Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

WHO na wadau wasongesha chanjo dhidi ya kipindupindu Malawi

Robert Mwale, (wa 2 kushoto) amepona kipindupindu. Sasa ni tabasamu akiwa nyumbani kwake huko kijiji cha Mfufu nchini Malawi.
UNICEF Malawi
Robert Mwale, (wa 2 kushoto) amepona kipindupindu. Sasa ni tabasamu akiwa nyumbani kwake huko kijiji cha Mfufu nchini Malawi.

WHO na wadau wasongesha chanjo dhidi ya kipindupindu Malawi

Afya

Kampeni ya kutoa chanjo dhidi ya ugonjwa wa kipindipindu nchini Malawi ikiwa imeingina siku ya nne hii leo  na ikitarajiwa kumalizika kesho, shirika la Umoja wa Matiafa la afya ulimwenguni, WHO barani Afrika imesema kampeni inaendelea vizuri na imekuja wakati mzuri ambapo ni msimu wa mvua na maji yanaweza kubeba vijidudu kwa urahisi kwa hiyo kinga itasaidia kuepusha maambukizi. 

Taarifa ya WHO kanda ya Afrika iliyotolewa kwenye mji mkuu wa Malawi, Likongwe inasema kampeni hiyo inalenga watu milioni 2.9 wenye umri wa kuanzia mwaka mmoja na kuendelea. 

Eneles Amos akionesha cheti alichopatiwa baada ya kupata chanjo dhidi ya kipindupindu nchini Malawi.
UNICEF Malawi
Eneles Amos akionesha cheti alichopatiwa baada ya kupata chanjo dhidi ya kipindupindu nchini Malawi.

Hadi Novemba 2022, watu 299 wamekufa kwa kipindupindu Malawi 

Mlipuko wa sasa wa kipindupindu alianza mwezi Februari mwaka huu wa 2022 na hadi tarehe 27 mwezi uliopita wa Novemba kulikuwa na wagonjwa 103306 na kati yao hao 299 wamefariki dunia. Ugonjwa huo umeripotiwa katika wilaya zote 29 za taifa hilo la kusini mwa Afrika. 

WHO kupitia kundi la kimataifa la uratibu wa chanjo, ICG, limeweza kupata jumla ya dozi milini 2.9 za chanjo dhidi ya kipindupindu na ufadhili ni kutoka Fuko la chanjo duniani, GAVI. 

Shirika hilo la Umoja wa Mataifa la afya ulimwenguni, linapendekeza matumizi ya chanjo dhidi ya kipindupindu ili kudhibiti mlipuko na kuepusha kusambaa zaidi kwa ugonjwa huo katika maeneo mengine. 

“Kampeni hii ya chanjo imekuja wakati muafaka wakati wa msimu wa mvua ambapo maji yanaweza kupata vijidudu kwa urahisi. Lakini chanjo ni kipande kimoja tu cha majawabu cha kudhibiti kipindupindu: Juhudi za pamoja za kutibu wagonjwa na kuboresha mifumo ya maji safi na majitaka ni muhimu zaidi,” amesema Dkt. Neema Rusibamayila Kimambo, Mwakilishi wa WHO nchini Malawi. 

Hii ni kampeni ya pili ya kukabili mlipuko wa kipindupindu nchini Malawi, ambapo kampeni ya aina hii ilifanyika mwezi Juni mwaka 2022 kwenye mkoa wa kusini mwa taifa hilo. 

Daina Denja akipata chanjo dhidi ya kipindupindu kwenye kijji cha Misili, wilaya ya Chikwawa nchini Malawi.
UNICEF Malawi
Daina Denja akipata chanjo dhidi ya kipindupindu kwenye kijji cha Misili, wilaya ya Chikwawa nchini Malawi.

Chanjo sambamba na kampeni ya usafi 

Kampeni ya sasa inapatia kipaumbele wilaya 13 zenye idadi kubwa ya wagonjwa ambazo ni Karonga, Rumphi, Mzimba North, Mzimba South, Likoma, Nkhatabay, Chitipa, Lilongwe, Salima, Nkhotakota, Kasungu, Nsanje, na Zomba.  

Pamoja na kupigia chepuo chanjo, WHO na shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto duniani, UNICEF na wadau wanasaidia serikali ya Malawi kutoa huduma za matibabu kwenye vituo vya tiba vilivyoanzishwa karibu na maeneo ya makazi. 

Halikadhalika wanapatia mafunzo wahudumu wa afya na kuimarisha mifumo ya kusafisha maji, na kutoa elimu kuhusu usafi na kujikinga na magonjwa. 

Kipindupindu huambukizwa vipi? 

Kipindupindu ni ugonjwa usababishao mgonjwa kuhara kwa kiasi kikubwa na husababishwa na na kula chakula au kunywa maji yenye kinyesi na kisababishi ni kimelea aina ya Vibrio cholerae.  

Ugonjwa huu unaweza kusababisha kifo iwapo tiba sahihi haitatolewa mara baada ya mgonjwa kuambukizwa.