Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Pengo la usawa linazuia utokomezaji wa janga la ukimwi: UNAIDS

Mandisa Dukashe na familia yake ni wakazi wa Eastern Cape, Afrika Kusini. Mandisa ni muuguzi na anahusika na udhibiti wa VVU na yeye mwenyewe anaishi na VVU. Lakini mumewe na binti zake wamepima VVU na hawana virusi hivyo.
AFP PHOTO/MUJAHID SAFODIEN
Mandisa Dukashe na familia yake ni wakazi wa Eastern Cape, Afrika Kusini. Mandisa ni muuguzi na anahusika na udhibiti wa VVU na yeye mwenyewe anaishi na VVU. Lakini mumewe na binti zake wamepima VVU na hawana virusi hivyo.

Pengo la usawa linazuia utokomezaji wa janga la ukimwi: UNAIDS

Afya

Tathimini iliyofanywa na Umoja wa Mataifa kuelekea siku ya ukimwi duniani ambayo kila mwaka huadhimishwa Desemba Mosi inaonyesha kuwa pengo la usawa ni kikwazo kikubwa katikia juhudi za kutokomeza janga la ukiwmi duniani. 

Kwa mujibu wa ripoti ya tathimin hiyo iliyotolewa leo na shirika la Umoja wa Mataifa la kupambana na ukimwi UNAIDS kwa mwelekeo wa sasa ulimwengu hautafikia malengo yaliyokubaliwa ya kimataifa kuhusu ukimwi.  

Lakini ripoti hiyo mpya ya UNAIDS, iliyopewa kichwa “Ukosefu wa usawa wenye hatari kubwa” inaonyesha kwamba hatua za haraka za kukabiliana na pengo la usawa zinaweza kurejesha hatua za vita dhidi ya ukimwi kwenye mstari. 

Mapema mwaka huu shirika hilo la Umoja wa Mataifa la vita dhidi ya ukimwi lilionya kwamba hatua za mapambano dhidi ya ukimwi ziko hatarini pamoja na kuongezeka kwa maambukizi mapya na kuendelea kwa vifo katika sehemu nyingi za dunia. na “kukosekana kwa usawa ni sababu kuu “. 

Pia ripoti inaonyesha jinsi viongozi wa dunia wanavyoweza kukabiliana na ukosefu huo wa usawa, na kuwataka wawe na ujasiri wa kufuata kile ambacho ushahidi unaonyesha. 

Hali halisi ya pengo la usawa 

Pengo hatari la ukosefu wa usawa kwa mujibu wa ripoti ya UNAIDS linafichua athari za kukosekana kwa usawa wa kijinsia katika hatua za vita dhidi ya ukimwi, ukosefu wa usawa katika makundi ya watu maalum, na ukosefu wa usawa kati ya watoto na watu wazima.  

Pia inaweka wazi jinsi gani vikwazo vya kifedha vinavyoongeza ugumu wa  kushughulikia ukosefu huo wa usawa. 

Ripoti inaonyesha jinsi gani kukosekana kwa usawa wa kijinsia na mila potofu vinavyorudisha nyuma hatua za kutokomeza janga la ukimwi. 

Mkurugenzi Mtendaji wa UNAIDS Winnie Byanyima amesema "Ulimwengu hautaweza kulishinda janga la ukimwi wakati unaimarisha mfumo dume. Tunahitaji kushughulikia ukosefu wa usawa unaowakabili wanawake. Katika maeneo yenye mzigo mkubwa wa VVU, wanawake waliofanyiwa ukatili na wenzi wao wanakabiliwa na uwezekano wa asilimia 50% zaidi wa kupata VVU.” 

Katika nchi 33 tangu mwaka 2015-2021 ni asilimia 41% tu ya wanawake walioolewa wenye umri wa miaka 15-24 wanaweza kufanya maamuzi yao wenyewe juu ya afya ya ngono.  

Ramani pekee yenye ufanisi ya kukomesha ukimwi, kufikia malengo ya maendeleo endelevu na kuhakikisha afya, haki na ustawi wa pamoja, ni ramani ya njia ya kupigania haki za wanawake ameongeza Bi. Byanyima.  

Ameendelea kusema kwamba “Mashirika na mavuguvugu yaa kupigania haki za wanawake tayari yako mstari wa mbele kufanya kazi hii ya ujasiri. Viongozi wanatakiwa kuwaunga mkono na kujifunza kutoka kwao.” 

Mwanamke mjamzito mwenye umri wa miaka ishirini aliyezaliwa na virusi vya Ukimwi, hutumia dawa kuzuia maambukizi kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto.
© UNICEF/UN0640796/Dejongh
Mwanamke mjamzito mwenye umri wa miaka ishirini aliyezaliwa na virusi vya Ukimwi, hutumia dawa kuzuia maambukizi kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto.

Wanawake wako hatarini zaidi Afrika 

Ripoti inasema madhara ya kukosekana kwa usawa wa kijinsia kwenye hatari za VVU kwa wanawake yanaonekana hasa katika bara la Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara, ambapo wanawake walichangia asilimia 63 ya maambukizi mapya ya VVU mwaka 2021. 

Wasichana vigori na wanawake vijana wenye umri wa miaka 15 hadi 24 wana uwezekano mara tatu zaidi wa kupata VVU kuliko wavulana na vijana wa rika moja katika eneo la Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara.  

Sababu inayochechea hali hiyo ni uwezo. Utafiti mmoja umeonyesha kuwa kuwawezesha wasichana kubaki shuleni hadi watakapomaliza elimu ya sekondari kunapunguza uwezekano wa kuambukizwa VVU kwa hadi asilimia 50%.  

Hili likiimarishwa na msaada wa uwezeshaji, hatari za wasichana kuambukizwa VVU hupunguzwa hata zaidi.  

“Viongozi wanatakiwa kuhakikisha wasichana wote wako shuleni, wanalindwa dhidi ya unyanyasaji ambao mara nyingi hurekebishwa ikiwa ni pamoja na ndoa za utotoni, na kuwa na njia za kiuchumi zinazowahakikishia mustakabali wenye matumaini.” Imesisitiza ripoti 

Hulka za mfumo dume uwafanya wanaume wasitafute msaada 

Kwa mujibu wa ripoti hulka mbayta za mfumo dume huwakatisha tamaa wanaume kutafuta huduma.  

Wakati asilimia 80% ya wanawake wanaoishi na VVU walikuwa wakipata matibabu mwaka 2021, ni asilimia 70% tu ya wanaume walikuwa kwenye matibabu.  

Kuongezeka kwa programu za kubadilisha mtazamo wa kijinsia katika sehemu nyingi za dunia ni muhimu katika kukomesha janga hili kwani kuendeleza usawa wa kijinsia kutanufaisha kila mtu. 

Ripoti inaonyesha kuwa hatua za kukabiliana na ukimwi  zinarudishwa nyuma na kukosekana kwa usawa katika upatikanaji wa matibabu kati ya watu wazima na watoto.  

Wakati zaidi ya robo tatu ya watu wazima wanaoishi na VVU wanatumia dawa za   kurefusha maisha, zaidi ya nusu ya watoto wanaoishi na VVU wanatumia dawa ya kuokoa maisha.  

Hii imekuwa na matokeo mabaya kwani mwaka 2021, watoto walichangia asilimia 4 tu ya watu wote wanaoishi na VVU lakini asilimia 15% ya vifo vyote vinavyohusiana na ukimwi hivyo kuziba pengo la matibabu kwa watoto kutaokoa maisha. 

Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Amina Mohammed (katikati kulia) alipoungana katika maandamano ya kuunga mkono siku ya wanawake huko Port Moresby Papua New Guinea.
United Nations
Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Amina Mohammed (katikati kulia) alipoungana katika maandamano ya kuunga mkono siku ya wanawake huko Port Moresby Papua New Guinea.

Unyanyapaa na ubaguzi vinakatili maisha 

Ripoti imesema kuwa ubaguzi, unyanyapaa na uharamishaji vinagharimu maisha na kuzuia ulimwengu kufikia malengo yaliyokubaliwa ya ukimwi. 

Uchambuzi huu mpya unaonyesha kuwa hakuna kupungua kwa maambukizi mapya miongoni mwa wanaume mashoga na wanaume wengine wanaofanya mapenzi na wanaume katika maeneo ya magharibi na kati mwa Afrika na kanda za mashariki na kusini mwa Afrika.  

Kukabiliana na maambukizi ya virusi, kushindwa kupiga za maendeleo kwa makundi muhimu kunadhoofisha hatua za kutokomeza ukimwi na kuainisha hatua ndogo zilizopigwa katika vita hivyo. 

Duniani kote,kwa mujibu wa ripoti hiyo ya UNAIDS  zaidi ya nchi 68 bado zinaharamisha mahusiano ya ngono ya jinsia moja.  

Uchambuzi mwingine ulioangaziwa katika ripoti hiyo umegundua kuwa wanaume mashoga na wanaume wengine wanaofanya mapenzi na wanaume wanaoishi katika nchi za Kiafrika zenye sheria kandamizi zaidi wana uwezekano mdogo wa kujua hali zao za VVU mara tatu zaidi kuliko wenzao wanaoishi katika nchi zenye ukandamizaji mdogo wa kisheria , ambapo maendeleo yanakua kwa haraka zaidi. Wafanyabiashara ya ngono wanaoishi katika nchi ambazo biashara ya ngono imeharamishwa wana nafasi kubwa mara 7 ya kuishi na VVU kuliko katika nchi ambazo biashara ya ngono imehalalishwa kwa kiasi fulani. 

Kuna nchi zilizopiga hatua 

Ripoti inaonyesha maendeleo dhidi ya ukosefu wa usawa yanawezekana na inaangazia maeneo ambayo hatua dhidi ya ukimwi zimepata maendeleo makubwa. Kwa mfano, wakati tafiti miongoni mwa makundi muhimu mara nyingi huangazia huduma za chini kati ya watu muhimu, kaunti tatu nchini Kenya zimefikia kiwango cha juu cha matibabu ya VVU miongoni mwa makahaba wa kike kuliko miongoni mwa idadi ya jumla ya wanawake wenye umri wa miaka kati ya 15-49.  

Hii imesaidiwa na programu dhabiti za VVU kwa miaka mingi, ikijumuisha huduma zinazoongozwa na jamii. 

Bi Byanyima amesema “Tunajua la kufanya kumaliza ukosefu wa usawa. Ni kuhakikisha kwamba wasichana wetu wote wako shuleni, salama na wenye nguvu. Kukabili unyanyasaji wa kijinsia. Kusaidia mashirika ya wanawake. Kukuza nguvu za kiume zenye afya kucha kuchukua nafasi ya tabia zenye madhara zinazozidisha hatari kwa kila mtu. Kuhakikisha huduma kwa watoto wanaoishi na VVU zinawafikia na kukidhi mahitaji yao, kuziba pengo la matibabu ili tukomeshe ukiwmi kwa watoto kabisa. Kutowanyima haki watu walio katika mahusiano ya jinsia moja, wafanyabiashara ya ngono, na watu wanaotumia dawa za kulevya, na kuwekeza katika huduma zinazoongozwa na jamii zinazowawezesha kujumuishwa hii itasaidia kuvunja vizuizi vya huduma na kuokoa mamilioni ya watu." 

Changamoto za fedha za ufadhili 

Ripoti imesisitiza kwamba uwekezaji mpya wa kushughulikia pengo la usawa unaohusiana na VVU unahitajika haraka.  

Wakati ambapo mshikamano wa kimataifa na kuongezeka kwa ufadhili kunahitajika zaidi, nchi nyingi za kipato cha juu zinapunguza misaada kwa afya ya kimataifa.  

Mwaka 2021, ufadhili uliopatikana kwa programu za VVU katika nchi za kipato cha chini na cha kati ulikuwa pungufu wa dola bilioni 8.  

Kuongezeka kwa usaidizi wa wafadhili ni muhimu ili kurudisha hatua za kupambana na VVU kwenye mstari. 

Pia ripoti imeongeza kuwa bajeti zinahitaji kuweka kipaumbele kwa afya na ustawi wa watu wote, haswa watu walio hatarini ambao wameathiriwa zaidi na ukosefu wa usawa unaohusiana na VVU.  

Nafasi ya kifedha kwa ajili ya uwekezaji wa afya katika nchi za kipato cha chini na cha kati unahitaji kupanuliwa, ikiwa ni pamoja na kufuta madeni makubwa na kutathinini ushuru unaoendelea kuongezeka.  

Kukutokomeza ukimwi ni rahisi sana kuliko kutokomesha ukimwi.