Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Jamii ziwezeshwe ili ziongoze harakati za kutokomeza majanga ya kiafya

Muuguzi akifanya kikao cha uhamasishaji kuhusu maambukizi ya VVU katika kituo cha afya nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.
© UNICEF/Gwenn Dubourthoumieu
Muuguzi akifanya kikao cha uhamasishaji kuhusu maambukizi ya VVU katika kituo cha afya nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Jamii ziwezeshwe ili ziongoze harakati za kutokomeza majanga ya kiafya

Afya

Katika mkutano wa kimataifa kuhusu Ukimwi unaoendelea huko Thailand, wawakilishi kutoka serikali, mashirika ya kiraia na Umoja wa Mataifa wamesema majanga ya kiafya duniani likiwemo janga la UKIMWI yanaweza kutokomezwa pale tu jamii zitakapoungwa mkono na kuongoza harakati za kutokomeza majanga hayo. 

Taarifa ya shirika la Umoja wa Mataifa la kukabiliana na UKIMWI, UNAIDS iliyotolewa kwenye mj iwa Chiang Mai nchini Thailand imesema hatua zinazoongozwa na jamii ziwe rasmi au si rasmi ni lazima zipewe kipaumbele kwenye ufadhili nah atua hizo ni pamoja na zile zinazojumuisha watu kutembelea mashinani wakiwemo wanaoaminika kwenye jamii ili kupaza sauti dhidi ya UKIMWI halikadhalika ushiriki wa jamii kwenye utoaji wa maamuzi.  

Mkutano huo umeshuhudia kuchapishwa kwa mara ya kwanza kwa ainisho la kwanza kabisa la hatua zinazoongowa na jamii katika kukabili majanga baada ya mashaurino ya miaka miwili yaliyohusisha wawakilishi wa serikali 11 kutoka kila bara duniani, halikadhalika wawakilishi wa mashirika 11 yasiyo ya kiserikali. 

Jopo hilo la UNAIDS la wadau kutoka serikali na mashiriki ya kiraia liliitishwa kwa pamoja na shirika la Umoja wa Mataifa la afya ulimwenguni, WHO na shirika la Umoja wa Mataifa la mpango wa maendeleo duniani, UNDP na kuwasilisha ripoti yake kwenye mkutano wa 51 wa bodi ya uratibu ya UNAIDS iliyokutana huko huko Thailand kando mwa mkutano huo wa kimataifa wa UKIMWI. 

Mipango mipya ishirikishe jamii katika kukabili majanga 

Wakitumia ainisho hilo jipya ya ushiriki wa jamii kwenye harakati za kukabili majanga ya kiafya, Waziri wa Afya wa Ujerumani Profesa Karl Lauterbach na Mkurugenzi MTendaji wa UNAIDS Winnie Byanyima leo wamechapisha kwenye jarida la kitabibu la Lancet, Makala inayotaka mipango mipya na makubaliano ya kimataifa na ufadhili ijumuishe miundombinu ya kijamii katika kinga, kujiandaa na hatua dhidi ya majanga. 

Katika hilo, viongozi hao wanaonesha kuwa miundombinu thabiti ya kijamii inayoshirikiana kwa dhati na serikali, ni muhimu lakini mara nyingi huenguliwa au kupuuzwa katika harakati za kinga, maandalizi na hatua dhidi ya majanga,” imesema taarifa hiyo. 

Waweka ushahidi wazi ni vipi jamii ina mchango chanya 

Kwa kutumia ushahidi kutoka majanga ya UKIMWI, COVID-19, MPOX na Ebola, Profesa Lauterbarch na Bi. Byanyema wanaeleza ni kwa vipi mashirika yanayoongozwa na jamii yanajenga imani, yanasambaza taarifana kufikia makundi yaliyo pembezoni na hivyo kusaidia harakati za serikali na kuimarisha uwiano. 

Ainisho hilo jipya na mapendekezo, kwa mujibu wa UNAIDS, vitasaidia wataalamu wa mipango na wahisani wa harakati za UKIMWI kuwa na mipango mujarabu inayojumuisha jamii.