Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tumewataka watalibani waondoe vikwazo vyote dhidi ya wanawake na wasichana Afghanistan- UN

Wanawake wakitembea katika mtaa wa Jalalabad Afghanistan. (Maktaba)
UN Photo/Fardin Waezi
Wanawake wakitembea katika mtaa wa Jalalabad Afghanistan. (Maktaba)

Tumewataka watalibani waondoe vikwazo vyote dhidi ya wanawake na wasichana Afghanistan- UN

Wanawake

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Amina J. Mohammed ambaye ameongoza ujumbe wa viongozi waandamizi wa Umoja wa Mataifa huko Afghanistan wametamatisha ziara yao ya siku nne iliyolenga kutathmini hali ilivyo, kuzungumza na uongozi ulioshikilia mamlaka na kusisitiza mshikamano na wananchi wa taifa hilo la Asia.

Viongozi wengine waandamamizi waliokuwemo kwenye ziara hiyo kwa niaba ya Katibu Mkuu wa UN ni Mkurugenzi Mtendaji wa shirika la Umoja wa Mataifa la masuala ya wanawake, UN Women, Sima Bahous na Naibu Mkuu wa Idara ya Siasa ya UN Khaled Khiari. 

Katika mikutano na viongozi watalibani kwenye mji mkuu Kabul na jimboni Kandahar, ujumbe huo umewasilisha moja kwa moja hofu kuhusu amri ya hivi karibuni ya kuzuia wanawake kufanya kazi kwenye mashirika ya kitaifa na kimataifa, hatua ambayo inadumaza kazi ya mashirika mengi yanayosaidia mamilioni ya wananchi wa Afghanistan. 

Hivi karibuni pia mamlaka hizo zimechukua hatua ya kuzuia wanawake nchini kote kujiunga na Vyuo Vikuu hadi itakapotangazwa ten ana tayari wamezuia watoto wa kike kujiunga na elimu ya sekondari, bila kusahau vizuizi kwa wanawake na wasichana kutembea kwa uhuru na katika maeneo mengi ya ajira wanawake hawaruhusiwi kufanya kazi.  

Wanawake pia wamezuiwa kwenda kwenye bustani za mapumziko, maeneo ya mazoezi na mabafu ya umma. 

Vikwazo vyote dhidi ya wanawake na wasichana viondolewe 

 “Ujumbe wangu uko wazi na dhahiri: Pamoja na kutambua hatua muhimu za kutoweka vikwazo maeneo mengine, vikwazo vilivyopo vinawaweka wanawake na wasichana wa Afghanistan katika mustakabali unaowabana majumbani tu, hivyo kukiuka haki zao na kunyima jamii huduma zitolewazo na wanawake,” amesema Bi. Mohammed. 

Ameongeza kuwa matamanio yao ya pamoja ni kwa Afghanistan yenye ustawi ndani yake na majirani zake, na kwenye mwelekeo wa maendeleo endelevu. “Lakini kwa sasa, Afghanistan inajitenga, katikati ya janga la kibinadamu na moja ya mataifa yaliyo hatarini zaidi kutokana na kuathiriwa na mabadiliko ya tabianchi. Lazima tufanye linalowezekana kuziba pengo hilo.” 

Wakati wa ziara hiyo, Naibu Katibu Mkuu wa UN na Mkuu wa UN Women walikuwa na mazungumzo na wanajamii, watumishi wa kiutu, mashirika ya kiraia na sekta nyingine muhimu kwenye mji mkuu Kabul, majimbo ya Kandahar na Herat. 

“Tumeshuhudia mnepo wa kipekee. Wanawake wa Afghanistan wametuacha pasi shaka yoyote kuhusu ujasiri wao na kukataa kufutwa kwenye maisha ya umma. Wataendelea kuchechemua na kupambania haki zao, na tumejiandaa kuwasaidia kufanikisha hilo,” amesema Bi. Bahous. 

Amekumbusha kuwa kinachoendelea Afghanistan ni janga kubwa la haki za wanawake na kengele ya hadhari kwa jamii ya kimataifa. 

“Inaonesha ni kwa kasi gani maendeleo ya haki za wanawake yaliyopatikana kwa miongo yanaweza kufutwa ndani ya siku chache. Ni jukumu la UN Women kusimama kidete kwa niaba ya wanawake wa Afghanistan na wasichana na kuendelea kupaza sauti zao ili waweze kurejeshewa haki zao zao.” 

UN na wadau wanashikamana na raia wa Afghanistan 

Naibu Msemaji wa Umoja wa Mataifa amesema Umoja huo na wadau wake yakiwemo mashirika ya kitaifa na kimataifa, wanasaidia wananchi milioni 25 wa Afghanistan ambao tegemeo lao ni msaada wa kibinadamu ili waweze kuishi na kwamba watasalia na kuendelea kutoa misaada nchini humo. 

Zuio la hivi karibuni la mamlaka ya Afghanistan kwa wanawake kutofanya kazi kwenye mashirika ya kiraia, limelazimu wadau wengi kusitisha operesheni zao ambazo haziwezi kuendelea kufanyika kwa usalama. 

Ziara nchini Afghanisan inafuatia mfululizo wa mashauriano ya ngazi ya juu kuhusu Afghansitan huko ghuba na Asia. 

Ujumbe huo pia ulikuwa na vikao na uongozi wa shirika la ushirikiano wa nchi za kiislamu, IOC, Benki ya Maendeleo ya kiislamku, makundi ya wanawake wa kiafganistan huko Ankara Uturuki halikadhalika mabalozi na wajumbe maalum wa Afghanistan walioko Doha, Qatar. 

Walikutana kujadili kuchechemua dhima muhimu na ushiriki wa wanawake na imependekezwa na kukubalika kimsingi kuwa na kukubaliwa kuwa mkutano wa kimataifa kuhusu wanawake na wasichana katika nchi za kiislamu ufanyike mwezi Machi mwaka huu wa 2023.