Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Watalibani wanazidi kukandamiza raia kinyume na madai yao - Wataalam UN

Kundi la wanawake na watoto wao wakitembea Daikundi katika eneo la mbali la katikati mwa Afghanistan.
© UNICEF/Mark Naftalin
Kundi la wanawake na watoto wao wakitembea Daikundi katika eneo la mbali la katikati mwa Afghanistan.

Watalibani wanazidi kukandamiza raia kinyume na madai yao - Wataalam UN

Haki za binadamu

Wataalamu wa Umoja wa Mataifa kuhusu haki za binadamu wamekosoa wazo la kila uchao la uongozi wa Talibani nchini Afghanistan la kudai kuwa linafanyia marekebisho sera zake huku wakisema mamlaka hiyo iliyojitwalia madaraka miaka miwili iliyopita inatekeleza mifumo ya ubaguzi, uenguaji na ukandamizaji wa wanawake na wasichana. 

Kupitia taarifa yao waliyoitoa leo huko Geneva, Uswisi, wataalamu hao wamesema miaka miwili iliyopita watalibani walitwaa madaraka Afghanistan na tangu wakati huo sera walizowekea wananchi wa taifa hilo zimesababisha mwendelezo, mfumo na ufutaji wa haki kadhaa za kibinadamu, ikiwemo haki ya elimu, ajira, uhuru wa kujieleza na kukusanyika.

Wamesema ripoti za uhakika na za mara kwa mara kuhusu watu kuuawa kiholela, kutoweshwa, kuteswa na kufurushwa makwao vimezidi kuongeza wasiwasi nchini Afghanistan, huku waathirika zaidi wakiwa wanawake, wasichana, makabila madogo, watu wenye ulemavu, watetezi wa haki , waandishi wa habari, walimu na viongozi wa serikali ya zamani.

Wataalamu hao wamesema licha ya hakikisho la mamlaka hizo zilizojiweka madarakani ya kwamba vizuizi vyovyote hasa vile vya kupata elimu vitakuwa vya muda, hali halisi ni tofauti kwani kuna mifumo imewekwa ya ubaguzi, kuengua wengine na kutesa watu.

Wamesema wakilinganisha na mwaka jana, watalibani kwa mwaka wa pili wameimarisha mfumo wa ubaguzi kwa lengo la kuwadhibiti zaidi wanawake na wasichana. Mwezi Aprili mwaka  huu wanawake walizuiwa kufanya kazi na kuna ripoti kuwa katika baadhi ya majimbo, watalibani wameagiza watoto wa kike wenye umri wa zaidi ya miaka 10 wasiende shuleni.

Wataalamu wametoa ujumbe kwa watalibani wenye vipengele sita; Mosi, kubadili mwelekeo wao dhidi ya wanawake na wasichana ambapo wanawake waruhusiwe kwenda kazini na waendeshe biashara.

Pili; Shule zote zifunguliwe, Tatu; visasi dhidi ya maafisa wa serikali ya zamani vikome, Nne; ukamataji holela wa watu nao ukome, Tano; kuondoa katazo la kubinya fursa za kiraia ikiwemo haki ya kukusanyika na Sita;  kuchukua hatua thabiti kuepusha ubaguzi dhidi ya makabila na madhehebu madogo.