UNFPA yahitaji dola milioni 835 kusaidia wanawake na wasichana katika nchi 61 mwaka 2022

Mwanamke ameshikilia ujumbe unaosema "unafuu" huko Tigrinya wakati wakifanya mazoezi kwenye nyumba salama huko Tigray, Ethiopia.
© UNFPA Ethiopia/Paula Seijo
Mwanamke ameshikilia ujumbe unaosema "unafuu" huko Tigrinya wakati wakifanya mazoezi kwenye nyumba salama huko Tigray, Ethiopia.

UNFPA yahitaji dola milioni 835 kusaidia wanawake na wasichana katika nchi 61 mwaka 2022

Msaada wa Kibinadamu

Shirika la Umoja wa Mataifa linalohusika na idadi ya watu na afya ya uzazi duniani UNFPA, hii leo limezindua ombi maalum la dola milioni 835 likiwa ni ombi lake kubwa zaidi la kibinadamu ili liweze kuwafikia zaidi ya wanawake, wasichana na vijana milioni 54 katika nchi 61 mwakani 2022 kwa ajili ya kutoa msaada muhimu.

Ombi hilo linafuatia kile kilichoelezwa kuwa hali mbaya duniani inayosababishwa na mabadiliko ya tabianchi, mizozo, na janga la COVID-19 ambavyo vimechochea watu kuyahama makazi yao na kwamba wanawake na wasichana wamekuwa ndio waathirika wakubwa. 

UNFPA imesema unyanyasaji wa kijinsia, kutopatikana kwa huduma za afya, na kuongezeka kwa mahitaji ya msaada wa afya ya akili kunatishia maisha na kunahitaji mwitikio wa kimataifa. 

Msisitizo wa ombi hilo ni kujikita katika maandalizi, hatua za mapema na hatua za kuokoa maisha ya wanawake na wasichana pamoja na vijana katika dharura mbalimbali, kudumisha utu na haki za binadamu ili kuleta matumaini ya mustakabali bora. 

 Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa UNFPA, Diene Keita (kushoto), akizungumza na mama mwenye mtoto mchanga.
UNFPA/Samuel Lamery
Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa UNFPA, Diene Keita (kushoto), akizungumza na mama mwenye mtoto mchanga.

Huduma zinakazopewa kipaumbele 

Usaidizi wa kibinadamu wa UNFPA kwa nchi unalenga katika kuimarisha uwezo na mifumo ya utoaji wa huduma muhimu, za kuokoa maisha za ngono na afya ya uzazi na unyanyasaji wa kijinsia, ikiwa ni pamoja na afya ya akili na usaidizi wa kisaikolojia.  

“Tumedhamiria kujitolea kufanya kazi kwa karibu na kuwasikiliza wanawake na wasichana na vijana wakati msaada unatolewa.” Limesema shirika hilo la Umoja wa Mataifa. 

Licha ya changamoto zinazoletwa na janga la COVID-19, mwaka 2021 UNFPA na washirika wake waliwafikia zaidi ya wanawake milioni 29 walio katika umri wa uzazi kwa kuwafikishia huduma za afya ya ngono na uzazi, na takriban watu milioni 2.4 kwa huduma za kukabiliana na athari za ukatili wa kijinsia, ikiwa ni pamoja na kupitia nyumba salama 12,000 zinazoungwa mkono na UNFPA. 

UNFPA imesema Afghanistan, Ethiopia na majanga mengine ya kibinadamu yamekuwa ni ukumbusho kamili wa jinsi mafanikio yaliyopatikana kwa bidii kwa wanawake na wasichana yanaweza kusambaratishwa wakati wa shida.  

Shirika hilo limeongeza kuwa kadiri mahitaji yanavyoongezeka, kuna haja ya kufanya juhudi zaidi na kufanya vyema zaidi ili kuhakikisha kwamba haki, majukumu na uharaka wa wanawake na wasichana katika mazingira ya kibinadamu na hali tete yako katika kipaumbele na ni kitovu cha hatua zetu za kibinadamu.