Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNHCR yatoa wito kwa mataifa ya Asia kuokoa watu 190 waliokwama katika bahari ya Andaman

 Boti inayobeba wakimbizi wa Rohingya iliyokwama katika bahari ya Adaman. Watu wanasubiri kupatiwa chakula. (Maktaba)
© UNHCR/Christophe Archambault
Boti inayobeba wakimbizi wa Rohingya iliyokwama katika bahari ya Adaman. Watu wanasubiri kupatiwa chakula. (Maktaba)

UNHCR yatoa wito kwa mataifa ya Asia kuokoa watu 190 waliokwama katika bahari ya Andaman

Msaada wa Kibinadamu

Takriban watu 190 waliokata tamaa wako kwenye hatihati ya kuangamia baharini, wakiwa wamekwama kati ya Bahari ya Andaman na Ghuba ya Bengal, limeeleza shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR likizitaka nchi za kusini mwa Asia kuwaokoa.

Hata hivyo, Mkurugenzi wa UNHCR kwa Asia na Pasifiki Indrika Ratwatte katika taarifa yake aliyoitoa leo amesema maombi yake yanaendelea kupuuzwa. “Janga hili la kushtua lazima lisiendelee, hawa ni binadamu - wanaume, wanawake na watoto”.

Hali zao ni mbaya

Ripoti zinaonesha kuwa watu hao wamekuwa baharini katika hali mbaya kwa mwezi mmoja, wakikosa chakula cha kutosha au maji, na hakuna juhudi kutoka kwa Mataifa yoyote katika eneo hilo kusaidia.

Wengi ni wanawake na watoto, huku kukiwa na taarifa za takriban watu 20 kufariki kwenye chombo hicho ambacho kinaweza kuzama baharini wakati wa safari.

"Tunahitaji kuona Mataifa katika eneo hilo yakisaidia kuokoa maisha na kutoruhusu watu kufa", alisisitiza Bw. Ratwatte.

Mwezi mzima baharini

Tangu ripoti za kwanza za mashua kuonekana kwenye upande wa Thailand, UNHCR imepokea taarifa ambazo hazijathibitishwa za meli hiyo kuonekana karibu na Indonesia na baadaye pwani ya Visiwa vya Andaman na Nicobar nchini India.

Eneo lake la sasa linaripotiwa kwa mara nyingine tena kuelekea mashariki, katika bahari ya Andaman kaskazini mwa Aceh.

UNHCR imeziomba mara kwa mara nchi zote katika eneo hilo kuweka kipaumbele cha kuokoa maisha na kuomba kituo cha uokoaji baharini cha India mapema wiki hii kuruhusu watu hao waweze kuteremka.

"Inasikitisha kujua kwamba watu wengi tayari wamepoteza maisha yao, wakiwemo watoto", aliongeza Ratwatte wa UNHCR.

Mwaka mbaya baharini

Ni vigumu sana kwa UNHCR kuthibitisha taarifa hizo, lakini ikiwa ni kweli, idadi ya waliofariki na kupotea katika Ghuba ya Bengal na Bahari ya Andaman itarekodiwa hadi karibu watu 200 mwaka huu pekee.

Mataifa yote yana jukumu la kuwaokoa wale walio kwenye mashua na kuwaruhusu kuteremka kwa usalama kwa misingi ya ubinadamu, UNHCR imeeleza.

Wakati huo huo, idadi hii ya kushangaza inawakilisha karibu asilimia 10 ya makadirio ya watu 2,000 ambao wametumia njia hii ya hatari ya kusafiri baharini katika eneo hilo tangu Januari.

"Kwa kusikitisha, hii inafanya kuwa moja ya miaka hatari zaidi katika bahari katika eneo hilo," alilalamika Mkurugenzi huyo wa UNHCR.

Hapo Jana mtaalam huru wa haki za binadamu aliyeteuliwa na Umoja wa Mataifa Tom Andrews alitoa taarifa akizitaka Serikali "mara moja na haraka kuratibu utafutaji na uokoaji wa mashua hii na kuhakikisha kuwa wanashuka salama kabla ya kupoteza maisha zaidi".

"Wakati watu wengi duniani wanajiandaa kufurahia msimu wa sikukuu na kuukaribisha mwaka mpya, boti zinazobeba wanaume, wanawake na watoto wadogo wa Rohingya, zinaendelea na safari za hatari kwa meli zisizofaa kusafirisha watu," alisema Mtaalamu Maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu Myanmar.

Katika ombi lake kwa Serikali zote za kikanda kwa "kuzingatia ubinadamu katika ukanda huo” kwa wale wanaokimbia ghasia za kikatili za junta, ikiwa ni pamoja na Rohingya, Mtaalamu huru Andrews alitoa wito wa "kusitishwa kabisa kwa uhamisho au kurudi nyuma kwa Myanmar" na vile vile utafutaji na usawazishaji na uokoaji baharini.

Safari za hatari

Hii ni moja ya safari za hivi karibuni katika mfululizo wa safari hatari, alisema mtaalamu huyo wa Umoja wa Mataifa.

Wiki mbili zilizopita, meli ya kampuni ya mafuta ya Vietnam iliyokuwa ikielekea Myanmar iliokoa mashua moja iliyozama ikiwa na wakimbizi 154 wa Rohingya.

"Walipokuwa karibu na maji ya Myanmar, waliripotiwa kukabidhi kundi hilo kwa mamlaka ya Myanmar", alisimulia.

"Imeripotiwa kuwa waliokuwemo ndani waliwekwa katika kizuizi cha wahamiaji nchini Myanmar na sasa wanaweza kukabiliwa na mashtaka ya uhalifu".

Na mwisho wa wiki iliyopita, Jeshi la Wanamaji la Sri Lanka liliokoa meli ya tatu katika hali ya tabu, ikiwa imebeba Warohingya 104, wakiwemo watoto wengi, wengine bila kusindikizwa.

"Jumuiya ya kimataifa lazima isonge mbele na kusaidia watendaji wa kikanda kutoa suluhisho la kudumu kwa Warohingya", alisema Andrews.