Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ushirikiano ni muhimu kutokomeza UKIMWI ifikapo 2030 

Mwanamume akipokea dawa za matibabu dhidi ya VVU wakati wa janga la COVID-19 nchini Colombia.
© PAHO/Diego Vega
Mwanamume akipokea dawa za matibabu dhidi ya VVU wakati wa janga la COVID-19 nchini Colombia.

Ushirikiano ni muhimu kutokomeza UKIMWI ifikapo 2030 

Afya

Mwaka mmoja tangu kupitishwa kwa azimio jipya la kisiasa kuhusu Virusi Vya Ukimwi, VVU na UKIMWI, ni dhahiri shahiri kuwa ushirikiano baina ya nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa ni muhimu ili kufanikisha utekelezaji wa azimio hilo. 

Azimio lilipitishwa mwezi Juni mwaka jana wakati wa mkutano wa ngazi ya juu wa viongozi kwa lengo la kuongeza juhudi za kutokomeza UKIMWI, ugonjwa ambao kwa mujibu wa shirika la Umoja wa Mataifa la kupambana na UKIMWI, UNAIDS, unasababisha vifo vya watu 13,000 kila wiki. 

Taarifa ya UNAIDS iliyotolewa leo jijini New York, Marekani kufuatia mkutano wa jana Alhamisi wa kutathmini mwaka mmoja baada ya kupitishwa kwa azimio hilo, inasema “nchi wanachama wameangazia umuhimu wa kushirikiana na kuongeza kasi kutekeleza azimio.” 

Kuna malengo ya 2025 

Zaidi ya wawakilishi wa nchi 35 wanachama wa Umoja wa Mataifa, walizungumza katika mkutano huo uliofanyika kwenye ukumbi wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa na wakisisitiza uharaka wa hatua za pamoja ili kufikia malengo ya mwaka 2025 sambamba na kushughulikia suala la ukosefu wa usawa wakati wa kukabiliana na VVU. 

Malengo ya mwaka 2025 yanaweka msisitizo katika kuondoa vikwazo vya kijamii na kisheria katika utoaji wa huduma za VVU na UKIMWI sambamba na kuunganisha au kujumuisha huduma za VVU na nyingine zinazohitajika na watu wanaoishi na VVU. 

Takwimu za UNAIDS zinaonesha kuwa maambukizi ya VVU na vifo visababishwavyo na UKIMWI havipungui kwa kasi inayotakiwa ili kutokomeza janga hilo ifikapo mwaka 2030 kama ilivyokubaliwa. 

Mwanamke aliyezaliwa na VVU akipokea dawa kwenye kliniki nchini Burkina Faso
© UNICEF/Frank Dejongh
Mwanamke aliyezaliwa na VVU akipokea dawa kwenye kliniki nchini Burkina Faso

Hakuna usawa katika kutokomeza UKIMWI 

Mwezi uliopita wa Mei, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres alitoa ripoti kuhusu utekelezaji wa azimio hilo la kisiasa, kama ambavyo azimio lilimtaka afanye ambapo ameonesha ni kwa jinsi gani ukosefu wa usawa na ukosefu wa uwekezaji unaifanya dunia iwe katika fursa finyu ya kushughulikia majanga ya sasa na ya siku zijazo. 

Akitoa taarifa ya Katibu Mkuu mbele ya Baraza Kuu wakati wa kikao cha tathmini ya mwaka mmoja wa azimio, Mkuu wa Ofisi ya Katibu Mkuu, Courtenay Rattray ametaja mambo makuu matatu ya kuzingatiwa ili kubadili mwelekeo wa sasa. 

Nini kifanyike? 

“Mosi, kushughulikia ukosefu wa usawa, ubaguzi na uenguaji wa jamii hali ambayo huongezewa makali zaidi kwa utungaji wa sheria za adhabu na sera,” amesema Bwana Rattray huku akitoa wito wa marekebisho ya sera ili kupunguza hatari zaidi ya maambukzi ya VVU kwa makahaba, watu wanaojidunga madawa ya kulevya, wafungwa, waliobadili jinsia na wanaume mashoga. “unyanyapaa ni kikwazo kwa afya ya umma. Unyanyapaa unaumiza kila mtu. Mshikamano wa kijamii unalinda kila mtu.” 

Pili amesema ni kuhakikisha teknolojia za kitabibu zinapatikana kwa kila mtu sambamba na dawa za kupunguza makali ya VVU na tatu ni kuongeza rasilimali zinazotakiwa ili kukabiliana na UKIMWI. “Uwekezaji katika UKIMWI huokoa maisha na fedha,” 

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mkutano  huo, Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, Abdulla Shahid amesema kuhakikisha huduma za afya zinapatikana kwa kila mtu ni suala la haki za binadamu ambalo linatoa hakikisho la afya kwa wote. 

“Hakuna mtu aliye salama hadi sote tuko salama. Kufanikisha malengo ya UKIMWI  kwa mwaka 2025 ni fursa ya kushirikiana na kuongeza uwekezaji katika mifumo ya afya na hatua dhidi ya majanga,” amesema Bwana Shahid.