Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mapigano yanazidi kusigina ajenda ya wanawake, amani na usalama

Naibu Katibu Mkuu wa UN Amina J. Mohammed akihutubia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuhusu ajenda ya Wanawake, Amani na Usalama 20-10-2022
UN Photo
Naibu Katibu Mkuu wa UN Amina J. Mohammed akihutubia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuhusu ajenda ya Wanawake, Amani na Usalama 20-10-2022

Mapigano yanazidi kusigina ajenda ya wanawake, amani na usalama

Amani na Usalama

Mapigano yakiwa  yanaendelea na kurudisha nyuma maendeleo ya haki za wanawake na wasichana duniani, ajenda ya wanawake, amani na usalama bado sana kufanikiwa hivi sasa kuliko wakati wowote ule, imesema ripoti mpya ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa iliyotolewa leo wakati ambapo Baraza la Usalama la chombo hicho pia limekutana jijini New York, Marekani katika mjadala wa wazi wa mwaka kuhusu Wanawake,Amani na Usalama: Kuimarisha mnepo na uongozi wa wanawake katika njia ya amani iliyogubikwa na vikundi vilivyojihami.

Ripoti inaweka bayana kuwa kuzorota kwa amani na usalama duniani kunasababisha machungu makubwa na kuna madhara mahsusi kwa wanawake na wasichana katika nchi hizo zenye vita na mizozo.

Wanawake wanakumbwa na vizuizi vya kupata sauti

Katika nchi nyingi, kwa mujibu wa ripoti hiyo, vikundi vyenye misimamo mikali vimetwaa mamlaka kinguvu na kufuta ahadi za usawa wa kijinsia na sasa wanawake wanaopaza sauti zao wanakumbwa na mateso.

Imetolea mfano ambako hali ni mbayá zaidi kuwa ni Afghanistan ambako watalibani wamefunga shule za sekondari za wasichana, wamezuia wanawake kutoonesha nyuso zao maeneo ya umma na kuzuia haki yao ya kuondoka majumbani mwao na sasa ripoti inataka hatua zichukuliwe kusaidia wanawake kuwa sehemu ya mabadiliko.

Akihutubia Baraza la Usalama, Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Amina J. Mohammed amesema tafiti mbalimbali zimedhihirisha kuwa mnepo na uongozi wa wanawake unapoimarishwa, kila mtu ananufaika wakiwemo wanaume na wavulana.

“Wanawake wana nafasi kubwa zaidi ya kuchochea uongozi jumuishi na utangamano wa kijamii; watajenga amani na kukomesha mapigano; watawekeza katika maendeleo endelevu- msingi wa jamii zenye amani, ustawi na endelevu,” amesema Bi. Mohammed.

Amesisitiza kuwa ushiriki wa wanawake katika ngazi mbalimbali, kuanzia jamii hadi kwenye mabunge umekuwa msingi muhimu katika kubadili mtazamo wa kushughulikia amani na usalama katika kipindi cha miaka 20 iliyopita.

Mtoto wa kike mwenye umri wa miaka 13 akijisomea nyumbani kwenye mji mkuu wa Afghanistan, Kabul baada ya serikali ya Taliban kutangaza kuwa shule hazitafunguliwa kwa ajili ya watoto wa kike wa darasa la 7 hadi 12.
© UNICE/Mohammad Haya Burhan
Mtoto wa kike mwenye umri wa miaka 13 akijisomea nyumbani kwenye mji mkuu wa Afghanistan, Kabul baada ya serikali ya Taliban kutangaza kuwa shule hazitafunguliwa kwa ajili ya watoto wa kike wa darasa la 7 hadi 12.

Mikataba 7 kati ya 10 haijumuishi kabisa wanawake

“Hata hivyo kasi ni ndogo,” amesema Naibu Katibu Mkuu akitolea mfano kuwa kati ya mwaka 1995 hadi 2019, kiwango cha mikataba yenye vipengele vya usawa wa jinsia imeongezeka kutoka asilimia 14 hadi 22. Mikataba minne kati ya mitano inapuunza usawa wa jinsia. Na katika ngazi za maamuzi bado kuna mparaganyiko. Na wakati huo huo, wanawake walikuwa wastani wa asilimia 13 ya wasuluhishi, asilimia 6 ya wapatanishi na asilimia 6 ya watia saini kwenye michakato ya amani.

Akifafanua zaidi amesema katika kila michakato 10 ya amani, 7 haikujumuisha kabisa wanawake kama wapatanishi au watiaji saini.

Bi. Mohammed amesema ni lazima kubadili mwelekeo na kuchukua hatua kadhaa kujumuisha wanawake kwenye michakato ya amani na kuhakikisha kuna fungu la kuwawezesha kushiriki.

Mfuko wa wanawake unasaidia watetezi wa haki

“Mfuko wa wanawake kuhusu amani na Usaidizi wa kiutu ambao tayari umesaidia zaidi ya mashirika ya kijamii 600 ya wanawake kwenye mizozo, umefungua dirisha la kusaidia wanawake wanaharakati walio hatarini,” amesema Bi. Mohammed.

Mouna Awata (kushoto) Rais wa kikundi cha wanawake kiitwacho Nyumba ya Amani ambayo hujadiliana na vikundi vilivyojihami ili kuleta amani huko Gao nchin Mali.
Kani Sissoko
Mouna Awata (kushoto) Rais wa kikundi cha wanawake kiitwacho Nyumba ya Amani ambayo hujadiliana na vikundi vilivyojihami ili kuleta amani huko Gao nchin Mali.

Amesema pamoja na hayo wanasaidia pia harakati za kuhakikisha kuna uwakilishi zaidi wa wanawake kwenye taasisi, akitolea mfano Jamhuri ya Afrika ya Kati, CAR, ambako mwanamke mmoja mgombea wa kiti cha ubunge “alitujulisha kuwa anakumbwa na vitoisho. Walinda amani walifika haraka na watu waliokuwa wamejihami walikimbia. Leo hii mgombea huyo sasa ni mbunge.”

Naye Mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa la masuala ya wanawake, UN-Women Sima Bahous alihutubia wajumbe na pia alinukuliwa katika ripoti ya Katibu Mkuu.

“Hakuna jaribio kubwa la ahadi yetu kwa amani kuliko kiwango ambacho tunahakikisha wanawake ndio kitovu cha kile tunachotafuta,” amesema Bi. Bahous.

Ripoti inasema kufungua milango kwa ajili ya ushiriki na ujumuishi wa wanawake katika masuala yote ya amani, kunatoa njia ya kupata amani endelevu na kuzuia mizozo.

Soma ripoti kamili hapa