Kampeni ya #Vaccineswork kutumika mtandaoni kuimarisha utoaji chanjo- UNICEF

18 Aprili 2019

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF tarehe 24 mwezi huu wa Aprili linazindua kampeni kamambe ya chanjo ili kukabiliana na ongezeko la milipuko  ya magonjwa yanayoweza kuzuilika kwa chanjo.

Taarifa ya UNICEF iliyotolewa leo mjini New York, Marekani inasema kampeni hiyo itakayoenda sambamba na wiki ya chanjo inayoanza tarehe 24 hadi 30 mwezi Aprili inabeba maudhui Tulindwe pamoja, CHanjo inafanya kazi.

UNICEF inasema lengo kuu ni kusisitiza umuhimu, uthabiti na usalama wa chanjo miongoni mwa wazazi na watumiaji wa mitandao ya kijamii.

Katika kampeni hiyo, UNICEF itashirikiana na taasisi ya Bill na Melinda Gates sambamba na shirika la afya duniani, WHO na fuko la chanjo duniani, GAVI kuhakikisha kampeni inakwenda mbali zaidi.

Taasisi ya Bill na Melinda Gates itachangia dola  1 kwa kila taarifa itakayochapishwa kwenye mtandao wa kijamii na kupendwa au kusambazwa zaidi pindi watakapotumia #VaccinesWork kwa kipindi chote cha mwezi Aprili na lengo ni kufikia dola milioni 1.

Matarajio ni kuhakikisha watoto wote wanapata chanjo wanazohitaji kuokoa maisha yao.

Mtoto huyu mkazi wa Sana'a mji mkuu wa Yemen akisubiria kupatiwa chanjo ya Surua na Rubella zinazotolewa na wahudumu wa afya kwenye kampeni iliyoendeshwa na UNICEF mwaka huu wa 2019
UNICEF/Aidroos Alaidroos
Mtoto huyu mkazi wa Sana'a mji mkuu wa Yemen akisubiria kupatiwa chanjo ya Surua na Rubella zinazotolewa na wahudumu wa afya kwenye kampeni iliyoendeshwa na UNICEF mwaka huu wa 2019

Mkuu wa chanjo UNICEF Robin Nandy anasema, wanataka kampeni ya matumizi ya #VaccineWork isambae mtandaoni kwa kuwa, “chanjo ni salama, zinaokoa maisha na ni  fursa ya kuonesha dunia kuwa mitandao ya kijamii inaweza kuwa na nguvu ya kuleta mabadiliko chanjo na pia kuwapatia wazazi taarifa za kuamini juu ya chanjo.”

Kila mwaka chanjo huokoa maisha ya hadi watu milioni 3, zikilinda watoto dhidi ya magonjwa hatari kama vile surau, kipindupindu, dondakoo na vichomi.

UNICEF inasema ni kutokana na matumizi ya chanjo ndio maana idadi ya vifo kutokana na surau vilipungua kati yam waka 2000 na 2017 na polio iko katika harakati za kutokomezwa.

Shirika hilo linasisitiza kuwa chanjo ndio njia bora zaidi na nafuu ya kuimarisha afya ambapo kila dola moja inayotumika kwenye chanjo wakati wa utoto inarejesha faida ya dola 44.

Hata hivyo licha ya manufaa ya chanjo, watoto wapatao milioni 1.5 walifariki dunia mwaka 2017 kutokanana magonjwa yanayozuilika kwa chanjo ambapo ingawa kwenye nchi zingine ni kutokana na uhaba wa chanjo, kwingineko ni familia kuchelewa kuwapeleka watoto kupata chanjo kutokana na imani potofu juu ya chanjo hizo.

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter