Mtaalam maalum wa haki za binadamu kuhusu ubaguzi wa rangi, Tendayi Achiume ameelezea wasiwasi wake kuhusu mpango wa India wa kutaka kuwarejesha kinguvu nyumbani warohingya wanaume saba, akisema kitendo hicho ni kinyume cha sheria za kimataifa.
Warohingya hao wanatoka kijiji cha Kyauk Daw kilichoko jimbo la kati la Rakhine nchini Mynmar na wamepangiwa kurejeshwa Kesho oktoba tatu. Watu hao wamekuwa ndani tangu mwa ka wa 2012 kwa madai ya kuingia India kinyume na sheria.
Bi. Achiume amesema kuwa ,” “Kwa kuzingatia utambulisho wa kabila la wanaume hawa, huku ni kuwanyima haki yao ya ulinzi na kunaweza kuwa ni kosa. Serikali ya India inawajibika kimataifa kuelewa kuhusu ubaguzi, chuki na ukiukwaji wa haki za binadamu vinavyowakibili watu hao nchini mwao na India inafaa kuwapatia ulinzi.”
Taarifa inasema serikali ya India inapaswa kuwakabidhi watu hao inaowashikilia kwa shirika la kuhudumia wakimbizi la Umoja wa Mataifa, UNHCR ili mahitaji yao ya usalama yaweze kushughulikiwa.
Mpango wa kuwarejesha Myanmar unafuatia amri ya serikali ya Agosti 8 mwaka wa 2017 ya kuwarejesha nyumbani warohingya hao.
Mahakama kuu ya India bado inatafakari rufaa inayopinga uamuzi huo wa mwaka 2017 kwa msingi kwamba ni kinyume na katiba ya nchi.