Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNFPA yahitaji haraka dola milioni 29.2 kuokoa na kulinda maisha ya wanawake na wasichana Afghanistan

Mwanafunzi wa ukunga mjini Kandahar, Afghanistan akitoa huduma chini ya matubabu chini ya uangalizi
© UNFPA Afghanistan
Mwanafunzi wa ukunga mjini Kandahar, Afghanistan akitoa huduma chini ya matubabu chini ya uangalizi

UNFPA yahitaji haraka dola milioni 29.2 kuokoa na kulinda maisha ya wanawake na wasichana Afghanistan

Msaada wa Kibinadamu

Shirika la Umoja wa Mataifa linalohusika na idadi ya watu na afya ya uzazi duniani UNFPA, leo limetoa ombi la ufadhili ili kukidhi mahitaji ya haraka ya wanawake na wasichana nchini Afghanistan wakati janga la kibinadamu likinyemelea nchini humo. 

Ombi hilo la dola milioni 29.2 ni kwa ajili ya kushughulikia mahitaji ya afya ya uzazi na ulinzi unaohitajika kwa wanawake na wasichana milioni 1.6 walio hatarinini nchini humo. 

Shirika hilo linasema kwa zaidi ya miaka 20 limekuwa likitoa huduma za afya ya uzazi na ulinzi nchini Afghanistan kupitia vituo 200 vya ulinzi na afya ya familia. Ombi la leo la ufadhili ni sehemu ya ombi la jumla la Umoja wa Mataifa la dola milioni 606 kwa ajili ya msaada wa kibinadamu Afghanistan hadi mwisho wa mwaka huu. 

Machafuko ya kisiasa na hali tete inayoendelea nchini Afghanistan, pamoja na kusimamishwa kwa ufadhili kutoka kwa wafadhili wa kimataifa tayari vimekuwa na athari mbaya  na ya kutishia maisha kwa wanawake na wasichana wengi kwani upatikanaji wa huduma ya afya ya kuokoa maisha umevurugika na kupunguzwa zaidi kwa huduma hizo, ikiwa ni pamoja na msaada wa elimu na utoaji wa huduma za kimsingi za afya na kijamii, kutakuwa na athari mbaya, na hatari kwamba nchi inaweza kuingia katika janga la kibinadamu kwa muda mrefu. 

Kuna hitaji la haraka na kubwa kwa jamii ya kimataifa kujitokeza na kuchukua hatua dhidi ya mgogoro wa kibinadamu unaoendelea nchini Afghanistan kwa kiwango kikubwa ili, kuokoa maisha, kuzuia mateso zaidi na kuchagiza matumaini ya maisha bora ya baadaye. 

Kwa mujibu wa shirika hilo fedha za nyongeza zitaturuhusu kuongeza idadi ya vituo vya huduma, kupanua kiwango cha huduma zinazotolewa na kufikia mamia ya maelfu ya wanawake na wasichana kwa vifaa vya kuokoa maisha na afya. 

Akisisitiza umuhimu wa kusaidia sasa mkurugenzi mtendaji wa UNFPA Dkt. Natalia Kanem amesema "Hivi sasa, kipaumbele chetu ni afya na ulinzi kwa karibu wanawake na wasichana milioni 4 ambao wanahitaji msaada wa haraka wa kibinadamu. Lazima tusimame imara na kusimama pamoja kuokoa maisha na kulinda haki za msingi na uhuru wa wanawake na wasichana, pamoja na haki yao ya kushiriki kikamilifu katika nyanja zote za jamii. ” 

Ameongeza kuwa kufuatia kusimamishwa kwa ufadhili wa Benki ya Dunia, pamoja na mradi wa Sehatmandi (wa kutoa huduma za msingi na za muhimu za afya), mfumo wa afya unaelekea kusambaratika.  

Wakati huo huo mahitaji yanaongezeka na wanawake na wasichana watakufa bila kupatikana kwa msaada wa haraka.  

“Makadirio yetu ya awali yanaonyesha kwamba hii inaweza kusababisha vifo vya wajawazito 51,000, mimba zisizotarajiwa milioni 4.8 na kuongezeka mara mbili kwa hitaji lisilotekelezwa la uzazi wa mpango kati ya sasa na mwaka 2025. Suluhisho la kuendelea kufadhili mfumo wa afya ni muhimu” Limesisitiza shirika hilo la UNFPA.