudi katika matumaini wakiona mwanga mwisho wa handani ukiangaza kuwapa matumaini, janga la asili linatokea. Tetemeko hili kubwa la ardhi limevunja matumaini yao, kama jinsi majengo yalivyobomoka wakati wa tetemeko lenyewe.”

Lakini wanawake na wasichana aliokutana nao ni nini hasa wanataka?

Tweet URL

“Nitakuambia kile hasa nilichowauliza wanawake kila mahali nilipoenda. Nikawaambia, kama ningeweza kuiambia jumuiya ya kimataifa jambo moja, ungeniomba niwaambie nini? Na bila kukosea, katika kila kundi la wanawake, hata awe mtu binafsi au kikundi, ujumbe wao ulikuwa sawa. Imetosha. Tumechoka, na tunachotaka ni upatanisho. Tunataka amani. Na tunatumaini katika wakati huu wa giza nene, itakuwa wakati ambapo mioyo na akili za kila mtu ziko wazi kuwa kuna uwezekano wa amani.”

Wengi wa wakimbizi wa ndani nchini Syria ni wanawake na wasichana hivyo hata kabla ya tetemeko la ardhi kulikuwa na mipango kadhaa iliyokuwa ikisimamiwa na UNFPA kwa kushirikiana na wadau wengine ili kusaidia utoaji wa huduma za afya ya uzazi na kukabiliana na unyanyasaji wakijinsia. Na sasa shirika hilo limelazimika kupanua wigo wa huduma zao kwani watu wengi kwa sasa wameweka kuweka makazi ya muda, katika misikiti, shule na bustani ambazo UNFPA imeeleza maeneo hayana vifaa kwa ajili ya wakazi wa kibinadamu kwani wanakosa maji, hawana usafi mzuri wa mazingira, umeme, na nchi hiyo kwas asa ipo katika msimu wa baridi.

Ombi la usaidizi

Ni kutokana na hali hiyo ndio maana Bi.Baker amesema UNFPA imetoa ombi la usaidizi ambapo “kwa Uturuki, ni milioni 19.7. Na kwa Syria ni zaidi ya milioni 24.”

Mbali na fedha hizo kutumika kwa ajili ya wanawake na wasichana ya nchi hizo mbili lakini pia zitatumika kwa ajili ya wafanyakazi wa UNFPA.

“Tutaimarisha watu wetu na uratibu wetu wa kutoa misaada mashinani kwa sababu tuna wajibu wa kuwatunza watoa huduma wetu pia. Naomba usisahau kwamba hawa ni watu ambao, wao wenyewe wamepatwa na kiwewe, na bado wanafanya kazi bila kuchoka usiku kucha. Tuna wafanyakazi ambao wamelala kwenye magari yao kwa siku nane, wakizunguka tu kutoka sehemu moja hadi nyingine baada ya kumaliza kazi na pia kujitolea muda wao. Tunaimani kuwa hiyo itakuwa hatua inayofuata ya kile tunachotowa.”

Mkuu huyo wa UNFPA katika kanda ya nchi za kiarabu alihitimisha mahojiano yake kwa kueleza pamoja changamoto lakini pia kuna habari njema na zakutia moyo ikiwemo wakina mama kuweza kuunganishwa na watoto pamoja na wajukuu zao ambao walipoteana baada ya kutokea kwa tetemeko.