Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Watoto nchi nzima ya Afghanistan wapatiwa chanjo za Surua na Polio

Msichana mdogo akipokea chanjo yake ya surua na polio kama sehemu ya kampeni ya chanjo ya nchi nzima nchini Afghanistan.
© WHO Afghanistan
Msichana mdogo akipokea chanjo yake ya surua na polio kama sehemu ya kampeni ya chanjo ya nchi nzima nchini Afghanistan.

Watoto nchi nzima ya Afghanistan wapatiwa chanjo za Surua na Polio

Afya

Zaidi ya watoto milioni 5 nchini Afghanistan wenye umri wa kuanzia miezi 9 hadi miaka 5 wamepatiwa chanjo dhidi ya surua ilhali watoto zaidi ya milioni 6 wenye umri wa kuanzia kuzaliwa hadi miaka 5 wamepatiwa chanjo dhidi ya polio katika kampeni ya kitaifa iliyoanza mwezi uliopita wa Novemba hadi tarehe 12 mwezi huu wa Desemba.

Mwakilishi wa shirika la Umoja wa Mataifa la afya ulimwenguni WHO nchini humo Dkt. Luo Dapeng amenukuliwa katika taarifa iliyotolewa na shirika hilo mjini Kabul, Afghanistan akisema inatia moyo kuona ya kwamba wameweza kulinda watoto wa Afghanistan dhidi ya magonjwa hayo hatari wakati huu wakianza majira ya baridi kali.

“Hii ni mara ya kwanza kufanya kampeni ya nchi nzima ya utoaji chanjo ya Surua na Polio tangu uongozi mpya ushike madaraka mwezi August 2021, na nawashukuru wafanyakazi wote wa sekta ya afya, wadau na wafadhili ambao wamewezesha kampeni hii kufanikiwa,” amesema Dkt. Dapeng

Kwa mujibu wa takwimu kutoka wizara ya afya ya umma na program ya utoaji chanjo, kampeni hii imetekelezwa katika wilaya 329 za majimbo yote 34 ya Afghanistan.

Kampeni hii ilijumuisha jumla ya timu 4341 za kutoa chanjo na kila timu moja ilikuwa na watu wanne.

Watoto wakionyesha alama kwa vidole baada ya kupokea chanjo ya nchini Afghanistan
Picha: © WHO Afghanistan
Watoto wakionyesha alama kwa vidole baada ya kupokea chanjo ya nchini Afghanistan

Kuhusu ugonjwa wa Surua

Surua ni moja ya magonjwa hatari duniani, ugonjwa huu mpaka sasa hauna matibabu maalum na namna ya kujikinga nao ni kupata chanjo.

Mtu anayeugua ugonjwa huu anaweza kuhara, kupungukiwa maji mwilini, kupata nimonia, matatizo ya masikio na macho. Mgonjwa wa surua pia anaweza kupata uvimbe kwenye ubongo, ulemavu wa kudumu na hata kifo.

Kabla ya kampeni hii nchi nzima, kulikuwa na mfululizo wa utoaji chanjo za surua katika wilaya 141 ambapo watoto milioni 3 walipatiwa chanjo.

Mwakilishi huyu wa WHO nchini Afghanistan anasema faida za chanjo hii ziko wazi, kwani ushahidi unaonesha chanjo ya surua iliokoa zaidi ya maisha milioni 23 duniani kote katika kipindi cha miaka 20 iliyopita.

“Surua inaambukiza sana, pia ni ugonjwa unaoweza kuzuilika. Hatupaswi kupoteza miongo kadhaa ya maendeleo ambayo tumefikia katika kutoa chanjo na kulinda watoto wa Afghanistan. Chanjo ya surua ni salama na imekuwa ikitumika kwa zaidi ya miaka 50,” aliongeza Dkt. Dapeng.

Wafadhili wa kampeni ya utoaji chanjo

Kampeni ya surua nchini Afghanistan iliungwa mkono na WHO na Shirika la Umoja wa Mataifa linalojihusisha na masuala ya watoto UNICEF.

Mashirika haya yalihusika na masuala ya ununuzi na utoaji wa chanjo, kuandaa miongozo ya chanjo na vifaa vya mawasiliano, na kuwajengea uwezo wahudumu wa afya ili waweze kusimamia na kutekeleza kampeni hiyo na kuhakikisha kuwa watoto wote wanaostahili wanalindwa kwa njia salama na chanjo zinazofaa kwa surua na polio.

Msaada wa kifedha kwa kampeni hiyo ulitolewa na Muungano wa kimataifa wa kugawa chanjo wa GAVI.