Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

WHO  yachapisha mwongozo wa tiba dhidi ya madhara yatokanayo na FGM

Wanawake kutoka kabila la wasamburu nchini Kenya
UNICEF/Samuel Leadismo
Wanawake kutoka kabila la wasamburu nchini Kenya

WHO  yachapisha mwongozo wa tiba dhidi ya madhara yatokanayo na FGM

Afya

Shirika la afya ulimwenguni, WHO limechapisha mwongozo wa kutibu wanawake na wasichana waliokumbwa na ukeketaji, FGM.

WHO inasema sambamba na mwongozo huo, kuna kijitabu cha kusaidia wahudumu wa afya na wakunga kushughulikia matatizo yatokanayo na FGM pamoja na madhara yake ikiwemo kutoka haja ndogo mfululizo na matatizo wakati kujifungua, na vyote vinapatikana kwenye wavuti wa shirika hilo.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Geneva, Uswisi hii leo, msemaji wa WHO, Tarik Jasarevic amesema FGM ni tatizo la dunia lakini limejikita zaidi Afrika, Mashariki ya Kati na Asia, likiwa limekumba zaidi ya wanawake na wasichana zaidi ya milioni 200.

“Ni muhimu sana wahudumu wa afya popote walipo waweze kutambua FGM na kuwatibu wanawke na wasichana kwa uhakika,” akiongeza kuwa ndio msingi wa kitabu  hicho cha mwongozo wa utabibu na kingine ambacho kinasaidia kuwahudumia wanawake na watoto waliokumbwa na FGM sambamba.

Mambo muhimu kuhusu FGM

  • Kati ya idadi hiyo, watoto wa kike wenye umri wa miaka 14 na chini ya hapo ni milioni 44, na idadi kubwa wanatoka Mali, asilimia 73, Gambia, asilimia 56, Mauritania, asilimia 54 na Indonesia asilimia 49.
  • Nchi zinazoongoza duniani kwa ukeketaji wa wanawake na wasichana wenye umri wa kuanzia miaka 15 hadi 49 ni Somalia, asilimia 98, Guinea asilimia 97, Djibouti asilimia 93 na Misri asilimia 87.
  • FGM hufanyiwa watoto katika umri wa tangu kuzaliwa hadi umri wa miaka 15.
  • FGM husababisha kutokwa kwa damu mfululizo, na matatizo ya kiafya ni pamoja na maambukizi, utasa na matatizo wakati wa kujifungua na pia huhatarisha maisha ya mtoto anayezaliwa.
  • FGM hukiuka haki za binadamu za wasichana na wanawake.
  • Lengo namba 5 la malengo ya maendeleo endelevu, SDG kuhusu usawa wa kijinsia, lengo dogo namba 5.3 linataka kutokomezwa kwa mila zote potofu kama vile ndoa za mapema, ndoa za lazima na ukeketaji au FGM..
  • Wito wa kutokomeza FGM umekuwa unatolewa na makundi mbalimbali ya nchi ikiwemo Muungano wa Afrika Muungano wa Ulaya na Umoja wa nchi za Kiislamu pamoja na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kupitia maazimio yake mbalimbali.