Nishati ya sola yaongeza kasi ya ajira duniani

22 Septemba 2022

Kama bado unapuuza suala la nishati jadidifu ikiwemo ile ya sola, ni wakati wa kuchukua hatua sasa kwani ripoti mpya iliyotolewa leo na shirika la kimataifa la nishati jadidifu, IRENA na lile la Umoja wa Mataifa la kazi duniani, ILO imethibitisha ukuaji wa ajira kwenye sekta ya nishati jadidifu na kutaka mikakati ya kuweka mnyonyoro tulivu wa thamani na ajira zenye hadhi, ikisema mwaka jana idadi ya ajira kwenye sekta hiyo ilifikia milioni 12.7, ikiwa ni ongezeko la ajira mpya 700,000 licha ya janga la COVID-19.

Ripoti hiyo iliyotolewa leo Geneva, Uswisi inasema ajira nyingi ni kwenye nishati ya jua au sola ambapo mwaka 2021 ilitoa ajira milioni 4.3, zaidi ya theluthi moja ya nguvukazi kwenye sekta ya nishati jadidifu duniani kote.

Kilichobainishwa kwenye ripoti ni kwamba ukubwa wa soko la ndani ya nchi ndio kichocheo cha ongezeko la ajira kwenye sekta ya nishati jadidifu, sambamba na gharama mbalimbali ikiwemo ajira.

Soko la ndani ndio jawabu la  ukuaji wa sekta ya nishati jadidifu

Kutokana na ongezeko la wasiwasi kuhusu mabadiliko ya tabianchi, kukwamuka kutoka janga la COVID-19 na kuvurugwa kwa mnyororo wa usambazaji wa bidhaa duniani, nchi zinavutiwa zaidi na kupata bidhaa kutoka ndani ya nchi na kufungua fursa za ajira ndani ya nchi.

Ripoti inaeleza kwa kina ni kwa vipi masoko ya ndani ni msingi wa kuchochea ukuaji wa nishati safi, huku ikiongeza suala hilo pia linategemea kuongeza uwezo wa kuuza nje ya nchi teknolojia za uzalishaji wa nishati hizo.

Francesco La Camera, ambaye ni Mkurugenzi Mkuu wa IRENA amesema, “tunapokabiliwa na changamoto lukuki, ajira kwenye nishati jadidifu zinasalia kuwa na mnepo na zimethibitisha kuwa injini inayoaminika ya kuzalisha ajira. Ushauri wangu kwa serikali duniani kote kufuatilia sera za viwanda ambazo zinahamasisha upanuzi nchini mwao wa ajira katika sekta ya nishati jadidifu.”

Bwana La Camera anasema kuimarisha thamani ya ajira ndani ya nchi siyo tu itajenga fursa za biashara na ajira mpya kwa wa jamii na taifa lakini pia kuimarisha uhakika wa upatikanaji wa nishati salama kwa wote.

Picha hii ya tarehe 18 mwezi Aprili mwaka 2018, inaonesha paneli za sola zinazozalisha umeme wa kusukuma maji katika mtambo uliojengwa na UNICEF huko Yambio , SUdan Kusini.
© UNICEF/Sebastian Rich
Picha hii ya tarehe 18 mwezi Aprili mwaka 2018, inaonesha paneli za sola zinazozalisha umeme wa kusukuma maji katika mtambo uliojengwa na UNICEF huko Yambio , SUdan Kusini.

China ina asilimia 42 ya ajira zote katika nishati jadidifu duniani

ripoti inaeleza takribani theluthi mbili ya ajira za mwaka jana kwenye nishati jadidifu ziko barani Asia. China pekee ina asilimia 42 ya ajira zote ikifuatiwa na nchi za Jumuiya ya Ulaya, EU na Brazil zote zikiwa na asilimia 10. India na Marekani ni asilimia 7 kila moja.

Mkurugenzi Mkuu wa ILO, Guy Ryder anasema, kando ya namba hizo, kuna umakini zaidi unaoongezeka kwenye ubora wa ajira na mazingira ya kazi kwenye nishati jadidifu.

“Ongezeko pia la ajira kwa wanawake linadokeza kuwa kwa kuwekwa kwa sera mahsusi na mafunzo, kunaweza kuongeza ushiriki wa wanawake kwenye ajira za sekta ya nishati jadidifu, ujumuishwaji na hatimaye usawa wa mpito wa nishati salama kwa wote,” amesema Bwana Ryder akitoa wito kwa serikali, wafanyakazi na waajiri kusalia kidete katika kutekeleza suala la mpito endelevu wa nishati ambao amesema ni muhimu kwa kazi za siku zijazo.

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter