Ukeketaji unaathiri wasichana na wanawake na gharama ya matibabu ni dola bilioni 1.4 kwa mwaka kimataifa-WHO

6 Februari 2020

Wakati dunia ikiadhimisha siku ya kutokomeza ukeketaji, shirika la afya ulimwenguni, WHO limesema kitendo hicho kinadhoofisha uchumi pamoja na nguvu kazi.

WHO imesema sio tu kwamba ukeketaji ni ukiukaji wa haki za binadamu lakini unaathiri afya kimwili na kiakili kwa mamilioni ya wasichana na wanawake na pia kutumia raslimali nyingi muhimu za nchi na kwamba uwekezaji zaidi unahitajika kumaliza ukeketaji na madhila unaosababisha.

Kwa mujibu wa makadirio mapya gharama ya matibabu kutokana na athari za ukeketaji huenda ikafika dola bilioni 1.4 kimataifa kwa mwaka iwapo mahitaji yote ya kiafya yatashughulikiwa. Katika nchi binafsi, gharama hii inakaribia asilimia 10 ya matumizi ya mwaka mzima ya afya kwa wastani ambapo katika baadhi ya nchi idadi hii huenda ikafika asilimia 30.

WHO imesema wanawake na wasichana waathirika wa ukeketaji wanakabiliwa na hatari kubwa katika afya yao na uzima, hii ni pamoja na athari pindi tu baada ya kukeketwa ikiwemo: maambukizi, kuvuja damu nyingi au kiwewe pamoja na magonjwa ya muda mrefu ambayo huenda yakatokea maishani.

Pia wanawake ambao wamekeketwa wana uwezekano mkubwa wa kupata tishio la kupoteza maisha wakati wa kujifungua, kukabiliwa na magonjwa ya akili na maambukizi ya muda mrefu.

Pia huenda wakahisi uchungu wakati wa hedhi, wakienda haja ndogo au wakati wa kitendo cha kujamiana. Abida Dawud ni mmoja wa waathirika wa ukeketaji akiwa eneo la Afar nchini Ethiopia, “Mimi ni manusura wa ukeketaji, niña watoto wane, wavulana wawili na wasichana wawili, kazi yangu kubwa ni kutoa mafunzo kuhusu madhara ya ukeketaji. Tunawaambia akina mama na wasichana kwamba ukeketaji una madhara kwa wasichana wetu na kwetu sisi , huenda sehemu ya mwili wangu ilichukuliwa lakini siwezi kamwe kutoa moyo wangu. Ndani ya moyo wangu ninawaza ni jinsi gani tunaweza kutomeza ukeketaji.”

Kwa upande wake manusura mwingine wa ukeketaji Khadija Mohammed kutoka eneo hilo la Afar pia amesema,“Iwe ni kwa kutangaza kwenye radio au televisheni au kuzungumzwa na watu wa Afar, ujumbe ni kutokomeza ukeketaji, iwapo hatutatokomeza kitendo hicho basi vizazi vijavyo vitaendeleza ukeketaji. Ni lazima tuusitishe hapa.”

Kwa kutumia takwimu za nchi 27 zilizo na visa vingi vya ukeketaji, makadirio ya kiuchumi yanaonesha faida za wazi za kiuchumi kufuatia kutokomeza ukeketaji. Iwapo kitendo hicho kitatokomezwa zaidi ya asilimia 60 kutokana na gharama za kiafya zingeweza kuokolewa.

Tangu mwaka 1997 hatua zimepigwa katika kutokomeza ukeketaji kupitia kazi ndani ya jamii, utafiti na marekebisho katika sheria na será. Nchi 26 barani Afrika na Mashariki ya kati zimeweka sheria ya wazi dhidi ya ukeketaji, pamoja na nchi 33 zilizo na wahamiaji kutoka nchi kunakofanyika vitendo vya ukeketaji.

Ukeketaji unatambulika kama ukiukaji wa haki za binadamu na hauna faida zozote za kiafya na unasababisha madahra. WHO inashikilia msimamo wake kwamba ukeketaji haupaswi kutekelezwa wakati wowote.

Ukeketaji ni ishara ya ukosefu wa usawa wa kijinsia-UN

Zaidi ya wasichana na wanawake milioni 200 duniani leo ni amnusura wa ukeketaji ambao una madhara ikiwemo athari za kiafya. Mwaka huu takriban wasichana milioni 4 wako hatarini kukeketwa.

Hayo yamesemwa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres katika ujumbe wake wa kuadhimisha siku ya kupinga ukeketaji akiongeza kwamba, “ukeketaji ni ishara tosha ya ukosefu wa usawa wa kijinsi uliokota mizizi katika mifumo ya kijamii, kiuchumi na kisiasa. Aidha ni ukiukaji wa haki za binadamu na ukatili mkubwa dhidi ya wanawake. Kwa bahati nzuri kuenea kwa visa hivi kumepungua kwa aslimia 25.”

Hatahivyo amesema, hata kisa kimoja cha ukeketaji hakifai na kwamba, “siku ya leo ya kupinga ukeketaji inaangazia umuhimu wa vijana kupaza sauti zao. Ni lazima tuimarishe sauti hizo na tuwasaidie kuchagiza kuleta mabadiliko na kwa ajili ya haki zao.”

Bwana Guterres amesema, “kwa pamoja tunaweza kuutokmeza ukeketaji kufikika mwaka 2030. Kwa kufanya hivyo kutakuwa na matokeo chanya ya muda mrefu kiafya, kielimu na kiuchumi kwa ajili ya wasichana na wanawake.”

Katibu Mkuu amehitimisha ujumbe wake kwa kusema, “wakati Umoja wa Mataifa ukianza muongo wahatua kufikia malengo ya maendeleo endelevu hebu na tufanya muongo huu uwe wa visa sufuri vya ukeketaji.”

Visa vya ukeketaji na wahudumu wa afya vimeongezeka

Takriban msichana mmoja au mwanamke kati ya wanne wamekeketwa au manusura milioni 52 kote duniani walikeketwa na mtaalam wa kiafya kwa mujibu wa utafiri wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF

Kwa mujibu wa UNICEF idadi hii ni maradufu miongoni mwa barubaru ambao asilimia 34 ya manusura wa ukeketaji walio kati ya umri wa miaka 15-19 walifanyiwa kitendo hicho katika kituo cha afya ikilinganishwa na asilimia 16 ya manusura walio katika ya umri wa miaka 45-49 huu ikiashiria ongezeko la visa hivyo katika vituo vya afya.

 Mkurugenzi Mkuu wa UNICEF, Henrietta Fore amesema, “ukeketaji uliotekelezwa na daktari bado ni ukeketaji. Wataalamu wa kiafya wanaotekeleza kitendo hicho bado wanakiuka haki za msingi, afya ya kimwili na kiujumla.”

 Ongezeko la visa vya ukeketaji katika vituo vya afya ni kufuatia dhana potofu kwamba hatari za ukeketaji zinatokana na suala la kiafya na wala sio ukatili wa haki za  wasichana.

Hatari ya ukeketaji katika vituo vya afya imeangaziwa kufuatia kifo cha msichana wa umri wa miaka 12 nchini Misri mwezi jana na kuzua vyombo yv akiamtaifa ikiwemo Umoja wa Mataifa kulaani vikali kitendo hicho. Misri ilitokomeza ukeketaji mwaka 2008 na kuongeza adhabu dhidi yake mwaka 2016.

Bi. Fore amesema, “ukeketaji umekita mizizi katika ukosefu wa usawa na hatua ya kwanza katika kuutomeza ni kubadili mtizamo wa watu.” Ameongeza kwamba, “tunapiga hatua. Mitizamo inabadilika. Tabia zinabadilika na kwa ujumla wasichana wachache wanakeketwa.”

 

 

♦ Kutembelea ukurasa maalum wa COP26 bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter