Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Miaka 12 ya vita imetuacha taaban tukipoteza matumaini: Raia Aleppo Syria

Takribani watu 200,000 ni wakimbizi wa ndani huko Idlib nchini Syria kutokana na mapigano  yanayoendelea kwenye eneo hilo
@WFP Syria
Takribani watu 200,000 ni wakimbizi wa ndani huko Idlib nchini Syria kutokana na mapigano yanayoendelea kwenye eneo hilo

Miaka 12 ya vita imetuacha taaban tukipoteza matumaini: Raia Aleppo Syria

Amani na Usalama

Leo ni miaka 12 kamili tangu machafuko yalipozuka Syria na kusababisha vita inayoendelea tangu mwaka 2011 iliyosambaratisha nchi hiyo na mamilioni ya raia wake. Maelfu wamepoteza maisha, mamilioni wamekuwa wakimbizi ndani na nje ya nchi yao na majanga mengine ya kila uchao yanazidi kuwaondolea matumaini raia wa taifa hilo la Mashariki ya Kati.

Adhana hiyo inaashiria ni siku nyingine isiyo na nuru bali iliyoghubikwa na machungu na kupoteza matumaini kwa wakaazi wa Aleppo ambayo ilikuwa mstari wa mbele wa vita, majengo yamesalia magofu ingawa bado kuna watu wanaoishi katika magofu haya.

Watu wengi waliosalia hapa ni wale waliotawanywa na vita inayoendelea kwa mwaka wa 12 sasa akiwemo Sabaha mkimbizi wa ndani aliyepoteza matumaini ya mustakbali bora akisema “Vita ilikuwa ngumu, tumepitia kila zahma kama njaa na mashambulizi ya mabomu. Mume wangu na kaka yangu waliuawa lakini hata wakati huo Maisha yalikuwa kidogo rahisi kuliko sasa”.

Mgao wa chakula wa kila mwezi ukisambazwa kwa familia zilizokimbia makazi yao katika eneo la Sukari huko Aleppo, Syria.
© WFP/Hussam Al Saleh
Mgao wa chakula wa kila mwezi ukisambazwa kwa familia zilizokimbia makazi yao katika eneo la Sukari huko Aleppo, Syria.

Kweli yumkini hali si hali, kwa mujibu wa shirika la Umoja wa Mataifa la mpango wa chakula duniani nusu ya watu wa silia wanakabiliwa na njaa na wanaishi kwa kutegemea msaada wa wahisani likiwemo shirika hilo wengi wakiishi katika maeneo ya wazi na katika shule. Kenn Crossely ni mkurugenzi wa WFP nchini Syria na anasema, 

"Kuna vitongoji Aleppo ambavyo vimesambaratishwa kabisa na kusalia kuwa vifusi. Maisha yao yote yenye tija, majengo, makazi yao, na maeneo ambayo watu walikuwa wakiishi havipo tena. Kisha tetemeko la ardhi likaja, na watu kutoka huko walilazimika kuhama tena, ilibidi wahamie kwenye mashule, wengine wahamie misikitini. Kulikuwa na jumuiya yenye nguvu ya kiraia, washirika wanaoshirikiana nao, NGO’s zinazofanya kazi ya kuwapa chakula cha moto na makazi, lakini kwa hakika watu wanachokitaka ni maisha yenye tija ,watu waweze kujikimu tene, lakini kila siku wamekuwa wakitegemea kwa kiasi kikubwa misaada ya kibinadamu.”

Mdororo wa kiuchumi, ukosefu wa ajira na mfumuko wa bei vimekuwa ni kuongeza chumvi juu ya kidonda kwa wakimbizi hawa wa ndani kama Nawal Shaban “ Hatuwezi kununua chakula cha kutosha kwa watoto wetu vyakula vingi bei haishikiki kama vile nyama na kuku na umeme gharama imekuwa juu pia.”

Hata hivyo kuna wale ambao bado wana imani ya nuru kurejea siku moja kama muna ambaye pia ni mkimbizi wa ndani Aleppo “Sasa kilichosalia ni matumaini kwamba vita hii, mgogoro huu ipo siku utakwimu. Nina matumaini makubwa kwamba watoto wangu wataendelea na elimu yao Mungua akipenda."