Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Theluthi moja ya watu kwenye nchi za Kiarabu wanaishi katika umasikini: ESCWA

© UNICEF/Delil Souleiman
Mtoto akiwa kwenye kambi ya muda huko Ain Issa nchini Syria. (3 Juni 2019)
© UNICEF/Delil Souleiman

Theluthi moja ya watu kwenye nchi za Kiarabu wanaishi katika umasikini: ESCWA

Ukuaji wa Kiuchumi

Kwa mujibu wa utafiti mpya uliotolewa leo na tume ya Umoja wa Mataifa ya kiuchumi na kijamii kwa mataifa ya Asia Magharibi ESCAWA kuhusu maendeleo ya kiuchumi na kijamii kwenye ukanda wa nchi za Kiarabu asilimia kubwa ya watu katika ukanda huo wanaishi chini ya mstari wa umasikini licha ya ukuaji wa uchumi. 

ESCAWA inasema uchumi wa ukanda huo unatarajiwa kukua kwa asilimia 4.5% mwaka 2023 na asilimia 3.4% mwaka 2024 licha ya usumbufu wa kuzorota kwa uchumi wa dunia uliosababishwa na janga la COVID-19 na vita ya Ukraine. 

Kulingana na Utafiti huo viwango vya mfumuko wa bei viliongezeka hadi asilimia 14% mwaka huu wa 2022, lakini kuna uwezekano wa kushuka hadi asilimia 8% na 4.5% katika miaka miwili ijayo, mtawaliwa.  

Pia utafiti umeonyesha kuwa “umaskini, unaopimwa dhidi ya mistari ya umaskini ya kitaifa, uliongezeka na kuathiri watu milioni 130 katika nchi za Kiarabu, yaani, zaidi ya theluthi moja ya wakazi wa eneo hilo ukiondoa nchi za Baraza la ushirikiano la Ghuba na Libya. Utafiti unatarajia kuongezeka zaidi kwa viwango vya umaskini katika miaka miwili ijayo, na kufikia asilimia 36% ya idadi ya watu mwaka 2024.” 

Zaidi ya hayo, eneo la Uarabuni lilisajili kiwango cha juu zaidi cha ukosefu wa ajira ulimwenguni mwaka 2022, kwa asilimia 12%.  

Utafiti unasema huenda kukawa na upungufu mdogo sana mwaka wa 2023 wa hadi asilimia 11.7%, kutokana na juhudi za kurejesha uchumi baada ya janga la COVID-19. 

Kuna tofauti kubwa miongoni mwa nchi 

Kulingana na Ahmed Moummi, mwandishi mkuu wa utafiti huo, licha ya mtazamo chanya wa ukuaji wa uchumi eneo hilo, kuna tofauti kubwa miongoni mwa nchi, ambazo zimechochewa na vita ya Ukraine.  

“Kwa hakika, madhara ya vita hivyo si sawa kwa nchi zote za Kiarabu. Nchi za baraza la ushirikiano la Ghuba na nchi nyingine zinazouza mafuta zitaendelea kunufaika na bei ya juu ya nishati, huku nchi zinazoagiza mafuta zikikabiliwa na changamoto kadhaa za kijamii na kiuchumi, ikiwa ni pamoja na kuongezeka kwa gharama za nishati, uhaba wa chakula, na kushuka kwa utalii na misaada ya kimataifa.” 

Moummi Amesisitiza kuwa "Hali ya sasa inatoa fursa kwa nchi za Kiarabu zinazouza mafuta nje ya nchi kubadilisha uchumi wao mbali na sekta ya nishati kwa kukusanya akiba na kuwekeza katika miradi inayoleta ukuaji jumuishi na maendeleo endelevu". 

Kupitia utafiti wake wa kila mwaka, ESCWA inatoa uchanganuzi wa mielekeo ya karibuni ya kijamii na kiuchumi katika kanda, ili kuunga mkono juhudi za nchi wanachama katika kuandaa na kutekeleza sera zenye msingi wa ushahidi, na kuboresha michakato ya kupanga uchumi ili kufikia maendeleo endelevu na jumuishi.