Vifo vitokanavyo na COVID-19 vyaongezeka duniani, China yaongoza

Shirika la Umoja wa Mataifa la afya ulimwenguni, WHO limesema idadi ya vifo kutokana na COVID-19 imeanza kuongezeka duniani tangu mwishoni mwa mwezi uliopita wa Desemba.
Mkurugenzi Mkuu wa WHO, Dkt. Tedros Ghebreyesus amesema hayo leo wakati akifungua kikao cha kamati Kamati ya kimataifa ya WHO , kuhusu dharura za magonjwa ambacho kimekutana leo kwa mara ya 14 kutathmini iwapo bado COVID-19 ni dharura ya afya ya umma au la, wakati huu ambapo wiki ijayo itakuwa gonjwa hilo linaingia mwaka wa nne.
Amesema kuondolewa kwa vizuizi nchini China kumesababisha ongezeko la vifo kwenye taifa hilo lenye idadi kubwa zaidi ya watu duniani.
“Wiki iliyopita, vifo takribani 40,000 vya COVID-19 viliripotiwa WHO na zaidi ya nusu ni kutoka China,” amesema Dkt. Tedros.
Amesema leo wataongeza taarifa mpya kwenye dashibodi ya COVID-19 ili kujumuisha wagonjwa wapya na vifo vilivyoripotiwa China katika wiki za karibuni.
Kwa ujumla amesema katika wiki nane zilizopita, zaidi ya watu 170,000 walikufa kwa COVID-19 duniani kote na idadi halisi inaweza kuwa kubwa.
Mkuu huyo wa WHO amesema chanjo, tiba na uchunguzi dhidi ya COVID-19 vimesalia hatua muhimu katika kuzuia ugonjwa huo na kuokoa maisha ya watu, sambamba na kuepusha shinikizo zaidi kwenye mifumo ya afya na wahudumu wa afya.
“Hata hivyo hatua za kimataifa bado zinasuasua kwa sababu katika nchi nyingi, hatua hizo muhimu za kuokoa maisha bado hazijafikia wale wanaohitaji zaidi, mathalani wazee na wahudumu wa afya,” amesema Dkt. Tedros.
Amefafanua kwa mifumo mingi ya faya duniani kote bado inahaha kukabiliana na COVID-19, kando ya kuhudumia wagonjwa wenye matatizo mengien kama vile homa ya mafua makali, wakati huu ambapo kuna uhaba wa watumishi na hata walioko wamechoka.
Dkt. Tedros ametaja changamoto nyingine kuwa ni ufuatiliaji nao umezorota huku imáni ya wananchi kwa mbinu za kinga kama vile chanjo inaendelea kutikiswa na msururu wa taarifa potofu na za uongo.
Jumatatu ambayo ni tarehe 30 mwezi Januari, itakuwa ni miaka mitatu tangu COVID-19 itangazwe kuwa dharura ya afya ya umma duniani na hivyo kikao cha leo kitamshauri Dkt. Tedros iwapo dharura hiyo iendelee au la.