Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Vita nchini Ukraine vyaweka njiapanda mafanikio ya kujikwamua kiuchumi duniani:UNCTAD

Mavuno ya ngano karibu na kijiji cha Krasne nchini Ukraine.
© FAO/Anatolii Stepanov
Mavuno ya ngano karibu na kijiji cha Krasne nchini Ukraine.

Vita nchini Ukraine vyaweka njiapanda mafanikio ya kujikwamua kiuchumi duniani:UNCTAD

Ukuaji wa Kiuchumi

Vita vinavyoendelea nchini Ukraine vinahatarisha kuvunja kasi ya kufufua uchumi wa ulimwengu navitapunguza ukuaji wa uchumi wa kimataifa kwa takriban asilimia , kulingana na makadirio mapya yaliyotolewa leo mjini Geneva Uswisi na kamati ya Umoja wa Mataifa ya biashara na maendeleo UNCTAD.

Kwa sababu ya vita vya Ukraine na mabadiliko ya sera za uchumi wa nchi katika miezi michache iliyopita, ripoti ya UNCTAD inarekebisha utabiri wake wa ukuaji wa uchumi wa dunia kutoka asilimia 3.6% hadi asilimia 2.6% kwa 2022.

UNCTAD inasema kutokana na hali hizi, mtazamo wa uchumi wa dunia unazidi kuzorota kwa kasi, ukienda sambamba na kupanda kwa bei za vyakula, mafuta na mbolea, kuongezeka kwa hali tete ya kifedha, urekebishaji tata wa mifumo ya ugavi katika masoko ya kimataifa na kupanda kwa gharama za biashara.

Pia ripoti hiyo ya makadirio ya uchumi imeeleza kwamba wakati Urusi itapata mdororo mkubwa wa uchumi mwaka huu, kushuka kwa kasi kwa ukuaji kunatarajiwa katika sehemu za Ulaya Magharibi na Kati, Kusini na Kusini-mashariki mwa Asia.

Rebeca Grynspan, katibu mkuu wa UNCTAD amesema: "Athari za kiuchumi za vita vya Ukraine zitazidisha mdororo wa sasa wa uchumi wa dunia na kudhoofisha ahueni ya kujikwamua kutoka kwa janga la coronavirus">COVID-19."

Shirika la fedha duniani (IMF) lilikuwa tayari limeonya kwamba mzozo wa Ukraine ungepunguza ukuaji wa uchumi na kusababisha mfumuko wa bei kuongezeka.

Shirika hilo linajiandaa kusahihisha utabiri wake wa awali wa ukuaji wa kimataifa wa uchumu kwa asilimia 4.4% katika mikutano yake ya majira ya chipukizi itakayoanza katikati ya mwezi Aprili.

Afrika kukabiliana na kupanda kwa bei ya vyakula

Marekani, ingawa imekingwa kwa kiasi kutokana na majanga ya sasa, lakini ripoti inasema itakabiliwa na shinikizo la ziada kwa matumizi ya watumiaji kutokana na kupanda kwa bei ya mafuta na vyakula.

Ulaya itaathirika zaidi na bei ya juu ya bidhaa kutokana na mzozo wa Ukraine.

Kuhusu uchumi wa China, UNCTAD inaamini kwamba lengo lililotangazwa hapo awali la ukuaji wa uchumi kwa asilimia 5.5% litakuwa changamoto.

Uchumi mwingine wa Asia utakabiliwa na dhoruba kali kutokana na mzozo huo.

Katika bara la Afrika, nchi zitaathiriwa kwa njia isiyo sawa, lakini utabiri wa ukuaji wa uchumi kwa mwaka 2022 kwa kanda hiyo kwa ujumla utakuwa chini kuliko makadirio yaliyotolewa mapema mwaka huu.

Uzito mkubwa wa mauzo ya mafuta na gesi kutoka kanda hiyo utasaidia kuongeza ukuaji wa uchumi.

Wakati bara linaweza kutegemea mauzo ya malighafi kutoka nje ya nchi, uchumi mwingi wa Afrika pia unategemea chakula au unakabiliwa na vikwazo vya usambazaji, imeeleza ripoti hiyo ya UNCTAD.

Kwa ujumla, mshtuko huo wa bidhaa duniani utamaanisha "mshtuko hasi kwa kanda kwa ujumla, hasa kupitia bei za vyakula na matumizi ya ndani".

UNCTAD inahofia kuwa mchanganyiko wa kudhoofika kwa mahitaji ya kimataifa na viwango vya juu vya madeni kutokana na janga hili vinaweza kusababisha "mawimbi ya mshtuko wa kifedha".

Haya yana uwezekano wa kusukuma baadhi ya nchi zinazoendelea katika "wimbi la kufilisika au madeni, mdororo wa kiuchumi na kudumaa kwa maendeleo".

Wafanyakazi wa Shirika la chakula duniani, WFP wakipakia magunia ya nafaka katika gari El Fasher, Darfur Kaskazini, Sudan.
© UN Photo/Albert Gonzalez Farran
Wafanyakazi wa Shirika la chakula duniani, WFP wakipakia magunia ya nafaka katika gari El Fasher, Darfur Kaskazini, Sudan.

 Kupanda kwa bei na mzigo wa madeni kwa nchi zinazoagiza chakula nje

Ni hali ya kutia wasiwasi, haswa kwani vita tayari vinasababisha kupanda kwa bei ya nishati na bidhaa za kimsingi. Shinikizo la ziada kutokana na kupanda kwa bei linazidisha wito wa mabadiliko ya sera katika nchi za uchumi wa hali ya juu. Hii inatishia kudorora kwa kasi kwa uchumi kuliko ilivyotarajiwa,” ripoti hiyo imesema.

Kulingana na UNCTAD, kupanda kwa bei ya vyakula na mafuta kutakuwa na athari za mara moja kwa walio hatarini zaidi katika nchi zinazoendelea, "kuleta njaa na ugumu wa maisha kwa kaya zinazotumia mapato yao mengi kwa chakula".

Pia imeongeza kuwa "Kupanda kwa bei kunatishia maisha, kukatisha tamaa uwekezaji na kuibua wasiwasi wa kuongezeka kwa nakisi ya biashara”.

Hivyo UNCTAD ina wasiwasi juu ya hatima ya nchi 104, zikijumuisha zaidi ya nchi 30 zilizo hatarini sana, ambazo ni waagizaji wa jumla wa bidhaa za chakula. Walikuwa na jumla ya deni la nje la nje la dolatrilioni $1.4 mwishoni mwa 2020.

"Nchi hizi zinakabiliwa na dola bilioni 153 katika malipo ya madeni yanayotarajiwa mwaka wa 2022, ambayo yanaweza kuwa hatarini ikiwa bei ya kimataifa ya chakula itaendelea kupanda," , Richard Kozul-Wright, mkurugenzi wa idara ya utandawazi na mikakati ya maendeleo katika kamati ya UNCTAD ameuambia mkutano wa wanahabari huko Geneva Uswis.

Nchi zinazoendelea zinakadiriwa kuhitaji dola bilioni 310 ili kuweza kulipa madeni yake ya  nje kwa mwaka 2022, sawa na asilimia 9.2 ya madeni ya nje ambayo hayajalipwa mwishoni mwa mwaka 2020, kulingana na tathimini ya UNCTAD.

Miongoni mwa nchi hizi zilizo hatarini ni Pakistan, Mongolia, Sri Lanka, Misri na Angola.

Tatu kati yao, Pakistan, Misri na Angola, tayari wana programu za muda mrefu za IMF. "Nchi nyingi zinazoendelea sasa zinakabiliwa na msukosuko mkubwa kutokana na vita. Ikiwa hii itasababisha machafuko au la, wasiwasi mkubwa wa kijamii tayari unaenea,” ameonya Bi Grynspan.

Katika mapendekezo yake, UNCTAD inatetea ongezeko la matumizi ya haki maalum ili kuongeza akiba rasmi na kutoa ukwasi kwa wakati ili kuepuka marekebisho makubwa ya upunguzaji wa bei.

Pia inachagiza kukuza sera za kisekta, ikiwa ni pamoja na udhibiti wa bei na ruzuku, ili kukabiliana na shinikizo la mfumuko wa bei kutoka upande wa ugavi na malighafi.

UNCTAD pia inapendekeza usaidizi mkubwa zaidi wa kifedha , usio na masharti, na wa kimataifa kwa nchi zinazoendelea ili kuziwezesha kuhimili misukosuko ya kifedha na kiuchumi na kuongeza uwekezaji ili kuendeleza ukuaji wa uchumi.