Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Msaada wa dola milioni 14 kutoka CERF kunufaisha zaidi ya watu 260,000 Sudan Kusini

Mafuriko ya hivi karibuni nchini Sudan Kusini
Picha: UN News
Mafuriko ya hivi karibuni nchini Sudan Kusini

Msaada wa dola milioni 14 kutoka CERF kunufaisha zaidi ya watu 260,000 Sudan Kusini

Msaada wa Kibinadamu

Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa masuala ya dharura, Martin Griffiths ametangaza kutoa dola million 14 kutoka mfuko mkuu wa dharura wa Umoja huo, CERF kwa ajili ya kupatia misaada ya kibinadamu wananchi wa Sudan Kusini walioathiriwa na ongezeko la mapigano na mafuriko, kwa kuzingatia kuwa ombi la usaidizi kwa taifa hilo bado uchangiaji wake unasuasua. 

Taarifa iliyotolewa leo huko Juba, Sudan Kusini na Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya uratibu wa misaada ya dharura, OCHA imesema fedha zinalenga zaidi ya watu 260,000 na zitatumiwa na mashirika ya kibinadamu ya Umoja wa Mataifa nchini humo kutekeleza miradi ya usaidizi wa kibinadamu. 

Mashirika hayo ni lile la kuhudumia watoto, UNICEF, la afya, WHO, la uhamiaji, IOM, wakimbizi, UNHCR na mpango wa chakula duniani, WFP. 

Mapigano ya kila mara yamesababisha jamii kuhama makazi katika jimbo la Upper Nile nchini Sudan Kusini. (Maktaba))
© UNICEF/Phil Hatcher-Moore
Mapigano ya kila mara yamesababisha jamii kuhama makazi katika jimbo la Upper Nile nchini Sudan Kusini. (Maktaba))

Maeneo yaliyoathirika zaidi 

Mratibu wa Umoja wa Mataifa wa masuala ya kibinadamu nchini Sudan Kusini Beysolowo Nyanti amesema mashirika hayo yatatumia mfumo unaomulika mahitaji ya eneo husika ili kufikisha kile kinachohitajika zaidi kwa wananchi. 

“Waathirika wamekumba na changamoto lukuki zilizowalazimu kukimbia makazi yao, wengine wamepoteza mbinu zao za kujipatia kipato halikadhalika kule walikokuwa wanategemea kupatiwa msaada,” amesema Bi, Nyanti. 

Ametaja maeneo lengwa zaidi ni majimbo ya Unity, Upper Nile, Bhar-el-Ghazal Kaskazini, Jonglei na Warrap halikadhalika eneo la Abyei. 

Misaada ni pamoja na afya, elimu, maji na huduma za kujisafi ambapo Mratibu huyo amesisitiza  “umuhimu wa kupatia kipaumbele watu walio kwenye mahitaji zaidi miongoni mwa wakimbizi wa ndani na jamii za wenyeji zinazowahifadhi. Wanawake na wasichana, wazee na watu wenye mahitaji maalum na wale waliosalia nyuma kutokana na kushindwa kuondoka makwao mara nyingi wanabeba mzigo mkubwa kwenye majanga haya yasiyoisha na hivyo wanahitaji msaada.” 

Wahitaji walitambuliwa vipi? 

Taarifa hiyo ya OCHA imesema watu wenye mahitaji walitambuliwa baada ya mashauriano ya kina kupitia majukwaa mbalimbali yaliyojumuisha pia mashirika ya kiraia nchini Sudan Kusini. 

Kuhakikisha mashinani msaada huo unafika vizuri, asilimia 15 ya fedha hizo zitapelekwa kwa mashirika ya kiraia ya kitaifa nchini Sudan Kusini yakiwemo yale yanayoongozwa na wanawake yakishirikiana na mashirika ya Umoja wa Mataifa. 

“Miradi inayofadhiliwa itajikita kwenye ulinzi, jinsia na ujumuishaji na juhudi za pamoja za uwajibika kwa wananchi walioathirika,” imesema taarifa hiyo. 

Hali ya kibinadamu Sudan Kusini 

Bi. Nyanti amesema machungu ni mengi miongoni mwa raia Sudan Kusini, “hatuwezi kuwaacha wengi hao walio hatarini. Ombi la usaidizi wa kibinadamu kwa Sudan Kusini halijafadhiliwa ipasavyo na hivyo kuacha mamilioni ya watu wakiwa hatarini. Tunahitaji majawabu ya muda mrefu ili kuziba pengo hili la ufadhili na kufungua njia ya maendeleo.” 

Takribani watu milioni 9.4 nchini Sudan Kusini wako hatarini zaidi na watahitaji msaada wa kibinadamu mwaka 2023 ikilinganishwa na watu milioni 8.9 waliohitaji msaada mwaka 2022. Hadi tarehe 13 mwezi huu wa Desemba, mwitikio wa ombi la usaidizi kwa Sudan Kusini ulikuwa aislimia 67.3.